1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mambo yazidi kuwa magumu kwa Borussia

20 Oktoba 2014

Bayern Munich haina mpinzani katika Bundesliga msimu huu, kuporomoka kwa Borussia Dortmund kunaendelea , baada ya kukubali kipigo cha nne mfululizo ilipopambana na FC Kolon Jumamosi(18.10.2014).

https://p.dw.com/p/1DYnN
Fussball 1. Bundesliga 8. Spieltag 1. FC Köln - Borussia Dortmund
Marco Reus wa Borussia DortmundPicha: picture-alliance/dpa/Rolf Vennenbernd

Viongozi wa ligi ya Ujerumani Bundesliga Bayern Munich ambao pia ni mabingwa watetezi wameonesha kuwa hawana mpinzani baada ya kuibamiza Werder Bremen kwa mabao 6-0.

Bayern imeshinda michezo sita kati ya nane ya msimu huu na wana pointi 20 hadi sasa wakati Borussia Moenchengladbach , ambayo imeishinda Hannover kwa mabao 3-0 ikisogea hadi nafasi ya pili. Werder Bremen haikuonekana kuisumbua Bayern kabisa katika mchezo huo kama anavyothibitisha Sebastian Prödl mchezaji wa kati wa Bremen.

Bundesliga 8. Spieltag München - Bremen
Wachezaji wa bayern wakijipongeza baada ya kupata baoPicha: Hassenstein/Bongarts/Getty Images

"Bila shaka, kupata pointi hapa ni kitu kigumu mno, ambapo ni sawa na kutowezekana. Ni jinsi tulivyoshindwa hapa leo , ndio tunashindwa kuelewa na hatuwezi kuchukua chochote cha maana. Haisaidii kabisa. Tumeshindwa leo na tulikuwa timu mbovu kabisa. Bayern imekuwa na siku nzuri, sisi tulikuwa na siku mbaya , na ndio sababu tulistahili kipigo hicho."

Makamu bingwa wa msimu uliopita Borussia Dortmund iliangukia pua tena kwa kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya FC Kolon , kipigo cha tano katika kampeni ya msimu huu , kipigo ambacho kimeiweka Borussia katika nafasi ya 14 ya msimamo wa ligi, ikiwa na pointi saba tu kibindoni. Kocha wa FC Kolon Peter Stöger anasema amefurahishwa mno na ushindi huo.

"Ni hisia nzuri sana, kwamba kwa mara ya kwanza tumepata bao nyumbani kwetu na mchezo dhidi ya BVB , timu ngumu kabisa , tumeweza kushinda, hilo ni jambo la pekee kabisa. Ilikuwa muhimu kwetu baada ya wiki zilizopita, kucheza vizuri, lakini hatukupata pointi. Ni hali nzuri kupata pointi katika uwanja wetu, kama unavyoona , kwamba watu wamefurahi sana."

Fußball Bundesliga (2. Spieltag) VfB Stuttgart gegen 1. FC Köln Peter Stöger
Kocha wa FC Koln Peter StögerPicha: Getty Images

Kocha Roberto di Matteo ameanza kazi yake mpya akiwa na Schalke 04 kwa mafanikio , kwa ushindi dhidi ya Hertha Berlin kwa mabao 2-0 kwa magoli yaliyofungwa na Julian Draxler na Klaas-Jan Huntelaar. Di Matteo amesema amefurahishwa na ushindi lakini kuna mambo mawili matatu ya kurekebisha.

"Niko hapa sasa kwa siku kumi na kwa kweli sijafanyakazi na wachezaji wote, kwa kuwa wengi walikuwa katika timu zao za taifa. Tumeona kidogo utaratibu wa timu. Tunahitaji kuufanya kuwa bora zaidi. Hakuna anayetarajia , kwamba tungefanya kila kitu sahihi kabisa. Lakini nafikiri , ulikuwa msingi mzuri kwa ajili ya hapo baadaye."

Jana Jumapili (19.10.2014)Paderborn iliiadhibu Eintracht Frankfurt kwa kuifunga mabao 3-1 na Hamburg ikatoka sare na Hoffenheim kwa kufungana bao 1-1.

Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / afpe / rtre
Mhariri: Josephat Charo