1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kipsang, Kimetto kupambana katika London marathon

24 Aprili 2015

Ushindani mkali wa tangu jadi, ni mojawapo ya mambo yanayoweka mvuto katika mashindano makuu ya mbio za marathon. Waandalizi wa mbio za London Marathon wamezipa jina la "mapambano ya mabingwa"

https://p.dw.com/p/1FEZx
Lond Marathon 2013
Picha: picture alliance/empics

Bingwa mtetezi wa mbio za London marathon Mkenya Wilson Kipsang atapambana na mwanariadha anayeshikilia rekodi ya ulimwengu Mkenya mwenzake Dennis Kimetto, katika mbio za mwaka huu jijini London kesho Jumapili.

Waandalizi wa mbio hizo wamezipa jina la “mapambano ya mabingwa” ambapo Kimetto, aliyeweka muda bora ulimwenguni wa saa mbili, dakika mbili na sekunde saba mnamo mwezi Septemba katika mbio za Berlin marathon, atashiriki kwa mara ya kwanza jijini London wakati Mkenya Kipsang akitafuta taji lake la tatu baada ya kushinda mbio hizo mwaka wa 2012 na 2014.

41. Berlin Marathon 28. Sept. 2014 Kimetto Weltrekord
Bingwa anayeshikilia rekodi ya ulimwengu Dennis KimettoPicha: picture-alliance/dpa/Rainer Jensen

Orodha ya wanariadha nguli watakaoshiriki mbio za London marathon imejaa wakenya, akiwemo Emmanuel Mutai, mshindi wa London mwaka wa 2011, na ambaye alimaliza wa pili nyuma ya Kimetto mjini Berlin, na Stanely Biwott, aliyemaliza nyuma ya Kipsang mwaka jana mjini London.

Kipsang amesema mbio hizo zitakuwa za aina yake "Nadhani mara nyingine inavutia kuwa na watu kama hawa katika mchuano mmoja. Kwa sababu ninaposhiriki katika mchuano, ninashinda na kisha atakwenda katika mbio nyingine na ashinde. Hivyo wakati mwingine haivutii sana katika mchezo. Lakini wakati tunakuwa pamoja watu wanaweza kuona uwezo wa wanariadha, na hiyo ni rahisi kwa sababu unakuta kuwa mara nyingine, ukiwa na kundi kama hilo, kunakuwa na uwezekano mkubwa wa wanariadha wengi wanaokaribia katika nafasi za kwanza na nadhani hilo linavutia zaidi".

40. Berlin-Marathon Wilson Kipsang Kiprotich 29.09.2013
Bingwa mtetezi wa London Marathon Wilson KipsangPicha: picture-alliance/dpa

Kimetto ambaye alivunja rekodi ya ulimwengu iliyowekwa na Kipsang mnamo mwaka wa 2013 kwa sekunde 26, ndiye mwanariadha wa kwanza duniani kukimbia chini ya saa mbili na dakika tatu. Na Kipsang anatarajia ushindani mkali. "Nadhani natarajia ushindani mkali kwa sababu nilivunja rekodi, kisha Kimetto akaivunja mwaka jana, na ni mara ya kwanza ambapo tutakutana katika marathon lakini tumewahi kushindana katika mbio nyingine chache na nusu marathon. Hivyo nadhani alinishinda mara moja, nikampiku mara moja, hivyo nadhani ukiangalia tofauti pekee ni kuwa huenda nina uzoefu zaidi. Ameshiriki mbio chache za marathon lakini amefanya vyema sana. Katika mbio hizi kitu muhimu ni, vipi ulivyojiandaa kuzikabili mbio hizo kutoka mwanzo hadi mwisho".

Hata hivyo hakuna uwezekano wa kuwekwa rekodi nyingine ya ulimwengu hapo kesho, kwa sababu ya barabara zilizopinda za London zinafanya iwe vigumu kwa wanariadha ikilinganishwa na barabara zilizonyooka na pana jijini Berlin.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/AP/Reuters
Mhariri: Daniel Gakuba