1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za kufufua amani ya Mashariki ya Kati

16 Desemba 2014

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani J. Kerry anaendelea na juhudi zake za kuufufua utaratibu wa amani ya Mashariki ya kati.Baada ya kuonana na Netanyahu mjini Roma,amepangiwa kukutana na Saeb Erakat mjini London

https://p.dw.com/p/1E5TK
Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry (kushoto)akizungumza na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mjini RomePicha: Reuters/E. Vucci

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani aliyewasili London jana usiku ataonana pia na katibu mkuu wa jumuiya ya nchi za kiarabu Nabil El Arabi.

Waziri Kerry anaendeleza mazungumzo barani Ulaya kwa lengo la kujaribu kufufua utaratibu wa amani kati ya Israel na Palestina.Baada ya mazungumzo yake jumapili iliyopita pamoja na waziri mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov,alikutana na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwa muda wa masaa karibu matatu mjini Roma.

"Wanasiasa hao wawili walikuwa na mazungumzo ya muda mrefu na ya kina kuhusu usalama wa Israel na matukio katika Umoja wa mataifa"duru ya wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani imesema.

Baadae jana usiku waziri Kerry akakutana na mawaziri wenzake wa Ufaransa Laurent Fabius,wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier na wa Uengereza Philip Hammond katika uwanja wa ndege wa Orly mjini Paris.

"Tumesema wazi kabisa wakati wa mazungumzo pamoja na washirika wetu,kuna baadhi ya mambo hatuwezi kamwe kuyatetea" amesema afisa mmoja wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani mwishoni mwa mazungumzo hayo,akimaanisha Marekani haiko tayari kuridhia madai ya wapalastina.

Wapalastina wameelezea azma yao ya kuwasilisha hapo kesho kupitia mwakilishi wa Jordan,mswaada wa azimio mbele ya baraza la usalama la Umoja wa mataifa ili kudai Israel ikome kukalia ardhi zao mnamo muda wa miaka miwili inayokuja.

Ufaransa inasaka Azimio la Maridhiano

Ufaransa pia tangu wiki kadhaa sasa imeanzisha mashauriano pamoja na London na Berlin na baadae na Washington na Amman ili kuandaa hati ya maridhiano ambayo hailingani na ile ya wapalastina na ambayo ingeweza kuungwa mkono na wanachama wote 15 wa baraza la Usalama.

Frank-Walter Steinmeier mit Laurent Fabius 15.10.2014 Berlin
Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier (kulia) na waziri mwenzake wa Ufaransa Laurent FabiusPicha: picture-alliance/dpa/Bernd von Jutrczenka

"Paris inasaka ufumbuzi wa pamoja katika juhudi za kidiplomasia zlizoanzishwa na umoja wa Mataifa kuhusu mzozo kati ya Israel na Palestina" amesema waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Laurent Fabius,muda mfupi kabla ya kukutana na mawaziri wenzake.

"Ikiwa wapalastina watawasilisha mswaada wao wa azimio,wamarekani wameshasema watatumia kura yao ya turufu kuupinga.Kwa hivyo kwa upande mmoja mswaada huo wa azimio hautaweza kukubaliwa na kwa upande wa pili kuna jibu litakalofuatia kutoka upande wa wapalastina.Sisi tunachotaka,ni kufikia ufumbuzi wa pamoja."ameeleza waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa.

Pendekezo la Ufaransa linazungumzia juu ya kuanzishwa haraka mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestina kwa misingi muhimu kama vile kuishi pamoja kwa amani dola ya Israel na dola ya Palestina lakini bila ya kuwekwa muda kwa Israel kuyahama maeneo inayoyakalia ya wapalastina.

Wamarekani wanaliangalia kwa jicho la tahadhari pendekezo hilo la Ufaransa.

Netanyahu azikosoa nchi za Ulaya kuelemea upande wa wapalastina

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa amepangiwa pia kukutana mjini Paris na katibu mkuu wa jumuia ya nchi za kiarabu Nabil Al Arabi na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Palastina Riyad Al-Malki.

Netanjahu bei Beersheba 10.12.2014
Waziri mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Reuters/B. Ratner

Waziri mkuu wa Israel anaepinga hatua yoyote ya kupewa muda wa kuyahama maeneo ya wapalastina amezituhumu nchi za Ulaya kuwapendelea wapalastina."Ninavutiwa sana na juhudi za waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani za kuepusha hali isizidi kuwa mbaya" amesema.Na kuongeza tunanukuu:"juhudi za wapalestina na nchi kadhaa za Ulaya za kuilazimisha Israel na kuipa masharti zitapelekea hali kuzidi kuwa mbaya na kuitumbukiza Israel katika hali ya hatari."

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/AP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman