1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

Taarifa ya Habari za Ulimwengu kutoka Idhaa ya Kiswahili ya DW

Habari | 22.08.2014 | 10:11

Pillay alikosoa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Mkuu wa Kamisheni ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa, Navi Pillay, amelikosoa vikali Baraza la Usalama la Umoja huo kwa kushindwa kwake kuutatua mzozo wa Syria na mizozo mingine hatari duniani. Akizungumza kwenye hotuba yake ya mwisho mbele ya baraza hilo hapo jana, Pillay alisema uharaka mkubwa zaidi wa Baraza la Usalama kushughulikia mizozo, ungeliweza kunusuru maisha ya maelfu ya watu. Pillay ameliambia Baraza hilo kuwa mgogoro wa Syria ni kielelezo cha kushindwa jamii ya kitaifa kuzuia maafa. Kiongozi huyo anayemaliza muda wake mwishoni mwa mwezi huu, alikuwa akizungumza kwenye kikao ambacho kilipitisha azimio linaloahidi kuchukuwa hatua madhubuti zaidi kuzuia migogoro. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, alisema umefika wakati wa Baraza la Usalama kuwa na ushirikiano na vitendo. Umoja wa Mataifa unasema kufikia mwezi Aprili mwaka huu, zaidi ya Wasyria 190,000 walishapoteza maisha kwenye mzozo huo ulioanzia Machi mwaka 2011.

Vikosi vya Peshmerga vyasonga mbele

Vikosi vya Peshmerga vya jimbo lenye utawala wa ndani la Kurdistan nchini Iraq vimesonga mbele kuelekea mji wa Jalawla, uliotwaliwa na wapiganaji wa kundi linalojiita Dola ya Kiislamu. Kwa mujibu wa afisa mmoja wa chama cha PUK cha Kurdistan, Shirko Mirwais, mapigano ya kuuchukuwa mji huo ambao uliangukia mikononi mwa waasi tarehe 11 mwezi huu, yameshasababisha vifo vya wapiganaji kadhaa kwa pande zote mbili. Mji huo ulio umbali wa kilomita 130 kaskazini mashariki mwa mji mkuu wa Iraq, Baghdad, ni muhimu sana kwa kuwa kwake karibu na mpaka wa Iran. Katika hatua nyengine, serikali ya Iraq imeahidi kumuachia huru waziri wa mwisho wa ulinzi katika serikali ya Saddam Hussein, Sultan Hashem, aliyekuwa amehukumiwa kifo. Hatua hii iliyotangazwa na naibu waziri mkuu anayemaliza muda wake, Saleh Mutlaq, inaweza kuhusishwa na jitihada za kuwaridhisha raia wa Kisunni, ambao hisia zao za kutengwa na serikali ya Nouri al-Maliki zinadhaniwa kuwafanya wawaunge mkono waasi wa Dola ya Kiislamu.

Israel yaendelea kuishambulia Gaza

Mashambulizi ya anga ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza yameuwa watu wawili asubuhi ya leo, siku ya tatu baada ya kuvunjika kwa mazungumzo ya amani mjini Cairo. Kwa mujibu wa jeshi la Israel, kufikia majira ya saa nne leo, tayari walishashambulia mara 20 huku Hamas wakirusha makombora mawili kuelekea Israel. Makombora ya Israel yaliangukia kwenye zizi la mifugo, ambako wafanyakazi wawili waliuawa na watano kujeruhiwa huko al-Khidra. Jana, Israel iliwauwa makamanda watatu wa ngazi za juu wa Hamas inaosema walihusika na hujuma kadhaa dhidi ya taifa hilo la Kiyahudi. Hadi sasa, zaidi ya Wapalestina 2,000 wameshauawa, robo yao wakiwa watoto, huku Israel ikipoteza wanajeshi 64 na raia watatu.

