1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kerry na Lavrov wakutana kwa mazungumzo

Mjahida2 Machi 2015

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry anakutana na mwenzake wa Urusi Sergey Lavrov kwa mazungumzo, wakati hali ikiwa bado ni ya wasiwasi nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/1Ejgt
Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov
Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Urusi Sergei LavrovPicha: picture-alliance/AP Photo

Hakuna hata mmoja kati ya mawaziri hao wawili Kerry na Lavrov aliyeonekana kuwa na tabasamu kwa mwezake walipokutana leo asubuhi katika hoteli moja mjini Geneva.

Kukutana kwa mawaziri hawa wa mambo ya nchi za nje wa Marekani na Urusi kunajiri wiki moja tu baada ya John Kerry kuliambia bunge la Marekani, kuwa maafisa wa Urusi walimdanganya juu ya wajibu wa nchi hiyo katika mgogoro wa Ukraine.

Tamko hilo lilikemewa vikali na wizara ya mambo ya kigeni ya Urusi. Hata hivyo maafisa wa Marekani kwa upande wao walisema Kerry hakumshutumu Lavrov moja kwa moja bali alikuwa anazungumzia taarifa za umma na ripoti zinazotoka katika vyombo vya habari kuhusu mgogoro wa Ukraine, japokuwa Lavrov ndio afisa pekee aliyekutana ana kwa ana na Kerry katika miezi ya hivi karibuni.

Ukraine pamoja na waasi wanaoiunga mkono Urusi wanaendelea kutupiana lawama juu ya ukiukwaji wa mkataba uliotiwa saini hivi karibuni wa kusitisha mapigano Mashariki mwa Ukraine.

Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry
Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Marekani John KerryPicha: Reuters

Aidha mkutano wa Kerry na Lavrov unafanyika wakati Marekani na washirika wake wa Magharibi wakifiria kuiadhibu Urusi kwa kuiwekea vikwazo zaidi kufuatia nchi hiyo kujihusisha na mgogoro wa Ukraine.

Wiki iliopita Kerry alisema vikwazo vipya tayari vimeshatayarishwa na kusema kwamba vinaweza kutekelezwa hivi karibuni.

Marekani yataka uchunguzi wa kina kufanywa juu ya mauaji ya Boris Nemstov

Mkutano wa leo pia unafuatia mauaji ya kiongozi mashuhuri wa upinzani nchini Urusi Boris Nemtsov ambapo Marekani na maafisa wa nchi nyengine za Magharibi wametaka uchunguzi huru na wa uhakika kufanywa ili kubaini kipi kilichosababisha kifo chake. Rais Vladimir Putin amesema atahakikisha uchunguzi huo unafanyika.

Kwa upande mwengine shirika la Umoja wa Mataifa la kutetea haki za binaadamu limesema zaidi ya watu 6,000wameuwawa tangu kuanza kwa ghasia nchini Ukraine mnamo mwezi Aprili mwaka uliopita. Kulingana na mkuu wa shirika hilo Zeid Ra'ad Al Hussein ghasia hizi zimesababisha wakaazi wengi kupoteza makaazi yao pamoja na miundo misingi kuharibiwa.

Kiongozi mashuhuri wa upinzani nchini Urusi Boris Namestov
Kiongozi mashuhuri wa upinzani nchini Urusi Boris NamestovPicha: Kirill Kudryavtsev/AFP/Getty Images

Ripoti hiyo ambayo ni ya tisa kutoka kwa shirika hilo la Umoja wa Mataifa imeonya kuzidi kupanuka kwa mzozo wa Ukraine kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari Zeid Ra'ad Al Hussein ametoa wito kwa pande zote mbili kuheshimu makubaliano ya amani yanayoyumba yaliotiwa saini mjini Minsk na kusimamisha mara moja mapigano ambayo yamesababisha hali ngumu kwa wakaazi wa Ukraine.

Mwandishi: Amina Abubakar/AP/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman