1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kitisho cha IS chaongeza wakimbizi

22 Septemba 2014

Wanamgambo wa dola la Kiislamu wamesema wako tayari kuakabiliana na muungano wa kijeshi unoongozwa na Marekani huku wakitoa mwito kwa waislamu wote ulimwenguni kuwaua raia wa mataifa yaliyojiunga katika mapambano hayo.

https://p.dw.com/p/1DH4I
Mapambano Kati ya vikosi vya wanajeshi wa Iraq na IS eneo la Ramadi Iraq
Mapambano Kati ya vikosi vya wanajeshi wa Iraq na IS eneo la Ramadi IraqPicha: Reuters/Osama Al-dulaimi

Kauli ya kundi la IS inakuja katika wakati ambapo idadi ya wakimbizi wanaotoroka mapigano katika nchi hiyo ya Iraq na Syria ikizidi kuongezeka nchini Uturuki

Msemaji wa kundi la Dola la Kiislamu Abu Mohammed al-Adnani amesema Muungano wa kijeshi unaoongozwa na rais Barack Obama hauwezi kufanikiwa kuwashinda wapiganaji wa Jihad.Akizungumza katika ukanda wa sauti uliotolewa jana usiku Al Adnan ametoa mwito watu kuwakataza watoto wao kujiiunga na kile alichokiita waasi ambao Marekani inapanga kuwapa mafunzo kupambana na kundi hilo la dola la Kiislamu.

Akitoa kitisho msemaji huyo wa kundi la Dola la kiislamu amesema watakaojiunga na kikosi hicho cha muungano wa kijeshi wa nchi za Mgharibi watajichimbia makaburi yao wenyewe kwa mikono yao na kukatwa vichwa.Kitisho hicho kimetolewa katika wakati ambapo waziri mkuu wa Iraq Haidar al-Abadi ametoa tamko la kukataa kupelekwa wanajeshi wakigeni nchini Iraq kama sehemu ya juhudi za kupambana na wapiganaji hao wa Jihad

Mpaka wa Uturuki wa Suruc na Syria
Mpaka wa Uturuki wa Suruc na SyriaPicha: Bulent Kilic/AFP/Getty Images

Msimamo wa al-Abadi

Akizungumza na waziri wa ulinzi wa Australia David Johnston mjini Baghadad hii leo waziri mkuu al Hadi ametamka wazi msimamo wake na kusisitiza kwamba anapinga kwa kila hali kupelekwa kwa vikosi vya kigeni kuingilia kati mgogoro wa Iraq.Yote haya yanajitokeza wakati ambapo tayari Marekani na Ufaransa zimekuwa zikiwashambulia kutokea angani wanamgambo wa dola la Kiislamu nchini Iraq kampeini ambayo huenda ikapanuliwa hadi kufikia nchini.

Hata hivyo Marekani imeshasema si mara moja kwamba haitothubutu kutuma wanajeshi wa nchi kavu katika taifa hilo ambako wanajeshi wake walipambana katika vita vya umwagikaji damu mkubwa na vilivyoigharimu kiasi kikubwa cha fedha kabla ya kuondoka mwishoni mwa mwaka 2011.Hata hivyo kwa upande mwingine Marekani hiyo hiyo imeshapeleka mamia ya wanajeshi wake nchini Iraq tangu mwezi Juni kwa asjili ya kutekeleza jukumu maalum ambalo ni pamoja na kutoa ushauri kwa vikosi vya Iraq.

Juu ya Hilo wizara ya ulinzi ya Marekani imearifu kwamba itatuma ndege za kivita kutoka kambi yake iliyoko kwenye jimbo lenye utawala wake wa ndani la Kurdistan nchini Iraq kama sehemu ya mapambano makubwa zaidi dhidi ya wanamgambo hao wa dola la Kiislamu.

Iran yajitutumua

Katika muktadha mwingine rais wa Iran Hassan Rouhani ametoa kauli yake hii leo akisema nchi yake ndio msingi wa usalama katika Mashariki ya kati katika wakati ambapo eneo hilo linakabiliwa na magaidi.

Amesema watu wa kanda hiyo wanajitetea na wataendelea kujilinda dhidi ya magaidi na serikali pamoja na vikosi vya Jamhuri hiyo ya kiislamu vitawasaidia kila mahala.Msimamo huo wa Rouhani unajitokeza siku kadhaa baada ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry kusema Iran inajukumu la kubeba katika kuwashughulikia wanamgambo wa Dola la Kiislamu ambao wameyateka maeneo kadhaa ya Syria na Iraq.

Waziri mkuu wa Iraq Haider al-Abadi
Waziri mkuu wa Iraq Haider al-AbadiPicha: picture alliance / AP Photo

Wakati huohuo kutokana na wimbi la wakimbizi nchini Uturuki wanaotoroka vita Syria na Iraq,Ujerumani imejitwika jukumu la kuandaa mkutaano wa Kimataifa juu ya mgogoro huo wa wakimbizi.Wizara ya mambo ya nje imesema leo Ujerumani itaandaa mkutano huo Oktoba 28 ingawa haikutajwa wapi mkutano huo utafanyika.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Mohammed AbdulRahman.