1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Weltklasse-Prozess

Elizabeth Shoo12 Septemba 2014

Hatimaye mahakama ya Afrika Kusin imemkuta mwanariadha Oscar Pistorius na hatia ya kuua bila kukusudia. Kwa maoni ya mwandishi wetu Claus Stäcker, kesi hii itabadilisha maisha ya nyota huyo daima.

https://p.dw.com/p/1DBFP
Oscar Pistorius akisikiliza hukumu yake
Picha: Reuters/P. Magakoe

Oscar Pistorius sio muuaji! Mashabiki wa nyota huyu wa michezo bila shaka watafarijika kusikia habari hiyo. Hawakutaka kuamini kwamba mwanariadha huyu mlemavu angeweza kumuua mpenzi wake wa kike kikatili. Na kila aliyemuona kizimbani jinsi alivyoonyesha kusikitika, alivyolia na hata kutapika, anaamini kuwa Pistorius alikuwa anaonyesha hisia za kweli. Hakuwa anaigiza. Kortini mawakili hawakusita kudhihirisha kila aina ya ushahidi, hata taarifa za siri, kuhusu uhusiano wa Pistorius na mpenzi wake Reeva Steenkamp.

Ingawa Pistorius hajapata hukumu kali sana, maisha ya mwanariadha huyo yamevunjika. Kabla ya usiku ule alipomfyatulia mpenzi wake risasi na kumuua, Pistorius alikuwa nyota wa michezo ya walemavu. Makampuni makubwa yalimteua kwa ajili ya kufanya matangazo ya bidhaa zao. Leo hii, mabango ya matangazo yalikuwa yanamwonyesha mwanamichezo huyo na yaliyokuwa yametapakaa Johannesburg na Cape Town hayapo tena. Wafadhili wametafuta wanamichezo wengine kwa ajili ya matangazo yao. Maisha ya Pistorius hayana mwelekeo tena. Atabakia kuwa mtu ambaye habari za maisha yake zinachambuliwa kwenye magazeti ya udaku.

Matajiri wana haki zaidi?

Lakini suala la muhimu sio maumivu binafsi anayoyapata Pistorius kutokana na kesi hii. Miaka 20 baada ya ubaguzi wa rangi kupigwa marufuku Afrika Kusini jaji Mwafrika mweusi ametoa hukumu ya haki bila kuzingatia kwamba Pistorius ni Mwafrika Kusini Mzungu. Jaji Thokozile Masipa hakujali shinikizo kutoka kwa vyombo vya habari na kwa umma uliokuwa unaifuatlia kesi hii. Alitoa hukumu yake kwa utulivu na bila papara.

Claus Stäcker, mkuu wa idhaa za Afrika za DW
Claus Stäcker, mkuu wa idhaa za Afrika za DWPicha: DW

Ni kweli kwamba jaji Masipa hakuweza kujibu swali iwapo ni jambo la kawaida kwa raia wa Afrika Kusini kuweka bunduki karibu na wanapolala na kuifyatua mara wanapohisi tu kuwa labda mwizi ameingia kwenye nyumba. Na swali lingine ni iwapo matajiri wana nafasi nzuri zaidi wanaposimama kizimbani kwasababu wana uwezo wa kuajiri mawakili bora zaidi.

Raia wa Afrika Kusini wameifuatilia kesi hii kwa ukaribu. Lakini mwisho wa siku wanachojali zaidi ni kuona kwamba hata wahalifu wengine wanafikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa haraka. Hii ni kwasababu si jambo la kawaida kwa mauaji kutokea katika majumba ya kifahari kama ambapo walikuwa wakiishi Pistorius na Steenkamp. Lakini ni suala linalotokea kila siku katika makaazi ya watu maskini.

Mwandishi: Claus Stäcker

Tafsiri: Elizabeth Shoo

Mhariri: Saumu Yusuf