1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Obama apaswa kwenda Ferguson

27 Novemba 2014

Maandamano Marekani kufuatia uamuzi wa baraza la mahakama huko Ferguson yanaonyesha kwamba suala la ubaguzi wa rangi nchini humo bado halikumalizika.Michael Knigge wa DW anataka Rais Barack Obama aende Ferguson.

https://p.dw.com/p/1DuVV
Polisi wakikabiliana na waandamanaji Ferguson.(26.11.2014)
Polisi wakikabiliana na waandamanaji Ferguson.(26.11.2014)Picha: Reuters/L. Jackson

Kwa hakika hatua kadhaa zimepigwa katika kipindi cha miongo iliopita lakini bado kuna ukosefu wa usawa kati ya weusi na wazungu katika nyanja nyingi za maisha ya wananchi wa Marekani.Rais Obama anajuwa fika kwamba suala hilo haliwezi kumalizika hivi hivi tu kwa urahisi au kurekebisha hali kwa chochote atakachofanya sasa baada ya kutolewa kwa uamuzi wa baraza la mahakama katika kesi ya kuuwawa kwa kijana mweusi kulikofanywa na polisi mzungu huko Ferguson.

Akiwa kama mwanasheria wa zamani aliye elimika katika chuo kikuu chenye hadhi anajuwa pia kwamba hata kama matokeo ya utaratibu uliotumika kutowa uamuzi huo ulikuwa na utata kiasi gani kwa sasa hauwezi kuupinga kisheria.Na yumkini Obama ambaye mara nyingi anaelezewa kama bashirifu katika taifa la kipindi cha baada ya ubaguzi inamuwia vigumu kuonyesha msimamo wake.

Kila kauli atakayoitowa,kila hisia atakayoionyesha itachambuliwa na kuzungumziwa mara elfu.Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni nchi hiyo imegawika vibaya kutokana na uamuzi wa kadhia ya Ferguson.

Wajibu wa kihistoria

Hata hivyo Barack Obama anatakiwa kuchukuwa hatua. Akiwa kama rais wa kwanza mweusi mama yake akiwa ni mzungu amejaaliwa kuliko mtu mwengine yoyote yule kuyachambuwa matukio ya Ferguson kwa mapana yake kwa kuzingatia uhusiano wa kibaguzi unaoendelea nchini Marekani.

Obama ana wajibu wa kihistoria kufanya hivyo. Taarifa zake kame kufuatia uamuzi wa baraza la mahakama kuhusiana na kadhia ya Ferguson na kutokana na umuhimu mkubwa sana wa suala hilo haitokuwa sawa kwa dhima yake kama rais.

Rais Obama aliwahi kutowa hotuba nzito kuhusiana na uhusiano na ulimwengu wa Kiarabu mjini Cairo hapo mwaka 2009 au kufuatia mauaji ya holela yaliofanyika shule huko Newton Marekani mwaka 2013.

Suala la ubaguzi katika kampeni ya uchaguzi

Michael Knigge wa Deutsche Welle (DW).
Michael Knigge wa Deutsche Welle (DW).Picha: DW/P. Henriksen

Hata hivyo hotuba yake kuu ya mwisho kuhusu suala la ubaguzi aliitowa kitambo mwaka 2008 wakati huo akiwa kama mgombea wa urais kufuatia matamshi yaliyozusha utata yaliyotolewa na mchungaji wake wa zamani Jeremiah Wright ambapo alikuwa chini ya shinikizo kubwa la wananchi kuyatolea maelezo.

Kutokana hotuba nzito yenye ushawishi kuhusu masuala ya ubaguzi Obama alifanikiwa wakati huo kugeuza mkondo na kunusuru ugombea wake wa wadhifa wa urais.

Kufuatia matukio ya Ferguson na maandamano ya taifa zima Obama hivi sasa ni kama alivyokuwa mwaka 2008 akishinikizwa kushughulikia tatizo la ubaguzi.Tafauti na wakati huo safari hii sio kwa maslahi yake binafsi bali kwa maslahi ya taifa.Kama rais hivi sasa anatakiwa aonyeshe sifa ya uongozi na kulishughulikia suala hilo ipasavyo.

Wakati umefika kwa Obama kwenda Ferguson.Hotuba kwa wakaazi wa eneo hilo haitondowa tatizo la ubaguzi lakini angalau hicho ndicho wanachokitaraji Wamarekani kutoka kwa rais wao.Na sio wao tu hata dunia inaangalia.

Mwandishi:Michael Knigge/ Mohamed Dahman

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman.