1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya vifo vya ebola yaongezeka

27 Novemba 2014

Shirika la Afya Duniani-WHO, limetangaza kuwa idadi ya watu waliokufa kutokana na ugonjwa wa Ebola imeongezeka na kufikia 5,689. WHO ime jumla ya watu 15,935 wameambukizwa ugonjwa huo katika eneo la Afrika Magharibi.

https://p.dw.com/p/1DuiR
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Margaret Chan
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Margaret ChanPicha: Reuters

Idadi ya mwisho iliyotolewa na WHO Ijumaa iliyopita, ilikuwa inaonyesha vifo 5,459 na watu 15,351 walikuwa wameathirika na Ebola. Hata hivyo, shirika la afya ulimwenguni linaamini kuwa idadi hiyo inaweza ikawa ya juu zaidi kutokana na ugumu wa kukusanya idadi sahihi ya ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa shirika hilo ugonjwa hatari wa Ebola umeendelea kuziathiri nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone.

Wagonjwa wapya 600 waliripotiwa wiki zilizopita katika nchi hizo tatu na kwamba nchi ya Mali ambayo imeathirika na Ebola hivi karibuni, tayari imeripoti vifo vya wagonjwa sita kati ya wagonjwa wanane walioambukizwa.

Madaktari wakiwa mjini Conakry, Guinea
Madaktari wakiwa mjini Conakry, GuineaPicha: picture-alliance/dpa/Kristin Palitza

Imeelezwa kuwa wahudumu wa afya ndiyo wameathirika vibaya na Ebola, ambapo 340 wamekufa kati ya wagonjwa 592 walioripotiwa.

Nje ya Afrika, wagonjwa wanne wa Ebola waliripotiwa nchini Marekani, ambapo mmoja alifariki. Pia kulikuwa na mgonjwa mmoja nchini Ushipania, ambaye amepona.

Chanjo mpya ya Ebola yaonyesha matokeo mazuri

Wakati huo huo, chanjo mpya dhidi ya virusi vya Ebola inayofanyiwa majaribio nchini Marekani, imeonyesha matokeo mazuri. Wanasayansi kutoka taasisi ya mzio na magonjwa ya kuambukiza-NIAID, wamesema chanjo hiyo mpya imeonyesha dalili nzuri na salama baada ya kufanyiwa majaribio kwa wagonjwa 20 ambao ni watu wazima.

Ama kwa upande mwingine serikali ya Ujerumani imezindua kile ilichokiita ndege ya kwanza duniani kwa ajili ya wagonjwa wa Ebola. Ndege hiyo aina ya Airbus chapa A340-300 ina eneo maalum lililotengwa, mfumo wa kupitisha hewa tofauti na eneo maalum ambako madaktari wanaweza kuzuia maambukizi pamoja na kuondoa uchafu katika suti maalum za kujikinga na Ebola.

Waziri wa Afya wa Ujerumani, Hermann Groehe, amesema leo kuwa ndege hiyo inawahakikishia Wajerumani wanaojitolea kupambana na Ebola Afrika Magharibi kwamba iwapo wataambukizwa ugonjwa huo, Ujerumani itafanya kila liwezekanalo kuwarudisha haraka kwa ajili ya kupatiwa matibabu bora. Ndege hiyo ina uwezo wa kusafirisha mgonjwa mmoja tu kwa wakati mmoja. Ujerumani imesema nchi nyingine zitaruhusiwa kuitumia ndege hiyo pia.

Ndege ya Ujerumani maalum kwa wagonjwa wa Ebola, Airbus A340-300
Ndege ya Ujerumani maalum kwa wagonjwa wa Ebola, Airbus A340-300Picha: AFP/Getty Images/T. Schwarz

Wakati hayo yakijiri, Rais Francois Hollande wa Ufaransa, kesho anaanza ziara yake nchini Guinea, akiwa ni kiongozi wa kwanza wa mataifa ya Magharibi kuzuru kwenye nchi iliyoathiriwa vibaya na Ebola.

Hiyo ni ziara ya kwanza kufanywa na Rais wa Ufaransa nchini Guinea tangu mwaka 1999, na ina lenga kufikisha ujumbe wa mshikamano na Guinea, wakati nchi hiyo ikipambana na Ebola. Ufaransa imeahidi kutoa Euro milioni 100 kama mchango wake katika mapambano dhidi ya Ebola, huku ikielekeza zaidi juhudi zake nchini Guinea.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,DPAE,APE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman