1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongo yafutilia mbali sensa kabla uchaguzi

Josephat Nyiro Charo23 Januari 2015

Baraza la seneti la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo leo (23.01.2015) limefuta kipengee kinachotaka sensa ifanyike kabla uchaguzi wa rais mwaka ujao katika muswaada utakaomuwezesha rais Joseph Kabila kubakia madarakani.

https://p.dw.com/p/1EPU9
Unterzeichnung Friedensabkommen im Kongo
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Joseph KabilaPicha: Reuters

Baraza la seneti katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limefutulia mbali kipengee kinachotaka kufanyike zoezi la sensa kabla uchaguzi wa rais mwaka ujao na kuidhinisha ibara ya 8 ya muswaada huo uliofanyiwa marekebisho, likisema usajili wa wapigaji kura katika daftari la wapiga kura lazima ufanyike kwa mujibu wa muda uliowekwa katika katiba kwa uchaguzi wa rais na bunge.

Kipengee hicho, ambacho kiliidhinishwa mwishoni mwa wiki iliyopita na bunge, kimeibua maandamano ya upinzani ambapo watu wapatao 42 waliuwawa mjini Kinshasa kwa mujibu wa shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu, International Federation for Human Rights (FIDH).

Tume inayowajumuisha wajumbe kutoka pande zote sasa itakuwa na jukumu la kuzidurushu sehemu mbili za miswaada hiyo kabla kura ya mwisho, inayotarajiwa kufanyika kabla kikao cha bunge kumalizika Jumatatu wiki ijayo. Zoezi la kuupigia muswaada wa awali lilikuwa lifanyike jana lakini likaahirishwa hadi leo, ili kuipa nafasi tume ya baraza la seneti inayodurusu vipengee vya sheria hiyo ilikuwa bado haijakamilisha kuyachungza marekebisho yaliyopendekzewa.

"Kwa mustakabali wa nchi yetu hatuwezi kuuvuruga muswaada huu. Ndio maana tunahitaji kuipa tume muda wa kukamilisha kazi yake tupate sheria itakayomridhisha kila mtu," alisema rais wa baraza la seneti Leon Kengo Wa Dondo, wakati alipowahutubai wabunge jana.

Baada ya siku tatu za maandamano utulivu ulirejea katika mji mkuu wa Kongo, Kinshasa, hapo jana, lakini machafuko yakaripotiwa katika mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, Goma, mashariki mwa nchi hiyo. Kwa mujibu wa maafisa wa Kongo watu wanne waliuwawa katika machafuko ya Goma.

Kongo Unruhen in Kinshasa
Machafuko mjini KinshasaPicha: Reuters/N'Kengo

Huduma za mtandao wa mawasiliano wa intaneti ambazo zilisimamishwa wakati wa maandamano hayo zilirejeshwa kwa sehemu ndogo jana, ingawa huduma ya kutuma ujumbe mfupi bado imefungwa.

Umoja wa Mataifa waonya kuhusu machafuko

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ameelezea wasiwasi mkubwa kuhusu machafuko yanayoendelea nchini Kongo na amezitaka pande zote husika kujizuia kufanya vurugu. Ban aidha amesema mchakato wa uchaguzi huru na wa haki sharti ufanyike kwa mujibu wa katiba ya sasa bila kucheleweshwa.

Akizungumza jana kuhusu machafuko yanayoendelea Kongo kabla kufanyika kikao cha baraza la usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York, kuhusu juhudi za kupambana na kundi la waasi la FDLR, naibu katibu mkuu anayehusika na tume za kulinda amani za umoja huo Herve Ladsous alisema, "Taarifa ya katibu mkuu wa Umoja wa Matiafa inaelezea wasiwasi wake kuhusu jinsi maandamano haya yalivyoshughulikiwa na vyombo vya usalama."

Ban Ki Moon und Leon Kengo Wa Dondo Kinshasa 22.05.2013
Ban Ki Moon na rais wa baraza la seneti la Kongo, Leon Kengo Wa Dondo, Kinshasa (22.05.2013)Picha: Junior D. Kannah/AFP/Getty Images

Ladsous pia alisema katibu mkuu alikumbusha kwamba uhuru wa kujieleza na kutoa maoni kwa waandamanaji wanaoandamana kwa amani, kwa vyombo vya habari na kila kitu kinachohusiana na uhuru wa watu kuandamana lazima uheshimiwe.

Wajumbe wa kimataifa kutoka nchi za eneo la maziwa makuu pia wamesema wameingiwa na wasiwasi kutokana na machafuko ya Kongo na wamewatolewa mwito viongozi wa nchi hiyo wafanye kila wanaloweza kuepusha machafuko zaidi na waandae uchaguzi kama inavyotakiwa katika katiba ya nchi.

Kufikia sasa jumla ya watu wapatao 42 wanaripotiwa kuuwawa katika makabiliano na maafisa wa usalama, kwa mujibu wa kundi moja lililoandaa maandamano hayo. Lakini serikali, ambayo inakanusha inapania kuchelewesha uchaguzi nchini humo, kwa upande wake inasema watu 15 wamekufa, wengi wao wakiwa wevi na wahalifu.

Mwandishi: Josephat Charo/RTRE/APE

Mhariri: Saumu Yusuf