1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Freiburg, Stuttgart zilitumia dawa za kuongeza nguvu

6 Machi 2015

Mtaalamu mmoja wa madawa amelitaka Shirikisho la kandanda la Ujerumani DFB, lichunguze madai kwamba vilabu viwili vya Bundesliga vilihusika katika kashfa ya utumiaji madawa ya kuimarisha nguvu yaliopigwa marufuku

https://p.dw.com/p/1EmYU
Bayer Ürdingen vs. SC Freiburg 1982
Picha: picture-alliance/dpa

Freiburg na Stuttgart zinadaiwa kuhusika katika kashfa ya utumiaji madawa ya kuimarisha nguvu yaliopigwa marufuku, mwishoni mwa miaka ya 1970 na mwanzoni mwa miaka ya 1980.

Fritz Soergel ambaye ni mwanachama wa tume ya uchunguzi kuhusu historia ya matumizi ya madawa hayo aliiambia televisheni ya ZDF kwamba kandanda ni mchezo wa umma na ulio muhimu zaidi nchini Ujerumani. Mjumbe wa tume hiyo Andreas Singler alisema katika taarifa kwa vyombo vya habari mapema wiki hii ambapo akitoa maelezo kwa mukhtasari juu ya ruipoti ya kurasa 60 kwamba, kilabu ya Stuttgart ilihusika kwa kiwango kikubwa wakati Freiburg wakati huo ikiwa katika ligi ya daraja la pili, nayo pia ilihusika katika matumizi ya dawa za kuongeza nguvu mwilini zilizopigwa marufuku.

Hata hivyo Stuttgart imesisitiza kwamba daktari wa michezo Armin Kluemper ambaye ni profesa wa chuo kikuu anayetajwa kuwa mstari wa mbele katika kashfa hiyo hakupata kuajiriwa na Stuttgart kuwa daktari wa kilabu. Freiburg nayo imesema bila ya kuiona ripoti kamili haiwezi kulichunguza kikamilifu suala hilo.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman
Mhariri: Josephat Charo