1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

M-PESA: Simu ya mkononi inapokuwa benki

7 Septemba 2012

Mambo mengi yamebadilika nchini Kenya tangu pale kampuni ya simu za mkononi, Safaricom, kuanzisha huduma ya M-Pesa ambayo wateja huitumia kutuma fedha kupitia ujumbe mfupi wa maandishi kwa simu ya mkononi.

https://p.dw.com/p/164rY
Huduma ya M-Pesa nchini Kenya.
Huduma ya M-Pesa nchini Kenya.Picha: DW

Neno M-pesa linatumika katika mabadilishano ya pesa kupitia simu ya mkononi. Sammy Lewa ni mtumiaji wa huduma hii na anafurahishwa nayo.

"Tangu nimesajiliwa kuwa mtumiaji wa huduma ya M-Pesa, maisha yamekuwa rahisi kwangu .Naweza sasa kutuma pesa kwa wazazi wangu kwa kutumia huduma hii ya M-pesa.Nalipia huduma ya maji na umeme kutumia M-Pesa.Na pia nalipia karo ya shule ya mwanangu kupitia M-Pesa.Na pia hununua muda wa maongezi katika simu yangu kupitia M-Pesa na wakati mwingine huwatumia muda wa maongezi marafiki zangu kwa kutumia M-Pesa." Anasema Tony Lewa.

Kwa kutoa huduma hii Safaricom hupata fedha kidogo kutokana na fedha inayotozwa watumiaji. M-Pesa imekuwa ni sehemu ya chanzo cha ajira, ambapo zaidi ya watu 250,000 wanapata ajira kupitia M-Pesa nchini Kenya. uchumi wa Kenya umefaidika kwa jumla , na kwamba watu wengi zaidi wamefaidika pia kupitia huduma hii ya fedha kupitia simu za mkononi. Uchumi umekua . Na hii ni kutokana na huduma ya M-Pesa , anasema Dr. Joy Kiiru, mtaalamu wa uchumi kutoka mjini Nairobi.

"M-Pesa imeleta athari nzuri katika uchumi, imeleta uhai katika sekta ya fedha na kuiongeza. Mambo yote hayo yamesababisha hali nzuri. Pia M-Pesa imeimarisha sekta ya fedha nchini Kenya."

M-PESA yakinga wizi wa fedha

Kwa kutumia M-pesa inaondoka hatari ya kuibiwa fedha taslim. Watu wengi zaidi wanaiamini huduma hii, wanawekeza fedha kidogo na kuanzisha biashara. Leo hii asilimia 70 ya Wakenya wanatumia huduma hii ya M-Pesa. Huduma hii ya simu ya mkononi imekuwa na mafanikio makubwa katika muda wa miaka mitano iliyopita, katika nchi hii inayoendelea. Na pia M-pesa imebadilisha maisha ya kila siku ya Wakenya.

Vituo vya kutuma na kupokea fedha kupitia huduma ya M-Pesa nchini Kenya.
Vituo vya kutuma na kupokea fedha kupitia huduma ya M-Pesa nchini Kenya.Picha: DW

"Kwa mfano unatumiwa fedha kutoka mbali , na mtu huyo yuko mjini Nairobi inakuwa rahisi unazipata wakati huo huo." Anasema Joyce, mwanafunzi na mtumiaji wa huduma ya M-Pesa.

Haiwezekani kufananisha wakati huu na wakati ambapo mtu hulazimika kuweka fedha katika akaunti ya benki, anasema Joyce. Hata hivyo si kila kitu kimekwenda sawa katika historia ya huduma hii ya M-Pesa. Elizabeth Mafura kutoka Nairobi anakumbuka miezi ya mwanzo ya huduma hii ya M-pesa.

"Wakati huduma hii ya M-Pesa inaanzishwa kulikuwa na matatizo. Kwa mfano mtu ameweka namba ambayo si sahihi na kutuma fedha kwa mtu ambaye hakumkusudia . Ukipiga simu Safaricom , simu haipokelewi. Lakini hivi sasa kuna huduma ya wateja na kila kitu kinafanykazi vizuri."

Mafanikio ya kiuchumi ya M-PESA

Kwa kutumia huduma ya M-Pesa baadhi ya Wakenya wamefanikiwa kutimiza malengo yao ya binafsi. Bila ya kuwa na akaunti ya benki na kutumia fedha nyingi za malipo, kwa kutumia M-Pesa unaweza kuhamisha fedha na kuzipeleka utakako. Ni pale tu hata hivyo iwapo hutabadili kadi ya simu yako. kutokana na msingi wa mafanikio haya makubwa ya M-pesa makampuni mengine ya simu za mkononi yameamua kufuata mkondo huu wa M-Pesa.

Vituo vya kutuma na kupokea fedha kupitia huduma ya M-Pesa nchini Kenya.
Vituo vya kutuma na kupokea fedha kupitia huduma ya M-Pesa nchini Kenya.Picha: DW

Kampuni ya Zain nchini Kenya kwa mfano ina huduma inayojulikana kama Airtel money. Makampuni mengine yanayoshindana katika huduma hii ni pamoja na YuCash na Orange money. Na kile kinachowezekana nchini Kenya , kinaweza kuleta matumaini kwingineko.

Hususan kule ambako watu wengi hawana uwezo wa kuwa na akaunti ya benki. Sudan, Tanzania, Afghanistan na India ni baadhi ya nchi ambazo zinatumia huduma hii kwa sasa. Na hata katika bara la ulaya kuna huduma kama hii nchini Uingereza.

Mwandishi: Alfred Kiti/Sekione Kitojo
Mhariri: Iddí Ssessanga