1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahasimu wa Sudan Kusini wasaini makubaliano

Mohammed Khelef22 Januari 2015

Viongozi wa pande hasimu nchini Sudan Kusini wamesaini makubaliano ya kuimairisha juhudi za kukomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe mjini Arusha, Tanzania, wakishuhudiwa na viongozi kadhaa wa Afrika.

https://p.dw.com/p/1EOu8
Katika picha hii ya tarehe 20 Oktoba 2014, Rais Jakaya Kikwete anaonekana akiwa katikati ya Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini (kushoto) na kiongozi wa waasi, Riek Machar.
Katika picha hii ya tarehe 20 Oktoba 2014, Rais Jakaya Kikwete anaonekana akiwa katikati ya Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini (kushoto) na kiongozi wa waasi, Riek Machar.Picha: AFP/Getty Images

Rais Salva Kiir na kiongozi wa waasi, Riek Machar, walisaini makubaliano hayo ambayo sasa yanazileta pamoja kambi mbili zinazopingana ndani ya chama tawala cha Vuguvugu la Ukombozi wa Sudan Kusini (SPLM).

Akizungumza baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Benard Membe, aliupongeza "uongozi wa SPLM kwa kufikia makubaliano ya kukiunganisha tena chama chao kwa maslahi ya Sudan Kusini."

Mazungumzo hayo yalikuwa chini ya usimamizi wa Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, huku viongozi kadhaa wa mataifa jirani wakihudhuria kuhakikisha kuwa mahasimu hao wawili wanasaini makubaliano hayo.

Hadi sasa, hakuna taarifa za vipengele vya makubaliano hayo zilizotolewa, lakini makundi hasimu yanayowania udhibiti wa siasa za nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta yameyavunja makubaliano ya kusitisha mapigano mara tano ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

IGAD yaendeleza juhudi za mapatano

Mazungumzo hayo nchini Tanzania yalikuwa sehemu ya juhudi za pamoja kusaka makubaliano zilizoanzishwa na Jumuiya ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Nchi za Mashariki na Pembe ya Afrika (IGAD) kwenye mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.

Mkutano wa upatanishi chini ya IGAD mwezi Novemba 2014 mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Mkutano wa upatanishi chini ya IGAD mwezi Novemba 2014 mjini Addis Ababa, Ethiopia.Picha: picture-alliance/Minasse Wondimu/Anadolu Agency

Mazungumzo mengine ya IGAD yanatazamiwa kufanyika kandoni mwa mkutano wa kilele wa viongozi wa mataifa wanachama wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa mwishoni mwa mwezi Januari.

Kwa mara ya kwanza, mapigano yalizuka kwenye taifa hilo jipya kabisa barani Afrika mwezi Disemba 2013, baada ya Kiir kumtuhumu makamu wake wa zamani, Machar, kutaka kumpindua. Baadaye yakageuka kuwa vita vya kikabila ndani ya SPLM na kuchochea mapigano ya kulipizana kisasi na mauaji nchi nzima yaliyopelekea vifo vya maelfu ya watu na kuirejesha nchi hiyo kwenye ukingo wa njaa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Kiir na Machar walikutana kwa mara ya mwisho mwezi Novemba mjini humo, ambako walikubaliana kusitisha mara moja vita, lakini makubaliano hayo yalivunjwa masaa machache tu baadaye.

Mapigano makali yaliripotiwa mapema wikik hii kati ya jeshi la waasi kwenye jimbo la kati la Lakes na siku ya Jumanne, msemaji wa jeshi, Philip Aguer, alivilaumu vikosi vya Machar kwa kukiripua kinu cha kuzalishia mafuta kwenye jimbo la Unity.

Hakuna orodha rasmi ya vita iliyorikodiwa na serikali au waasi au Umoja wa Mataifa, lakini taasisi ya kushughulikia mizozo duniani, International Crisis Group, inakisia kuwa kiasi cha watu 50,000 wameshapoteza maisha hadi sasa.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP/AP
Mhariri: Saumu Yussuf