1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Taarifa ya Habari za Ulimwengu kutoka Idhaa ya Kiswahili ya DW

Habari | 26.04.2015 | 03:30

1800 wafa kutokana na tetemeko la ardhi nchini Nepal

Viongozi wa dunia wametoa salamu za rambirambi kwa ajili  ya watu waliokufa kutokana na tetemeko kubwa  la ardhi lililoikumba Nepal.

Wizara ya mambo ya ndani ya  nchi hiyo imesema watu zaidi  ya 1800 wamekufa kutokana na tetemeko hilo lililofikia  kipimo cha 7.8.

Wengine zaidi ya 4700 wamejeruhiwa.

Kwa mujibu wa taarifa watu wengine kadhaa wamekufa  katika nchi jirani za India , China na  Bangladesh.

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Papa Francis amesema ameingiwa na huzuni kubwa na amesema yupo pamoja na  watu walioathirika na maafa hayo.

Serikali ya Nepal imetangaza hali ya hatari katika sehemu  zilizokumbwa na madhara ya tetemeko na imeiomba jumuiya ya kimataifa iisaidie nchi hiyo.   

  

Wapalestina wawili wapigwa risasi na polisi wa Israel

Polisi wa Israel wamewapiga risasi na kuwaua Wapalestina wawili waliowashambulia maafisa wa usalama kwa visu.

Kijana wa Kipalestina aliekuwa na umri wa miaka 20, aliepigwa risasi alimpiga kisu polisi mmoja kwenye sehemu ya kuvukia mpaka kwenye Ukingo wa Magharibi.

Hapo awali kijana mwengine wa Kipalestina, aliekuwa na umri wa miaka 17 pia alipigwa risasi na polisi wa Israel baada ya kujaribu kumshambulia polisi kwa kisu.

Juu ya kadhia hizo,Mamlaka ya Wapalestina imesema  Israel inasababisha mzunguko wa umwagikaji damu katika Mashariki ya Kati.

 

    

Adhabu ya kifo kutekelezwa Indonesia

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  Ban Ki-moon ameiomba Indonesia isiwanyonge watu 10 waliopatikana na hatia ya kuhusika na uhalifu wa madawa ya kulevya.

Indonesia imewaambia wafungwa  saba kati ya hao kumi kwamba adhabu ya kifo inayowakabili itatekelezwa karibuni  tu, na labda Jumanne ijayo.

Lakini utekelezaji wa adhabu hiyo kwa mfungwa wa Kifaransa umeahirishwa kwa muda ,baada ya serikali yake  kuishinikiza serikali ya Indonesia.

Watu hao waliohukumiwa adhabu ya kifo ,waliomba wasamehewe lakini maombi yao yamekataliwa.

Indonesia imesema inahitaji kuchukua hatua kali katika  kupambana na inachokiita hatari ya mihadarati. 

Watu wapiga kura kumchagua Rais nchini Togo

Idadi ya watu ilikuwa ndogo wakati wa kupiga kura ya kumchagua Rais nchini Togo .

Rais aliyemo madarakani Faure Gnasssingbe anaewania muhula wa tatu amepambana na wapinzani wanne katika kinyang'anyiro cha uchaguzi huo.

Mpinzani mkuu wa Rais ni Jean Pierre Fabre alieshika nafasi ya pili katika uchaguzi uliofanyika miaka mitano iliyopita nchini Togo.

Rais wa sasa Gnassingbe amekuwamo madarakani tangu mwaka wa 2005, baada ya baba yake kufariki, alietawala kwa muda wa miaka 38.

Uchaguzi huo uliofanyika jana ulicheleweshwa kwa muda  wa siku 10 kutokana na hitilafu zilizokuwamo katika orodha  za wapiga kura.

Uturuki yapinga vikali kuyaita mauaji ya Waarmenia kuwa ya kimbari

Rais  wa Uturuki ameulaumu vikali Umoja wa Ulaya pamoja na Marekani kwa kuyaita mauaji ya Waarmenia kuwa ni ya kimbari.

Mauaji hayo yalifanywa na majeshi ya himaya ya Osman miaka 100 iliyopita.

Rais huyo RecepTayyip Erdogan amezilaumu Ujerumani,Ufaransa na Urusi kwa kuyaunga mkono madai yanayotokana na uwongo wa Armenia.

Mabunge ya nchi zaidi ya 20 yanayatambua maangamizi  hayo kuwa ya kimbari. Bunge la Ujerumani pia limeyaita  mauaji hayo kuwa ya halaiki.

Mihadhara mbalimbali imefanyika duniani kote  kuyakumbuka mauaji hayo.

Taasisi za Ugiriki zalazimishwa kupeleka fedha Benki Kuu

Waziri wa mambo ya ndani wa Ugiriki amezungumzia   uwezekano wa kufanyika uchaguzi mwingine ili kuwapa watu  wa nchi hiyo fursa ya kutoa kauli ya mwisho juu ya sera ya uchumi ya serikali yao.

Waziri huyo Nikos Voutsis amesema, wale wanaofikiria kwamba serikali ya sasa nchini Ugiriki ni ya mpito, wanakosea.

Ameeleza kwamba wananchi wa Ugiriki wameshautoa uamuzi wao, lakini ikiwa itabidi,watapiga kura tena.

Waziri Voutsis aliyasema hayo wakati wa mjadala mkali  bungeni juu ya sheria ya kuzilazimisha taasisi za umma kuzipeleka akiba  zao za fedha kwenye Benki Kuu.

Lengo la hatua hiyo iliyojadiliwa bungeni ni kuiwezesha serikali kulipa mishahara ya watumishi wa umma  na kulipia riba za deni la serikali.          

Merkel: Tunatoa heshima zetu kwa Bartoszewski

Viongozi wa Ujerumani wamehuzunishwa na habari juu ya  kifo cha aliekuwa Waziri wa mambo ya nje wa Poland Wladyslaw Bartoszewski .

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amemsifu Bartoszewski kuwa mtu aliekuwa madhubuti katika kupigania  uhuru na maridhiano. Bibi Merkel amesema mwanasiasa huyo alikuwa mtu wa vitendo.

Naye Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank - Walter  Steinmeier amesema , mchango alioutoa mwanasiasa huyo wa Poland katika kuleta maridhiano baina ya nchi yake na Ujerumani, hautasahaulika.

Hayati Bartoszewski aliefariki akiwa na umri wa miaka 93  aliwahi kufungwa katika kambi ya mafashisti ya Auschwitz wakati wa vita vikuu vya pili na baadae alikuwa waziri wa mambo ya nje wa Poland.

   

.