Hamas yawauwa majasusi 11 wa Israel

Afisa mmoja wa usalama mjini Gaza amesema  kwamba Hamas imewauwa watu 11 wanaoshukiwa kuwa majasusi wanaoifanyia kazi Israel. Washukiwa hao 11 waliuawa mapema leo kwenye makao makuu ya polisi, baada ya kuhukumiwa na mahakama za huko. Habari hizo zimechapishwa pia kwenye mitandao ya Al Rai na Al Majid yenye mafungamano na Hamas. Mauaji hayo ya leo yametokea siku moja baada ya Israel kuwauwa makamanda watatu wa ngazi za juu wa Hamas katika nyumba moja kusini mwa Ukanda wa Gaza. Hamas imeapa kulipiza kisasi mashambulizi yoyote dhidi ya viongozi wake. Idara ya ujasusi ya Israel hutegemea majasusi wake ndani ya Gaza kuwaonesha walipo viongozi wa Hamas.

Syria yatuma wanajeshi zaidi Tabqa

Siku moja baada ya kuwauwa kiasi cha wanamgambo kundi linalojiita Dola ya Kiislamu, serikali ya Syria imetuma wanajeshi zaidi kwenye kituo chake cha kijeshi kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Kituo hicho cha Tabqa, kilicho umbali wa kilomita 40 mashariki mwa mji wa Raqqa, kilikuwa ngome kuu ya serikali kwenye eneo ambalo limekuwa likidhibitiwa na waasi hao. Kwa mujibu wa Shirika la Haki za Binaadamu la Syria, jana wanamgambo hao walikivamia kituo hicho kujaribu kukichukua, lakini wengi wakauawa kutokana na mashambulizi makali ya mabomu ya kurushwa kwa mkono na ya kutegwa ardhini. Shirika la habari la Syria, SANA, limekanusha ripoti kwamba wanamgambo wa Dola ya Kiislamu wameingia kwenye kituo hicho.

Jeshi la Ukraine ladai mafanikio makubwa

Jeshi la Ukraine linasema limesababisha hasara kubwa kwa wapiganaji wanaoiunga mkono Urusi mashariki mwa nchi hiyo. Maafisa wa wizara ya ulinzi wamesema hivi leo kwamba jeshi limeharibu mitambo 11 ya kutungulia ndege, vifaru vitatu na magari matano ya kubebea silaha katika mapigano kwenye mji wa Snizhne. Jeshi pia linadai kuwauwa waasi 100, ingawa madai hayo bado hayajathibitishwa na vyanzo huru. Wakati huo huo, waasi wamesema kwamba wamekamata majengo mawili magharibi mwa mji huo na kuwateka wanajeshi 13 wa Ukraine, wakiwemo maafisa watatu wa ngazi za juu. Waasi hapo pia wamelilaumu jeshi kwa kulenga maeneo ya raia. Katika hatua nyengine, msafara wa magari 70 yaliyobeba msaada wa Urusi yamevuuka mpaka na kuingia Ukraine mapema leo.

Malaysia yaomboleza raia waliokufa kwenye MH17

Malaysia imetangaza siku moja ya maombolezo hivi leo wakati  miili ya abiria 20 wa ndege yake ya MH17 ikirejereshwa nyumbani kwa mazishi, zaidi ya mwezi mmoja baada ya kuangushwa mashariki mwa Ukraine. Waziri Mkuu Najib Razak amewaongoza maafisa wa ngazi za juu wa serikali kuipokea miili na majivu ya abiria 20 kati ya 43 wa Malaysia waliokuwemo kwenye ndege hiyo. Bendera nchini kote zinapepea nusu mlingoti, huku Razak akiita siku ya leo kuwa mwanzo wa kuwarejesha raia hao nyumbani. Ndege hiyo ya shirika la ndege la Malaysia iliangushwa tarehe 17 Julai na kuuwa watu wote 298 waliokuwamo. Hadi sasa miili ya raia 30 imeshatambuliwa na timu maalum ya wataalamu wa uchunguzi katika mji mkuu wa Uholanzi, Amsterdam, ambako miili yote inayopatikana huhifadhiwa.