1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Rais Kenyatta mbele ya ICC

8 Oktoba 2014

Rais wa Kenya anafika mbele ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu mjini The Hague akiwa kama raia tu na sio rais.Kesi huenda ikasitishwa-ingawa nguvu za korti ya ICC ingebidi ziimarishwe anasema Andrea Schmidt

https://p.dw.com/p/1DRbE
Uhuru Kenyatta akiondoka Nairobi kama raia wa kawaida kuelekea The HaguePicha: REUTERS/N. Khamis

Kesi ya kihistoria dhidi ya rais wa kwanza aliyeko madarakani inaonyesha kumalizika hata kabla ya kuanza.Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC mjini The Hague, Fatou Bensouda tangu wiki kadhaa zilizopita amekua akitaka kesi dhidi ya rais Uhuru Kenyatta wa Kenya iakhirishwe kwa muda usiojulikana kutokana na ukosefu wa ushahidi. Kikao cha leo kitakachoamua juu ya hatima ya kesi hiyo ambacho rais wa Kenya ametakiwa ahudhurie binafsi kinadhihirika kama mbinu za mwisho za kutunisha misuli katika kadhia hii.Kesi dhidi ya rais Uhuru Kenyatta wa Kenya tangu mwanzo haikuwa katika nyota njema. Juhudi za usumbufu zilizoanza tangu wakati wa mwendesha mashtaka mkuu wa zamani wa ICC Moreno Ocampo, kutafuta ushahidi wa machafuko ya mwaka 2007 yaliyopelekea zaidi ya watu 1000 kuuwawa na malaki wengine kuyapa kisogo maskani yao, zimekuwa zikikorofishwa nchini Kenya. Kila wakati unapozidi kupita mashahidi nao wanazidi kujitoa,wanaonekana wanachokisema si cha kuaminika au wanatoweka kabisa.

Nyaraka muhimu zimezuwiliwa na zilizotolewa hazikukamilika. Na sasa rais mwenyewe wa nchi hiyo anasema anakwenda mahakamani lakini sio kama rais, bali kama raia wa kawaida-pengine kwa kufika The Hague anataka kuepusha tu asikamatwe kwa waranti wa kimataifa.

Mwaka uliopita kesi ho iliakhirishwa mara kadhaa.Madai ya mwendesha mashtaka mkuu Bensouda kutaka akabidhiwe hati za shughuli za benki, yamekataliwa na Kenyatta ingawa kila wakati amekuwa akisema atashirikana na korti kuu ya kimataifa mjini The Hague. Mashtaka dhidi yake ni pamoja na kuhusika japo si moja kwa moja na mipngo ya kuandaa mauwaji,kutimuliwa watu majumbani mwao na kuwasaidia kwa fedha wahalifu.

Pindi kesi ikisitishwa litakuwa pigo kubwa kwa wahanga na familia zao

Pindi kesi ikivunjika kwasababu ya kutokuwepo ushahidi wa kutosha au kuakhirishwa kwa muda usiojulikana,hilo litakuwa pigo kubwa sio tu kwa mahakama ya kimataifa ya uhalifu bali kwa suala jumla la haki ulimwenguni. Korti kuu ya kimataifa imeundwa ili kukomesha mitindo ya kutoandamwa kisheria wale wanaofanya visa vya uhalifu dhidi ya ubinaadam.

Mataifa 122 yametia saini mkataba wa Roma uliopelekea kuundwa mahakama hiyo ya kimataifa na Kenya imetia saini Marchi 15 mwaka 2005.Mashirika kadhaa ya huduma za jamii barani Afrika yameshiriki katika kubuniwa mkataba huo wa Roma kwasbabu hawakutaka tena kunyamaza wanapoona jinsi haki za binaadam zinavyoendewa kinyume.

Kenyatta sawa na watuhumiwa wote wengine ana haki ya kutotiwa hatiani kabla ya kukutikana na hatia.Lakini kwa makundi yanayopigania haki za binaadam,wahanga na jamaa zao nchini Kenya litakuwa balaa kubwa kama kesi itashindikana kwasbabu ya ukosefu wa ushahidi.Walijiwekea matumaini ya haki kuiona mahakama ya kimataifa ya uhalifu ikifichua ukweli na kufanya kila liwezekanalo kuwaandama waliofanya uhalifu dhidi ya ubinaadam.

Matokeo ya kesi zilizoendeshwa na korti hiyo hadi sasa ni finyu.Ndo kusema korti kuu ya kimtaifa ni sawa na chui asiyekuwa na meno?

Deutsche Welle Afrika Kisuaheli Andrea Schmidt Kommentar
Mkuu wa Matangazo ya Kiswahili ya DW,Andrea SchmidtPicha: DW

Korti kuu ya kimataifa ya uhalifu haina badala.Mitindo ya kutoandamwa kisheria wahalifu wa vita,wauwaji na wanaochochea machafuko lazma ikome. Wahalifu hawastahiki kujisikia salama.Wahanga na familia zao wanabidi wahakikishiwe kwamba korti ya dunia ni chombo huru na cha haki na halifu, naawe na cheo cha aina gani, atafikishwa mahkmani na kuhukumiwa.

Mwandishi:Andrea Schmidt/Hamidou Oummilkheir.

Mhariri:Mohamed Abdul-Rahman