1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kagame aapa kupambana na biashara ya binaadamu

20 Agosti 2014

Biashara haramu ya binaadamu inazidi kuongezeka Rwanda, huku Rais Paul Kagame wa nchi hiyo akikiri vijana, hasa wasichana, wamekuwa wakiuzwa kama bidhaa katika nchi jirani na hata mashariki ya mbali.

https://p.dw.com/p/1CxNQ
Rais Paul Kagame wa Rwanda.
Rais Paul Kagame wa Rwanda.Picha: picture-alliance/dpa

Biashara ya kuuza watu imekuwa ni kama haijulikani hapa Rwanda lakini tatizo hilo limeibuka kuwa tishio miaka ya hivi karibuni ijapokuwa chini kwa chini. Na sasa limechukua sura mpya baada ya Rais Kagame kulizungumzia, akisema kwamba kwa hatua lilikofikia haliwezi kuvumiliwa tena na hivyo ngazi za usalama hazina budi kuchukua hatua zaidi ya ilivyo sasa.

"Nimekuwa nikisoma ripoti na taarifa kuhusu watoto wetu hasa wale wa kike ambao wamebadilishwa kama bidhaa na kuuzwa,inakuwaje mambo haya yanafanyika! Yaani mtu anauzwa tu kama kitu cha kawaida tena sisi kama viongozi tukifahamu wazi kuwepokwa tatizo hilo. Hapa linapaswa kukoma." Alisema Rais Kagame katika hafla maalum ya kuwaapisha wajumbe wa baraza la mawaziri siku ya Jumatatu.

Akionekana mwenye kusikitishwa na visa hivyo, Rais Kagame alikwenda mbali na kuiomba jamii kwa ujumla kusimama kidete dhidhi ya tatizo hilo, kwani "ni suala ambalo hatuwezi kuliachia polisi peke yake ni lazima tusimame kidete na hatuwezi kuruhusu liendelee kuwepo ni jukumu la kila mmoja wetu kupambana na nalo."

Juhudi za vyombo vya usalama

Mkuu wa Idara ya Upelelezi, Tony Kuramba, ameithibitishia DW kuwa tatizo hilo lipo, na vyombo vya usalama vinakabiliana nalo ipasavyo.

Maadhimisho ya siku ya mauaji ya maangamizi mjini Kigali, tarehe 7 Aprili 2014.
Maadhimisho ya siku ya mauaji ya maangamizi mjini Kigali, tarehe 7 Aprili 2014.Picha: Getty Images

"Kwanza tunazidi kuihamasisha jamii, kuhakikisha kila mmoja anaelewa uzito wa biashara ya watu. Pili sisi kama polisi tunaendesha misako kwenye sehemu ambazo tunahisi vituo kunakofanyika vitendo hivyo, lakini kubwa tuna mikakati mingi zaidi ambayo si lazima kuitaja hapa kwenye vyombo vya habari. Kwa ujumla tuna njia nyingi za kulikabili tatizo hilo." Alisema Kuramba.

Lakini si kila mtu anaamini kuwa kweli vyombo vya usalama vinafanya ya kutosha kupambana na tatizo hili linalozidi kukuwa kwa sababu ya misingi yake kuwa ya kijamii zaidi kuliko kuwa ya kiusalama. Kanyehara John, mchambuzi wa masuala ya kijamii mjini Kigali, anasema kuwepo kwa visa hivi hasa siku za hivi karibuni ni ishara ya kumomonyoka kwa maadili ya jamii ya Rwanda.

"Ijapokuwa polisi haikuweza kutoa takwimu jumla za visa hivi lakini imefahamisha kwamba kadri siku zinavyosonga mbele ndipo tatizo hilo linavyozidisha kasi," alisema Kanyehara, akipigia mfano wa wasichana saba waliorudishwa kutoka Uganda mwaka jana baada ya kupelekwa huko kwa kudanganywa kwamba watapata kazi nzuri na kuishia kwenye vilabu vya pombe ambapo "wanatumikishwa kama watumwa wa ngono".

Mwandishi: Sylivanus Karemera/DW Kigali
Mhariri: Mohammed Khelef