1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano ya Hong Kong ,Afghanistan na Wakimbizi Magazetini

1 Oktoba 2014

Maandamano ya wapenda demokrasia Hong Kong, hali nchini Afghanistan na kashfa iliyosababishwa na kudhalilishwa wakimbizi katika jimbo la Nord Rhine Westphalia ni miongoni mwa mada magazetini

https://p.dw.com/p/1DO9h
Wapendsa demokrasia waendelea kuandamana Hong KongPicha: picture-alliance/dpa/Dennis M. Sabangan

Tuanzie barani Asia na hasa Hong Kong ambako waandamanaji wanaonyesha kupania huku serikali ya China mjini Beijing ikikataa kuridhia. Ndio kusema kilio cha Hong Kong kitayafikia maeneo mengine pia ya nchi hiyo yenye wakaazi wengi zaidi ulimwenguni?Suala hilo linajiuliza gazeti la "Saarbrücker Zeitung" na kusema:"Idadi kubwa ya wakaazi wa China hawajui chochote kuhusu maandamano ya Hong Kong. Ndio maana ni ujinga kuamini cheche za Hong Kong zitaenea kwengineko. Wakaazi wa Hong Kong wanapigania masilahi yao. Wanataka waziri mkuu achaguliwe bila ya ushawishi wa China. Wako tayari kujadiliana ili kulifikia lengo hilo. Lakini serikali kuu mjini Beijing haiko tayari kufikia maridhiano,haijazowea kufanya hivyo. Na kila wakati ambapo Beijing na vibaraka wake walioko Hong Kong wataendelea kuvuta kamba ndipo nao waandamanaji watakapozidi kumiminika majiani. Kwa hivyo kuna kila dalili ya malumbano na sio maridhiano.

Afghanistan baada ya 2014

Afghanistan pia imemulikwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo hii na kuchunguza hali jumla namna ilivyo wakati huu ambapo vikosi vya kimataifa vinavyoongozwa na jumuia ya kujihami ya NATO vinajiandaa kuihama nchi hiyo.Gazeti la "Volksstimme" linaandika:"Ni kweli kabisa,nchi za magharibi hazijafanikiwa pakubwa nchini Afghanistan. Wataliban bado wanaendelea kuwatisha watu katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo na katika sehemu nyingi watu wanendelea kuishi katika hali ya umaskini. Zaidi ya hayo rushwa imeenea haraka nchini humo kuliko hata fikra ya kuanzisha mfumo wa demokrasia na utawala unaoheshimu sheria.Na ndio maana kuna umuhimu mkubwa kwa NATO kutoitelekeza nchi hiyo na watu wake, badala yake serikali ya Afghanistan isaidiwe angalao kwa miaka miwili inayokuja kuunda jeshi lake ili angalao liweze kurejesha nidhamu na usalama.Hajakosea waziri wa zamani wa ulinzi Peter Struck wa kutoka chama cha SPD aliposema usalama wa Ujerumani na nchi za magharibi unalindwa kutokea Afghanistan. Ingawa Syria na Iraq pia zimeongezeka hivi ssa.Na hili ndilo somo lililotokana na mashambulio ya kigaidi ya septemba 11 mwaka 2001:Nchi ikishindwa,uhalifu unaweza kuenea na kuutisha ulimwengu mzima."

Kabul Anschlag 01.10.2014
Shambulio la bomu katika mji mkuu wa Afghanistan-KabulPicha: Reuters/Omar Sobhani

Kashfa ya kudhalilishwa wakimizi

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu kashfa ya kudhalilishwa wakimbizi katika vituo vya mapokezi katika jimbo hili la Nord Rhine Westphalia. Watumishi wa shirika la usalama wanaotuhumiwa kuhusika na visa hivyo vya kuwadhalilisaha wakimbizi,wamefukuzwa kazini na wanafunguliwa mashtaka. Hatua kali zimechukuliwa kuhakikisha visa kama hivyo havitokee tena humu nchini. Lakini Gazeti la Nürnberger Nachrichten linajiuliza, ni hivyo tu? Gazeti linaendelea kuandika:"Hasha.Yeyote ambae katika kampeni za uchaguzi anapendelea kutumia maneno ya kibaguzi, asistaajabu akiona hisia za chuki dhidi ya wageni zinaanza upya kuchomoza humu nchini.Anaewazuwia wakimbizi wasiruhusiwe kuishi katika nyumba za kibinafsi,ajue tu kwmba matokeo yake yatakuwa kukabailiana na hali isiyoridhisha katika vituo vya mapokezi vilivyojaa watu kupita kiasi.

Siegerland-Kaserne Flüchtlingsheim Flüchtlinge Burbach
Kituo cha kuwapokea wakimbizi cha BurbachPicha: picture-alliance/dpa/Federico Gambarini

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Khelef