1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa kijeshi achaguliwa Waziri mkuu wa Burkina Faso

Admin.WagnerD20 Novemba 2014

Rais wa mpito wa Burkina Faso Michel Kafando jana alimteua Luteni kanali Isaac Zida kuwa waziri mkuu licha ya jumuiya ya kimataifa kumtaka rais huyo kutowapa viongozi wa kijeshi nyadhifa kuu ili utawala wa kiraia urejee

https://p.dw.com/p/1DqEM
Picha: picture-alliance/dpa

Luteni Kanali Zida ambaye alijitangaza kiongozi wa Burkina Faso baada ya kung'atuka madrakani kwa Rais Blaise Compaore wiki tatu zilizopita, aliteuliwa hapo jana kuwa waziri mkuu wa Burkina Faso na kutwishwa jukumu la kuunda serikali mpya itakayokuwepo madarakani kwa kipindi cha mwaka mmoja kuelekea uchaguzi mkuu.

Licha ya kuwa Rais Kafando ambaye ni waziri wa zamani wa mambo ya nje kuwa kiongozi wa kiraia,uteuzi wa Zida unaonyesha kuwa jeshi la Burkina Faso halina mipango ya hivi karibuni kujiondoa katika uongozi wa kisiasa wa taifa hilo la magharibi mwa Afrika.

Zida aomba kuungwa mkono

Zida amewataka raia wa nchi yake na jumuiya ya kimataifa kuinga mkono serikali hiyo mpya katika azma yake ya kuhakikisha kuna kipindi cha mpito chenye amani na kusisitiza serikali haina nia ya kujali maslahi yake bali ya waburkina Faso.

Waziri mkuu mpya wa Burkina Faso Luteni Kanali Isaac Zida
Waziri mkuu mpya wa Burkina Faso Luteni Kanali Isaac ZidaPicha: STR/AFP/Getty Images

Kiongozi huyo wa kijeshi ameongeza kusema malengo ya serikali ni kuhakikisha kunafanyika uchaguzi mkuu huru na wa haki na kutekeleza mageuzi muhimu yatakayoisogesha mbele nchi hiyo.

Baadhi ya wawakilishi wa mashirika ya kijamii wamesema wanatiwa wasiwasi na uteuzi huo wa Zida mwenye umri wa miaka 49 lakini wako tayari kuwa na subira na kuchunguza utendaji wake.

Baadhi ya wakaazi wa mji mkuu wa Burkina Faso, Ougadogou hata hivyo wameshutumu uteuzi huo na kuutaja usaliti wa mapinduzi yao.

Rais Kafando aahidi taifa imara

ais Kafando mwenye umri wa miaka 72 aliapishwa rasmi Jumanne wiki hii kuwa rais wa serikali ya mpito na ameahidi atahakikisha taifa hilo lenye raia takriban milioni 17 haliwi taifa lisilo imara.

Rais wa serikali ya mpito wa Burkina Faso Michel Kafando
Rais wa serikali ya mpito wa Burkina Faso Michel KafandoPicha: picture-alliance/dpa

Kulingana na makubaliano ya mfumo wa serikali hiyo ya mpito,Kafando na Zida wote hawataruhusiwa kugombea katika uchaguzi mkuu unoatarajiwa mwezi Novemba mwaka ujao.Serikali hiyo ya mpito itakuwa na mawaziri 25 na kiongozi wa kiraia ndiye atakayeliongoza bunge litakalokuwa na wabunge tisini tu.

Umoja wa Afrika ulikuwa umeonya taifa hilo huenda likawekewa vikwazo iwapo halitamchagua kiongozi wa kiraia kuliongoza na kuteuliwa kwa Kafando kulipongezwa na umoja huo wa Afrika.

Hata hivyo kurejea madarakani kwa Zida kama waziri mkuu wa Burkina Faso kumezua mashaka katika jumuiya ya kimataifa kuhusu wajibu wa jeshi katika uongozi wa taifa hilo.

Ikizingatiwa Compaore aliingia madarakani akisisitiza hana kiu cha madaraka lakini alisalia uongozini miaka 27 baada ya mapinduzi ya kijeshi na alilazimika kunga'tuka madarakani na kukimbia nchi jirani ya Cote d´Ivoire kufuatia shinikizo kutoka kwa umma baada ya kujaribu kutaka kubadilisha katiba ili arefushe muda wa kuendelea kuwepo madarakani.

Mwandishi:Caro Robi/Afp/Ap

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman