1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kizazi njia panda - awamu ya pili

4 Februari 2015

Mercy, Trudy, Dan na Niki ni wanafunzi kwenye Bongo Academy. Katika awamu ya pili ya mchezo huu wanakabiliana na athari za matendo yao, zinazowatia mashakani zaidi. Ipo haja ya kushirikiana katika majaribio!

https://p.dw.com/p/1CQPT
Wahusika wa awamu ya pili ya Kizazi njia panda
Picha: DW

Nchini Laboria anakotoka Dan, vita vya kikabila vimezuka na kuiathiri kwa kiasi kikubwa familia yake. Kwa sasa, Dan yuko salama shuleni Bongo Academy iliyoko nchi jirani, lakini hiyo haimaanishi ameepukana na matatizo. Mtazamo wake dhidi ya wanawake unamtia mashakani. Je yuko tayari kujitwika majukumu?

Mercy ana mengi yanayomsumbua akili. Wadogo zake mapacha Kadu na Banda hatimaye wamerejea nyumbani kuungana tena na familia yao - lakini ni yapi waliyopitia? Ni kwa nini wanaota ndoto mbaya kila siku na ni kwa nini Banda anakohowa kila wakati? Msoto, baba yake Mercy anaandamwa na polisi, huku mkewe pia akiamua kumgeuka. Hata hivyo, haya yote hayawezi kulinganishwa na masaibu yanayomuandama Mercy ambayo bado ni siri kubwa…

Urafiki wa Mercy na Trudy shuleni unapitia jaribio kubwa huku Niki akianguka kwenye masomo yake, kwani sio tena mwanafunzi bora darasani…

Vijana hawa kwenye mchezo wa "Kizazi njia panda" wanakabiliwa na masaibu mengi wakati wa muhula wa pili shuleni. Hata hivyo, baadaye wanafahamu kwamba ipo haja ya kushirikiana ili kukabiliana na changamoto hizi wakati mambo yanapokwenda mrama.

Waigizaji wanafanya nini katika mchezo huu?

Waigizaji wakuu kwenye mchezo huu wa Kizazi njia panda, na marafiki na familia zao wanawakilisha na kuelezea maisha ya jamii za matabaka mbalimbali. Vipindi vipya vya "Learning by ear - Noa bongo, jenga maisha yako" vinaangazia masuala mbalimbali yanayowakumba vijana na muingiliano wa rika mbalimbali miongoni mwa jamii.

Baadhi ya hoja na masuala yanayopewa kipaumbele katika mchezo huu ni kuhusu yale wanayopitia vijana maishani, kama vile urafiki, uaminifu, matarajio makubwa na jinsi ya kukabiliana na msukumo kutoka kwa wazazi wao. Kuna mabadiliko ya mara kwa mara wakati vijana hawa wanapotoka rika la ujana hadi uzee. Wanakabiliana na uhusiano wa kimapenzi, wivu, kushiriki ngono, uzazi wa mpango na mimba za mapema. Pia mchezo huu wa "Kizazi Njia Panda" unaweka wazi masuala nyeti mfano unyanyasaji wa kingono na kijamii. Pia unaangazia masuala ya afya na njia bora za kudumisha afya mfano tahadhari dhidi ya matumizi mabaya ya dawa na umuhimu wa kupata tiba bora.

Masuala ya kiuchumi yameelezewa pia katika mchezo huu. Siku zote pesa ni kigezo muhimu pale watu wa matabaka mbalimbali wanapotengamana. Vipindi hivi vinaelezea uhalisia wa ufisadi, biashara haramu na vinaonyesha umuhimu wa fedha na uhuru hasa miongoni mwa kina mama, changamoto na manufaa ya kujihusisha katika biashara na ujasiriamali. Biashara haramu ya watoto, ajira kwa watoto na maisha katika taifa linalokumbwa na vita pia ni miongoni mwa matatizo yanayotajwa kwenye mchezo huu.