1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ivory Coast ni mabingwa wa Kombe la Afrika

9 Februari 2015

Ivory Coast hatimae imejishindia Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kuukosa chupuchupu ubingwa wa michuano hiyo kwa takriban muongo mzima kwa kuifunga Ghana kwa mikwaju ya penelti 9-8 katika fainali.

https://p.dw.com/p/1EYE0
Wachezaji wa Ivory Coast wakifurahia ushindi wa Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Ghana mjini Bata, Guinea ya Ikweta. (08.02.2015)
Wachezaji wa Ivory Coast wakifurahia ushindi wa Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Ghana mjini Bata, Guinea ya Ikweta. (08.02.2015)Picha: Reuters

Mlinda mlango wa Ivory Coast Boubacar Barry mwenye umri wa miaka 35 ndie aliyeinusuru timu yake na kuifungia bao la ushindi katika fainali za michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kutoka sare ya bila kwa bila katika uwanja wa Estad de Bata hapo Jumapili(08.02.2015).

Golkipa huyo aliupanguwa mkwaju wa golkipa mwenzake wa Ghana Razak Braimah na baadae akaupachika wavuni mkwaju wake na kuipa timu yake ya Ivory Coast ushindi wa penelti 9-8 katika fainali hizo za jana za Kombe la Mataifa ya Afrika zilizofanyika huko Bata, Guinea ya Ikweta.

Mechi hiyo katika uwanja wa Bata ilikuwa imemalizika kwa sare ya bila kwa bila baada ya dakika 120.Ivory Coast ambayo ilikuwa imepoteza fainali mbili kwa mikwaju ya penelti muongo mmoja uliopita ilishindwa kufunga mikwaju yake miwili ya kwanza ya penelti lakini mfululizo wa mikwaju mengine ilitinga wavuni ikiwemo ile ya Yaya na Kole Tuore na Salomon Karou.

Huo ni ushindi wa pili wa Ivory Coast ambapo ushindi wake wa kwanza katika michuano hiyo ulipatikana pia kwa kuitowa Ghana kwa mikwaju ya penelti 11 kwa 10 mjini Dakar hapo mwaka 1992.

Maafa yatia kiwingu ushindi

Ushindi wao huo umekuja wakati wa usiku ambapo mashabiki 19 wa soka wamekufa baada ya vikosi vya usalama kuwazuwiya kuingia uwanjani wakati wa mechi ya soka mjini Cairo.

Vurugu za Cairo katí ya mashabiki wa Zamalek na vikosi vya usalama. (08.02.2015)
Vurugu za Cairo katí ya mashabiki wa Zamalek na vikosi vya usalama. (08.02.2015)Picha: STR/AFP/Getty Images

Madaktari na mashahidi wa tukio hilo wamesema watu hao wamekufa baada ya kukosa pumzi kutokana na mkanyagano uliosababishwa na hatua ya polisi kutumia gesi ya kutowa machozi kuwatawanya mashabiki wa soka waliokuwa wakijaribu kuingiwa uwanjani kwa nguvu wakati wa mechi ya ligi ya timu za Cairo, Zamalek na Ennpi.

Vurugu hizo zinaonyesha matatizo yanayolikabili kabumbu la Afrika na kutia kiwingu msisimko wa michuano ya fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika huko Guinea ya Ikweta nchi ambayo ilijitolea kuandaa michuano hiyo baada ya Morocco kugoma na kuvuliwa haki ya kuwa mwenyeji wa michuano hiyo.

Sifa ya aina yake

Ushindi wa Ivory Coast pia umempa kocha Mfaransa wa timu hiyo Herve Renard sifa ya aina yake ya kuwa kocha wa kwanza kunyakuwa ushindi wa Kombe la Mataifa ya Afrika na nchi tafauti baada ya kushinda akiwa na timu ya Zambia hapo mwaka 2012 wakati walipowashinda Ivory Coast kwa mikwaju ya penelti.

Herve Renard kocha wa timu ya taifa ya Ivory Coast.
Herve Renard kocha wa timu ya taifa ya Ivory Coast.Picha: picture-alliance/dpa

Renard amekaririwa akisema walikuwa na timu yenye mwamko sahihi wa kupambana na wameitumia vizuri zaidi bahati yao.

Matukio ya penelti za utata na ghasia za mashabiki wa soka katika michuano hii yanalaumiwa kwa kuharibu sifa ya kabumbu la Afrika ambapo Rais wa chama cha Soka Afrika CAF Issa Hayotou ameyaangalia kwa jicho tafauti.

Amesema matukio kama hayo yakitokea Ulaya wanasema kwamba ni makosa lakini yakitokea Afrika wanaanza kuzungumzia juu ya rushwa.

Kuendeleza ukoloni

Kwa mujibu wa Hayotu vyombo vya habari vya mataifa ya magharibi vilikuwepo hapo kuendeleza ukoloni tu na sio jengine.

Issa Hayatou Rais wa Chama cha Soka cha Afrika (CAF).
Issa Hayatou Rais wa Chama cha Soka cha Afrika (CAF).Picha: AFP/Getty Images/F. Senna

Tunisia iligoma kuomba radhi kwa CAF kwa vitendo vya wachezaji na maafisa wao kumfanyia fujo mwamuzi wa Mauritius Rajindraparsad Seechhurn aliyewapa penelti yenye utata katika dakika za majeruhi timu ya Equatorial Guinea wenyeji wa michuano hiyo ambapo timu hiyo ilisawazisha na baadae kuja kushinda kwa mabao 2-1 na kuingia nusu fainali.

Venginevyo Tunisia inaomba radhi kufikia mwishoni mwa mwezi wa Machi Tunisia itapigwa marufuku kushiriki michuano ya kuwania nafasi ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2017.

Utata katika michuano hii ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2015 ulianzia wakati nchi iliokuwa imepangiwa kuandaa michuano hii Morocco ilipovuliwa haki hiyo baada ya kugoma kuiandaa kutokana na wasi wasi wa kuenea kwa ugonjwa wa Ebola.Morocco imepigwa marufuku kushiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika ya mwaka 2017 na mwaka 2019.

Guinea ya Ikweta iliyojitolea kuwa mwenyeji wa michuano hiyo ilikuwa na miezi miwili tu ya kuandaa michuano hiyo iliyoshirikisha timu 16.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AFP

Mhariri : Yusuf Saumu