1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano yafikiwa Burkina Faso

Mjahida14 Novemba 2014

Jeshi la Burkina Faso limefikia makubaliano na vyama vya upinzani, mashirika ya kiraia, na viongozi wa kidini juu ya kipindi cha mpito cha kukabidhi madaraka kwa raia, wiki mbili baada ya kujiuzulu rais Blaise Compaore

https://p.dw.com/p/1Dmnz
Luteni Kanali Issac Zida akikabidhiwa pendeklezo la serikali ya mpito
Luteni Kanali Issac Zida akikabidhiwa pendeklezo la serikali ya mpitoPicha: picture-alliance/dpa/R. Zoeringre

Wajumbe katika mazunguzo yaliopelekea maafikiano hayo wamesema, chini ya makubaliano hayo, rais wa kipindi cha mpito atachaguliwa na kikundi maalum cha uchaguzi. Kisha rais atatarajiwa kumchagua waziri mkuu ama kutoka upande wa raia au kijeshi ambaye ataongoza serikali ya mpito itakayokuwa na mawaziri 25.

Pia kiongozi wa kiraia ataongoza bunge litakalokuwa na wajumbe 90 litakalojulikana kama baraza la kitaifa la mpito. Aidha makubaliano hayo yanaweka wazi kabisa, kwamba hakuna mjumbe wowote wa baraza la mawaziri la serikali ya mpito atakayeruhusiwa kugombea katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka 2015.

Kulingana na muandishi wa shirika la habari la AFP, taarifa ya makubaliano hayo yaliyofanyika hapo jana jioni zimepokewa kwa shagwe kuu huku wimbo wa taifa ukipigwa baada ya kikao cha mazungumzo.

Rais wa Zamani wa Burkina Faso Blaise Compaore
Rais wa Zamani wa Burkina Faso Blaise CompaorePicha: picture alliance/AP Photo/R. Blackwell

Ablasse Ouedraogo, waziri wa zamani wa masuala ya kijamii wa Burkina Faso, amesema kwa sasa mustakbali wa nchi hiyo umelindwa huku akisema mpango huo utasaidia kufungua nafasi au fursa mpya kwa ajili ya vijana. Kwa upande wake Adama Kanazoe, mwanasiasa kijana anayeongoza muungano wa upinzani wa vijana amesema mpango huo umeonesha demokrasia kamili na kukuwa kwa siasa za nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Rais wa Senegal asema ana matumaini rais wa mpito atapatikana

Akizungumzia makubaliano yaliofikiwa, Rais Macky Sall wa Senegal ana imani katika siku kadhaa zijazo rais wa mpito atapatikana na taifa hilo litaendelea mbele kwa manufaa ya raia wake.

"Nina matumaini kwamba, katika masaa machache au siku chache zijazo, uamuzi thabiti utachukuliwa kwa kumchagua rais wa kuongoza kipindi cha mpito na pia kuwachagua wale wote wanaopaswa kuchaguliwa," alisema rais Macky Sall.

Rais wa Senegal Macky Sall
Rais wa Senegal Macky SallPicha: AP

Blaise Compaore alilazimika kujiuzulu na kukimbilia Cote d'Ivoire baada ya maandamano makubwa dhidi yake yaliopinga jaribio lake la kubadilisha katiba ili aendelee kuiongoza nchi hiyo baada ya miaka 27 ya utawala wake.

Muda mfupi baadaye Luteni Kanali Isaac Zida, aliye na umri wa miaka 49 akajitangaza kama kiongozi mpya atakayeiongoza nchi hiyo ilio na idadi ya watu milioni 17 na koloni la zamani la Ufaransa.

Lakini jeshi hilo limekuwa likishinishikizwa kimataifa kukabidhi madaraka kwa serikali ya mpito inayoongozwa kiraia.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef