1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

John Kerry mbioni kujenga mfungamano dhidi ya Dola la Kiislamu

Abdu Said Mtullya11 Septemba 2014

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry ameanza mazungumzo nchini Saudi Arabia juu ya kuunda mfungamano wa kuiunga mkono Marekani katika harakati za kupambana na dola la Kiislamu .nchini Syria na Iraq.

https://p.dw.com/p/1DAeh
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John KerryPicha: Reuters

Waziri Kerry amesema wajumbe kwenye mazungumzo hayo wataijadili hatari ya ugaidi katika maeneo yao,na makundi ya itikadi kali yanayoongoza ugaidi huo. Shirika la habari la Saudi Arabia limeripoti kwamba wajumbe pia watazijadili njia za kuukabili ugaidi.

Waziri Kerry amekaririwa akisema kwamba mazungumzo ya mjini Jeddah ni muhimu sana. Mbali na wajumbe kutoka nchi za Ghuba, mazungumzo ya mjini Jeddah yanahudhuriwa pia na wajumbe kutoka Misri,Jordan ,Lebanon na Uturuki.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani anajaribu kuangalia jinsi nchi za Ghuba na nyingine jirani wa Iraq na Syria zitakavyokuwa tayari kuiunga mkono Marekani katika kupambana na wapiganaji wa dola la Kiislamu wanaozidhibiti sehemu za nchini Iraq na Syria. Nchi karibu 40 zimekubali kuchangia katika mfungamano wa kimataifa wenye lengo la kuwatokomeza magaidi wa dola la Kiislamu.

Mkakati wa Obama

Hapo jana Rais Barack Obama aliufafanua mkakati wa Marekani wa muda mrefu, juu ya kuwakabili magaidi wa dola la Kiislamu .Pamoja na hatua nyingine Marekani itayaimarisha mashambulio ya ndege dhidi ya wapiganaji wa dola la kiislamu nchini Iraq na Syria.

Waziri Kerry anajaribu kuujenga mfungamno wa kikanda ambapo nchi za kiarabu na Uturuki zitatoa mchango muhimu. Tayari Saudi Arabia imesema itazitoa kambi zake za kijeshi kwa ajili ya mafunzo ya waasi wa Syria wenye itikadi za wastani. Baadhi ya nchi za Ghuba zinaweza kutoa mchango kwa kufanya mashambulio ya ndege dhidi ya wapiganaji wa dola la Kiislamu ,wakati nchi nyingine zinaweza kusaidia kwa kutoa silaha,mafunzo na taarifa za upelelezi.

Uturuki haitapeleka askari wake

Hata hivyo Uturuki imesema haitaruhusu ardhi yake itumiwe kwa ajili ya kufanyia mashambulio dhidi ya dola la Kiislamu nchini Iraq na Syria. Afisa mmoja wa serikali ya Uturuki ameliambia shirika la habari la AFP, kuwa Uturuki haitakubali vituo vyake vya kijeshi vitumiwe na nchi za mfungamano unaoongozwa na Marekani ili kufanya mashambulio ya ndege dhidi ya wapiganaji wa dola la kiislamu.

Afisa huyo ambae hakutaka kutajwa jina pia ameliambia shirika la habari la AFP kuwa majeshi ya Uturuki hayatashriki katika harakati za kijeshi dhidi ya dola la Kiislamu.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry anafanya juhudi za kidiplomasia katika Mashariki ya Kati kabla ya mkutano utakaojadili njia za kuiimarisha Iraq utakaofanyika mjini Paris Jumatatu ijayo. Wajumbe kutoka nchi wanachama wa kudumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pia watahudhuria mkutano huo.

Mwandishi:Mtullya abdu/afp,rtre

Mhariri:Yusuf Saumu