1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandalizi ya London Marathon yaendelea

23 Machi 2015

Gwiji wa mbio za masafa marefu wa Ethiopia Kenenisa Bekele amejiondoa katika mbio za marathon za London zitakazoandaliwa mwezi ujao, kutokana maumivu ya mishipa ya miguu.

https://p.dw.com/p/1EvfZ
Äthiopien Kenenisa Bekele
Picha: picture-alliance/dpa

Bekele ambaye ni bingwa mara kadhaa wa Olimpiki na ulimwengu katika mbio za ndani ya uwanja, alikuwa ametarajiwa kushiriki kwa mara ya kwanza katika mbio za marathon jijini London mnamo Aprili 26, lakini akaumia wakati akishiriki katika mbio za marathon za Dubai mwezi Januari.

Waandalizi wa mbio za London wametangaza washiriki wapya wawili ambao ni Mkenya Geoffrey Mutai na Muethiopia Aselefech Mergia. Mutai ni bingwa mara mbili wa New York marathon na mshindi wa mbio za marathon za Berlin mwaka wa 2012.

Orodha ya washiriki tayari ina jina la anayeshikilia rekodi ya marathon kwa sasa Mkenya Dennis Kimetto na aliyewahi kushikilia rekodi hiyo ambaye ni bingwa mtetezi wa London Marathon Mkenya Wilson Kipsang.

Na mmoja wa watakaoshiriki mbio hizo kwa upande wa wanawake ni Mkenya Mary Keitany ambaye alizishinda katika mwaka wa 2011 na 2012. Keitany kwa sasa anayanoa makali mjini Iten, eneo la bonde la Ufa nchini Kenya.

Mbio hizo za London zitakuwa zake za pili baada ya kurejea kutoka likizo ya kujifungua. Alishinda mbio za New York mwaka jana na analenga kuweka muda bora zaidi kwenye barabara za London.

Keitany atapambana katika mbio za London na wakenya wenzake wakiwemo bingwa wa sasa Edna Kiplagat, Florence Kiplagat, Priscah Jeptoo na Jemimas Sumgong.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman