1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Löw amtafuta msaidizi wake

18 Julai 2014

Joachim Löw ameyaangazia macho yake kwa changamoto ijayo – kuiga ushindi wa Uhispania kama Mabingwa wa Ulimwengu na Ulaya. Na sasa kocha huyo wa Ujerumani yuko mawindoni kumtafuta msaidizi wake mpya.

https://p.dw.com/p/1CfIl
Joachim Löw Hans-Dieter Flick WM 2014 Ankunft Weltmeister
Picha: Karina Hessland/Bongarts/Getty Images

Naibu kocha Hans-Dieter Flick, amekuwa msaidizi wa Löw tangu mwaka wa 2006, wakati Löw alipoichukua mikoba kutoka kwa Jürgen Klinsmann baada ya kukamilika Kombe la Dunia lililoandaliwa katika ardhi ya nyumbani. Kuanzia Septemba mosi, Flick atachukau jukumu la kuwa Mkurugenzi mkuu wa Shirikisho la Soka Ujerumani - DFB.

Mwezi wa Septemba utakuwa wenye shughuli nyingi kwa Die Mannschaft. Kando la uteuzi huu, pia kutakuweko na mechi za kirafiki dhidi ya Argentina walioshindwa katika fainali, na Scotland.

Mnamo Oktoba 2013, Löw aliurefusha mkataba wake na Shirikisho la DFB hadi mwishoni mwa mashindano ya UEFA Euro 2016. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 53 kisha atakuwa amekamilisha kipindi cha mwongo mmoja kama kocha wa Ujerumani.

Kocha wa zamani wa Mainz Thomas Tuchel anaripotiwa kuwa mmoja wa majina yanayotarajiwa kujaza pengo la naibu kocha wa taifa. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 39 alihama klabu ya Mainz kwa ghafla mwishoni mwa msimu uliopita wa Bundesliga licha ya kuisaidia klabu hiyo kufuzu katika dimba la Europa League kwa mara ya pili katika historia ya klabu hiyo.

Rais wa DFB Niersbach ameweka wazi kuwa Löw atafanya uamuzi kamili kuhusiana na nafasi hiyo, na hapatakuwa na hali yoyote ya kuingilia kati kwa maafisa wengine wa DFB pamoja na wadau wa soka Ujerumani.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA/AFP/reuters
Mhariri: Mohammed Khelef