1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICC yaliandama bara la Afrika

Admin.WagnerD9 Desemba 2014

Mahakama ya uhalifu ya kimataifa (ICC) yenye wanachama 122 imeanza mkutano wake huku zingatio likiwa ni bara la Afrika, na huku ikiandamwa na kivuli cha kufutwa kwa kesi dhidi ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta.

https://p.dw.com/p/1E1JU
Bosco Ntaganda Prozess ICC Den Haag 10.01.2014 Bensouda
Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC, Fatou BensoudaPicha: Reuters

Mkutano huo ulioanza jana unafanyika siku tatu tu baada ya mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama hiyo yenye makao yake makuu mjini The Hague Fatou Bensouda, kufuta mashtaka dhidi ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta. Bensouda aliishutumu Kenya kwa kile alichosema ni kuzuwia uchunguzi wake, huku akikosolewa vikali na baadhi ya waafrika ambao wanasema ICC inaliandama bara hilo pekee, tangu ilipoundwa mwaka 2002.

Sura mbaya ya Afrika kuhusu mahakama ya ICC

Rais mpya wa Baraza la mataifa wanachama wa mahakama hiyo Sidiki Kaba alitowa wito wa maridhiano ya kanda zote na hasa bara la Afrika. Katika hotuba yake ya ufunguzi alisema wanachama wa ICC wanapaswa kubadili sura mbaya ya Afrika kuhusu mahakama hiyo. Akasisitiza kwamba malalamiko yanapaswa kusikilizwa, ingawa kuna yasio halali wala msingi madhubuti. Kaba ambaye ni Waziri wa sheria wa Senegal, alisema Afrika haiwezi kubakia zingatio pekee la mahakama hiyo.

Akakumbusha kwamba mwendesha mashtaka mkuu na mahakimu wanne ni kutoka bara la Afrika, na kuwa Congo, Uganda,Jamhuri ya Afrika kati, Cote dÍvoire na Mali zote ziliiomba mahakama ichunguze maovu yaliotendeka katika nchi hizo.

Kenia Uhuru Kenyatta
Rais wa Kenya Uhuru KenyattaPicha: picture-alliance/dpa

Balozi wa Kenya Macharia Kamau alilitaka baraza hilo kuyashughulikia malalamiko ya nchi yake na Umoja wa Afrika. Kenya imeataka kuwepo na mashauriano kuhusu mwenendo wa mahakama na Bibi Bensouda katika kesi dhidi ya Rais Kenyatta na Makamu wake Wiliiam Ruto juu ya madai ya kuhusika katika machafuko ya baada ya uchaguzi wa Disemba mwaka 2007.

Katika kipindi cha miaka 12 kumefanyika uchunguzi wa visa 9 vyote vinavyodaiwa barani Afrika, na hadi sasa ina watuhumiwa 7 walio kizuizini. 13 wangali wakisakwa licha ya waranti uliotolewa. Miongoni mwao ni Rais wa Sudan Omar Hassan al-Bashir na Kiongozi wa waasi wa kundi la Lord's Resistance Army (LRA) nchini Uganda, Joseph Kony.

Wapalestina kukubaliwa rasmi uwanachama wa ICC

Wakati huo huo, Wapalestina wamekubaliwa rasmi kuwa waangalizi katika mkutano wa kilele wa nchi 122 za ICC. Mahakama hiyo inasema uamuzi huo ni hatua moja mbele ya kujiunga kama mwanachama kamili wa mahaka hiyo ya uhalifu ya kimataifa. Rais wa Palestina Mahmoud Abbas ametishia kuomba uwanachama kamili ili kushinikiza mashtaka ya uhalifu wa kivita dhidi ya Israel.

Mkutano huo wa nchi wanachama 122 wa mahakama ya uhalifu ya kimataifa mjini New York, utadumu kwa muda wa wiki mbili.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, AP

Mhariri: Saumu Yusuf