1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaua kwenye shule ya Umoja wa Mataifa Gaza

30 Julai 2014

Mashambulizi ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza yameingia wiki ya nne, huku takribani Wapalestina 40 wakiuawa na wengine zaidi ya 120 kujeruhiwa, wengi wao wakiwa wamejihifadhi kwenye shule ya Umoja wa Mataifa.

https://p.dw.com/p/1CmFI
Kijana wa Kipalestina akiangalia moto ukiwaka kwenye kinu cha mafuta kilichoshambuliwa tarehe 29 Julai 2014 Gaza.
Kijana wa Kipalestina akiangalia moto ukiwaka kwenye kinu cha mafuta kilichoshambuliwa tarehe 29 Julai 2014 Gaza.Picha: Getty Images

Ni siku nyengine ingawa si siku tafauti kwa Gaza ndani ya wiki hizi tatu. Hakuna mahala palipo salama kukimbilia. Hakuna asiyelengwa na makombora ya Israel.

Kufikia asubuhi ya leo, wizara ya afya ya Palestina imetangaza watu 43 kuwa wameuawa kwenye mashambulizi ya alfajiri kote Gaza, wakiwemo 16 waliouawa kwenye skuli ya Umoja wa Mataifa katika kambi ya wakimbizi ya Jabaliya, na saba wa familia moja katika kiunga cha Tuffah.

"Watu wameuawa mbele ya macho yetu. Viungo vyao tumeviona vikitenganishwa. Watu watano, akiwamo mwanamke mmoja, wameuliwa kwenye darasa hili. Tulikimbilia hapa kutoka maeneo yanayolengwa na majeshi ya Israel kwa kuwa kule hakukuwa salama. Hapa pia hatujaona usalama wowote. Hapana palipo salama ndani ya Gaza," amesema Abdel-Karim al-Masamha aliyeshuhudia mauaji ya leo kwenye skuli ya Umoja wa Mataifa.

Wanyama, misikiti yashambuliwa

Picha za vidio za shirika la habari la Reuters zinaonesha kuwa kwenye mashambulizi ya alfajiri ya leo katika kiunga cha Jabaliya, hata punda hawakunusurika. Punda kadhaa, wanyama ambao hutumika kama njia mbadala na ya kuaminika zaidi ya usafiri katika eneo hilo lisilo uhakika wa mafuta ya kuendeshea magari, wanaonekana wakielea kwenye damu, wengi wao wakiwa wameshauawa na wachache wakiwa wamejeruhiwa vibaya.

Msichana wa Kipalestina kwenye eneo ambalo kombora la Israel liliuawa watu wanane wa familia moja Gaza.
Msichana wa Kipalestina kwenye eneo ambalo kombora la Israel liliuawa watu wanane wa familia moja Gaza.Picha: Reuters

Msikiti uliomo kwenye kambi ya wakimbizi ya Shati pia uliharibiwa vibaya na mashambulizi ya usiku wa jana.

"Watu 138 huswali hapa mara tano kwa siku, sasa waende wapi? Hii ndiyo haki kwa Netanyahu? Sijui hasa ni kipi kinachotokezea. Nilikuwemo kwenye Vita vya Pili vya Dunia hadi mwaka 1949 na nilipigana kati ya Waingereza na Wajerumani, ila haikuwa kama vita hivi. Anachokifanya Netanyahu si vita," amesema Mohamed Sousi ambaye ndiye aliyeujenga msikiti huo.

Mashambulizi ya hivi sasa yalitanguliwa na yale ya jana ambapo Israel iliuwa Wapalestina 128 ikidai kuwa iliyalenga maeneo muhimu sana kwa kundi la Hamas.

Hospitali zinasema idadi kamili ya waliokufa na vifo vyao kuripotiwa kwenye taasisi rasmi ni Wapalestina 1,280, wengi wao wakiwa raia, na watoto wakiwa wahanga wakubwa wa mauaji haya.

Kwa upande wa Israel, jeshi la nchi hiyo limethibitisha kupoteza wanajeshi wake 53, huku raia watatu wakiuawa tangu mashambulizi yalipoanza hapo tarehe 8 mwezi huu.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef