1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

FIFA kutathmini ripoti kuhusu Urusi na Qatar

21 Novemba 2014

Shirikisho la kandanda duniani FIFA limesema litafanya mapitio mapya ya uchunguzi kuhusiana na kuwania kuwa mwenyeji wa fainali za kombe la dunia mwaka 2018 na 2022 nchini Urusi na Qatar

https://p.dw.com/p/1DrKa
FIFA Ethikkommission Garcia Eckert
Picha: Sebastien Bozon/AFP/Getty Images

Hiyo ni katika hatua ya kupanua nafasi ya kupatikana kwa ripoti iliyoandikwa na mwendesha mashataka wa zamani wa Marekani kuhusiana na madai ya rushwa.

Hatua hiyo ilitangazwa baada ya mkutano mjini Zurich kati ya mkuu wa uchunguzi huo Michael Garcia, ambaye aliongoza uchunguzi uliodumu miezi 18 kuhusiana na utata wa kampeni za Urusi na Qatar, pamoja na jaji kutoka Ujerumani Hans-Joachim Eckert. Watu hao wawili wamekuwa katika mvutano kuhusiana na ni kiasi gani cha ripoti hiyo kiwekwe hadharani.

Wakati huo huo katibu mkuu wa zamani wa FIFA Jerome Champagne amesema wiki hii ana matumaini uchaguzi wa rais wa shirikisho hilo mwakani utafanyika katika utaratibu wa usawa. Mgombea huyo raia wa Ufaransa ndie pekee aliyethibitisha kupambana na rais wa sasa Joseph Blatter katika uchaguzi utakaofanyika Mei 29 mwaka 2015.

Champagne amesema fainali za kombe la dunia mwaka 2022 zitafanyika nchini Qatar pale tu iwapo ukandamizaji wa wafanyakazi wahamiaji utakapositishwa.

Nalo shirikisho la kandanda barani Ulaya UEFA litafanya uamuzi juu ya iwapo litambue michezo inayochezwa na klabu za jimbo la Crimea chini ya sheria za shirikisho la kandanda la Urusi , Desemba 4 mwaka huu , amesema hayo rais wa UEFA Michel Platini.

Timu tatu za jimbo hilo zimeruhusiwa kucheza katika ligi ya Urusi kufuatia matatizo ya kisiasa katika jimbo hilo. Shirikisho la kandanda la Ukraine limeiomba FIFA na UEFA kuweka vikwazo dhidi ya shirikisho la kandanda la Urusi kwa kile ilichokieleza kuwa ni ukiukaji mkubwa wa sheria za soka.

Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / afpe / rtre

Mhariri: Mohammed Khelef