1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gerrard kuihama Liverpool

2 Januari 2015

Nahodha wa Liverpool Steven Gerrard ametangaza kuwa ataihama klabu hiyo mwishoni mwa msimu. Atahamia ng'ambo katika kile amesema kuwa ni “uamuzi mgumu kabisa kuwahi kuufanya maishani mwake“.

https://p.dw.com/p/1EEK9
Steven Gerrard
Picha: picture-alliance/dpa/Georgi Licovski

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 34 aliyejiunga na Liverpool akiwa na umri wa miaka 8, amekuwa nahodha kwa miaka 12 na hajawahi kuichezea klabu nyingine. Ameshinda Kombe la Ulaya, Vikombe viwili vya FA, Mataji matatu ya League Cup na Taji la UEFA Cup miongoni mwa mafanikio mengine.

Gerrard amesema ataendelea kucheza kandanda japokuwa hatofichua kwa sasa ni wapi atacheza, lakini anachofahamu kwa hakika ni kuwa klabu atakayojiunga nayo haitakuwa mpinzani wa moja kwa moja wa Liverpool, maana hawezi maishani mwake kucheza dhidi ya Liverpool.

Huku kukiwa na uvumi kuwa huenda akachukua jukumu la ukufnzi uwanjani Anfield katika siku za usoni, nahodha huyo wa zamani wa England amesema anatumai na kuomba kuwa siku moja ataweza kurejea kuihudumia Liverpool tena, katika wadhifa wowote ule.

Kocha Brendan Rodgers, na wachezaji wenzake wamemiminia sifa nguli huyo wakimtakia kila la kheri katika kazi yake ya usoni. Rodgers amesema, kama kiongozi na kama mtu, hawezi kufananishwa na yeyote ambaye amewahi kufanya kazi naye. Na kiwango cha kazi yake kinapaswa kuwa mfano kwa mwanasoka yeyote.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri:Gakuba Daniel