1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maiti za wahanga wa MH17 zapelekwa Uholanzi

23 Julai 2014

Ndege ya kwanza inayobeba majeneza 14 yaliyo na miili ya waliokufa katika mkasa wa ndege ya Malaysia iliyodunguliwa wiki iliyopita Mashariki mwa Ukraine imeondoka kutoka uwanja wa ndege wa Kharkiv, kuelekea Uholanzi leo

https://p.dw.com/p/1Ch0b
Picha: Reuters

Familia za waathiriwa hao, viongozi wa Uholanzi na wawakilishi wa Malaysia wanatarajiwa kuipokea miiili hiyo huku benderea zikikipeperushwa nusu mlingoti katika siku ya kitaifa ya maombolezi Uholanzi ambayo imewapoteza raia wake 193 waliokuwa katika ndege hiyo iliyodunguliwa mashariki mwa Ukraine.

Uholanzi na nchi nyingine ambazo ziliwapoteza raia wao katika ndege ya Malaysia MH17 zinapendekeza kutuma maafisa wa polisi kulilinda eneo la mkasa mashariki mwa Ukraine.

Polisi wa kimataifa kutumwa Ukraine

Rais wa Ukraine Petro Poroshenko amesema pendekezo hilo limetolewa na waziri mkuu wa Uholanzi Mark Rutte ili kuhakikisha uchunguzi huru kutoka kwa wataalamu wa kimataifa unaendeshwa kubaini chanzo cha ajali hiyo.

Jeshi likitoa heshima ya mwisho kwa waliokufa katika ajali ya ndege ya Malaysia
Jeshi likitoa heshima ya mwisho kwa waliokufa katika ajali ya ndege ya MalaysiaPicha: Reuters

Maafisa wa Marekani wamesema ndege hiyo iliyokuwa ikitokea Amsterdam kuelekea Kuala Lumpur ilidunguliwa kimakosa na waasi wanaoungwa mkono na Urusi wanaotaka kujitenga kwa eneo la mashariki mwa Ukraine.

Wachunguzi wa mkasa huo wanatumai kuwa visanduku viwili vyeusi vya kunakili mawasiliano ya ndege ambavyo vimetumwa Uingereza hii leo kwa uchunguzi vitasaidia kung'amua ukweli kuhusu ajali hiyo iliyosababisha vifo vya watu wote 298 waliokuwa ndani.

Ushahidi uliokusanywa kufikia sasa na maafisa wa kijasusi wa Marekani unadokeza kuwa waasi wa Ukraine ndiyo walirusha kombora aina ya SA 11 kutoka ardhini kuelekea angani iliyoidungua ndege hiyo ya Malaysia Alhamisi iliyopita lakini bado haijabainika ni nani hasa aliyelifyatua kombora hilo na kwanini.

Inaaminika huenda kombora hilo lilirushwa na kundi la wapiganaji wasio na ujuzi wa kutosha kushughulikia makombora na ndiposa vidokezo hivyo vya awali vinaashiria ilikuwa ni kitendo ambacho hakikusudia kuidungua ndege ya abiria.

Urusi yakanusha kuhusika

Urusi ambayo inashutumiwa na jumuiya ya kimataifa kwa kuwapa silaha na mafunzo waasi hao wa mashariki mwa Ukraine imekanusha kuwa iliwapa kombora hilo lililotumika kuidungua ndege hiyo.

Rais wa Ukraine Petro Poroshenko katika eneo la mkasa
Rais wa Ukraine Petro Poroshenko katika eneo la mkasaPicha: picture-alliance/dpa

Licha ya waasi hao kukubali kuikabidhi miili 200 ya waathiriwa na visanduku viwili vyeusi kwa wachunguzi wa kimataifa,bado hatma ya miili mingine ya waathiriwa wa ajali hiyo haijulikani.

Wachunguzi wa kimataifa wa shirika la usalama na ushirikiano barani Ulaya OSCE wanasema mabaki ya miili mingine ambayo imesalia katika eneo la mkasa ambayo hayajachukuliwa na sehemu ya mabaki ya ndege hiyo yameondolewa kutoka eneo la mkasa.

Waziri mkuu wa Australia Tony Abbott amesema haijulikani wazi ni miili mingapi iliyowasili katika mji wa Kharkiv na ni mingapi iliyosalia katika eneo la mkasa na kuongeza kuwa huenda miili mingine isiwahi kupatikana iwapo uchunguzi kamili hautafanywa katika eneo la mkasa na maeneo yaliyo karibu.

Mwandishi:Caro Robi/ap/Afp

Mhariri:Josephat Charo