1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Eneo takatifu lafunguliwa tena Jerusalem

31 Oktoba 2014

Israel Ijumaa (31.10.2014) imefungua tena eneo takatifu la Jerusalem na kuwaweka askari wa usalama zaidi ya 1,000 kufuatia mapambano kati ya Wapalestina na polisi wa kutuliza ghasia wa Israel.

https://p.dw.com/p/1DfGL
Msikiti wa Al-Aqsa ulioko katika eneo takatifu la Jerusalem linalogombaniwa kati ya Wapalestina na Israel.
Msikiti wa Al-Aqsa ulioko katika eneo takatifu la Jerusalem linalogombaniwa kati ya Wapalestina na Israel.Picha: AFP/Getty Images/Ahmad Gharabli

Makundi madogo ya waumini wa Kipalestina yameingia kwenye eneo hilo ambalo linajulikana kama Mlima Mzeituni kwa Wayahudi na Masjid Al-Aqsa kwa Wapalestina kwa kupitia vituo kadhaa vya ukaguzi vya Israel huku mvua ikinyesha.

Hakuna mapigano yaliyoripotiwa baada ya kumalizika kwa sala wakati wa mchana juu ya kwamba askari wa usalama wa Israel walifyetuwa gesi za kutowa machozi mara kadhaa kwa vijana wa Kipalestina waliokuwa wakivurumisha mawe ambao walijikusanya katika kituo cha ukaguzi cha Qalandiya karibu na mji wa Ukingo wa Magharibi wa Ramallah.

Hakukuwa pia na repoti zilizopatikana mara moja kuhusu majeruhi au watu waliokamatwa.

Eneo takatifu la Jerusalem limekuwa eneo la mvutano kati ya waaumini wa dini mbili kwa miongo kadhaa sasa na kutilia mkazo kipengee cha kidini kilioko katika mzozo wa Wapalestina na Israel.Ziara iliofanywa na kiongozi wa upinzani wakati huo Ariel Sharon hapo mwaka 2000 ilianzisha vuguvugu la uasi wa mwisho wa Wapalestina dhidi ya utawala wa Israel.

Kuepusha ghasia

Serikali ya Israel ilisema inapunguza watu wanaoingia kwenye eneo hilo Ijjumaa kwa kutaka wanaume wa Kiislamu wawe wale wenye umri uliopindukia miaka 50 ikiwa kama ni juhudi za kupunguza uwezekano wa kuzuka ghasia zilizochochewa na kuuwawa hapo Alhamisi kwa mwanaume wa Kipalestina anayetuhumiwa kujaribu kumuuuwa mwanaharakati wa Kiyahudi wa siasa kali.

Wanajeshi wa Israel wakilinda eneo takatifu la Jerusalem.30.10.2014
Wanajeshi wa Israel wakilinda eneo takatifu la Jerusalem.30.10.2014Picha: Getty Images/J. Guez

Muisrael-Mmarekani rabbi Yehuda Glick alipigwa risasi mara tatu hapo Jumatano usiku lakini hali yake hivi sasa inaelezwa kuwa sio mbaya.Glick amekuwa akifanya kampeni kwa Wayahudi zaidi kuruhusiwa kuingia katika eneo hilo jambo ambalo limekuwa likipiganiwa na wanaharakati wa kidini wa sera za utaifa ambao wanauchukia msimamo wa muda mrefu wa Israel wa kutowaruhusu Wayahudi kufanya ibada mahala hapo.

Tangazo la vita

Wakichochewa na harakati za mshirika wa sera kali za mrengo wa kulia wa serikali ya mseto ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu,Wayahudi wengi zaidi wamekuwa wakilitembelea eneo hilo katika miezi ya hivi karibuni na kusababisha upinzani mkali kutoka kwa Waislamu wanaohofia ushawishi mkubwa zaidi wa Israel kwa Jerusalem kutokana na kuongezeka kwa maakaazi ya walowezi ya Kiyahudi katika sehemu ya Wapalestina ya mji huo.

Vijana wa Kipalestina wakipambana na polisi wa Israel Jerusalem ya mashariki.30.10.2014.
Vijana wa Kipalestina wakipambana na polisi wa Israel Jerusalem ya mashariki.30.10.2014.Picha: Getty Images/J. Guez

Kwa mara ya kwanza tokea ziara ya Sharon Israel ililifunga eneo hilo kwa muda mfupi hapo Alhamisi hatua ambayo kiongozi wa Wapalestina Mahmoud Abbas ameita kuwa tangazo la vita dhidi ya Wapalestina na ulimwengu mzima wa Waarabu na Waislamu.Awali Abbas alitaka Wayahudi wapigwe marufuku katika eneo hilo na kuwataka Wapalestina kulilinda eneo hilo dhidi ya Wayahudi wanaolizuru ambao amewaita mchunga wa n'gombe.

Eneo hilo ni takatifu kabisa kwa dini ya Kiyahudi na la tatu kwa utakatifu kwa dini ya Kiislamu.Wayahudi wanasema ni mahala ambapo ulikuweko mlima wa mzeituni uliotajwa kwenye biblia wakati Waislamu wanasema ni mahala ambapo Mtume Muhammad (SAW) alipandishwa peponi.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AP

Mhariri:Josephat Charo