1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yataka kambi ya Daadab ifungwe

12 Aprili 2015

Kenya imeupa Umoja wa mataifa miezi mitatu kuiondoa kambi inayowahifadhi karibu wakimbizi nusu milioni kutoka Somalia, kama sehemu ya jibu kwa mauaji ya watu 148 yaliyofanywa na Wasomali wenye silaha nchini Kenya.

https://p.dw.com/p/1F6V2
Kenia Dadaab, Somalische Flüchtlinge
Wakimbizi katika kambi ya Daadab nchini KenyaPicha: Getty Images

Kenya hapo nyuma imekuwa ikiwashutumu wanamgambo wa Kiislamu kwa kujificha katika kambi hiyo ya Daadab ambayo inalitaka shirika la Umoja wa mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR kuwahamisha wakimbizi hao na kuwapeleka ndani ya Somalia.

"Tumewataka UNHCR kuwahamisha wakimbizi katika muda wa miezi mitatu, wakishindwa kufanya hivyo tutawahamisha wenyewe," makamu wa rais William Ruto amesema katika taarifa siku ya Jumamosi.

Kenia Impfung Dadaab Flüchtlingslager
Madaktari wakitoa chanjo kwa watoto katika kambi ya DaadabPicha: Getty Images

"Jinsi Marekani ilivyobadilika baada ya mashambulizi ya Septemba 11 ndivyo Kenya itakavyobadilika baada ya Garissa," amesema, akimaanisha chuo kikuu cha Garissa ambacho kilishambuliwa Aprili 2.

Emmanuel Nyabera, msemaji wa shirika la UNHCR nchini Kenya, amesema bado shirika hilo halijapokea mawasiliano ya awali kutoka serikali ya Kenya kuhusiana na kuhamishwa kwa kambi ya Daadab na hawezi kusema lolote kuhusu hilo.

Kambi kubwa kabisa duniani

Kambi hiyo inawahifadhi kiasi ya wakimbizi 600,000 kutoka Somalia, kwa mujibu wa Ruto , iko katika eneo kame kaskazini mashariki mwa Kenya, kiasi ya mwendo wa saa moja kwa gari kutoka mjini Garissa.

Flüchtlingslager Dadaab Kenia
Kambi ya Daadab nchini KenyaPicha: AP

Kambi hiyo ilitengenezwa kwanza mwaka 1991 wakati vita vya wenyewe kwa wenyewe vilipozuka katika nchi jirani ya Somalia, na katika miaka iliyofuatia imepokea wimbi la wakimbizi wengine wanaokimbia mzozo huo pamoja na ukame.

Umoja wa mataifa unasema idadi ya wakimbizi waliorodheshwa katika kambi hiyo ambayo ina wakaazi wengi zaidi na ambayo ina majengo ya kudumu, vyumba za udongo na mahema, kuwa ni wakimbizi 335,000. Kambi hiyo ina shule, huduma ya afya na vituo cha kijamii.

Kila nchi inawajibu wa kuwalinda binadamu

Macharia Munene, profesa katika masuala ya uhusiano wa kimataifa katika USIU- Afrika, amesema uwezo wa kuwahamisha mamia kwa maelfu ya wakimbizi ndani ya mipaka ya Somalia itakuwa jambo gumu sana.

Flüchtlingslager Dadaab Kenia
Nyumba katika kambi ya Daadab nchini KenyaPicha: AP

Lakini amesema hakuna maeneo salama ndani ya Somalia ambako wanamgambo wa Kiislamu wa al-Shabaab wamefurushwa na majeshi ya jeshi la Umoja wa Afrika katika miaka ya hivi karibuni.

"Kenya ni hali ya dharura ....Kila nchi inawajibu wa kuwahifadhi binadamu kwanza," ameliambia shirika la habari la Reuters.

Mazishi ya wanafunzi waliouwawa katika viunga vya chuo kikuu yalifanyika nchini humo. Picha za familia zenye majonzi zilionekana katika vyombo vya habari, zikiwakumbusha Wakenya kuhusu shambulio hilo.

Ruto amesema Kenya imeanza kujenga ukuta katika eneo la kilometa 700 katika mpaka wote na Somalia kuwazuwia wapiganaji wa al-Shabaab.

Kenia President Kenyatta Rede Terroranschläge 02.12.2014
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta(kushoto) na makamu wa rais William Ruto(kulia)Picha: AFP/Getty Images/S. Maina

"Tunapaswa kuilinda nchi hii kwa gharama yoyote, hata kama tutapoteza biashara na Somalia, potelea mbali," amesema.

Siku ya Jumanne , Kenya ilifunga makampuni 13 yanayosafirisha fedha, kuzuwia fedha zinazotuhumiwa kwenda kwa makundi yenye itikadi kali. Ruto amesema biashara yoyote ambayo inashirikiana na al-Shabaab itafungwa.

Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre

Mhariri: Iddi Ssessanga