1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ebola yaiweka dunia kwenye taharuki

Mohammed Khelef11 Oktoba 2014

Shirika la Afya Duniani (WHO) linaonya idadi ya watu waliokufa kwa ugonjwa hatari wa Ebola imepindukia 4,000 na kama hali haikudhibitiwa haraka zaidi ya watu milioni 1 watakuwa wameambukizwa kufikia Januari 2015.

https://p.dw.com/p/1DTXR
Kampeni ya kuchunguza Ebola, Casablanca, Morocco.
Kampeni ya kuchunguza Ebola, Casablanca, Morocco.Picha: picture alliance/AP Images/A. Bounhar

WHO inasema watu 4,033 wamefariki dunia kutokana na Ebola hadi kufikia tarehe 8 Oktoba kati ya wagonjwa 8,399 waliosajiliwa katika nchi saba duniani. Takwimu hiyo mpya inazuka katika wakati ambapo shirika hilo likisema kuwa fedha za msaada zilizohitajika kupambana na mripuko wa maradhi hayo zikiwa na nakisi ya dola bilioni 1.

Licha ya kwamba takribani maambukizi na vifo vyote vimetokea barani Afrika, kuambukizwa kwa muuguzi mmoja nchini Uhispania akiwa anawahudumia raia wawili wa nchi hiyo waliokuwa wamerejeshwa nyumbani baada ya kuuguwa nchini Sierra Leone na Liberia, kumeongeza wasiwasi wa kimataifa.

Uhispania yaimarisha kampeni dhidi ya Ebola

Siku ya Jumamosi (11 Oktoba), maafisa wa serikali ya Uhispania walitazamiwa kukutana kwenye kamati maalum inayoshughulika na hali ya dharura, huku kukiwa na miito ya kuimarishwa kwa itifaki ya afya na kuchunguza mapungufu yaliyosababisha muuguzi huyo, Teresa Romero, kuambukizwa Ebola.

Uwanja wa Kimataifa wa John F. Kennedy, New York, Marekani.
Uwanja wa Kimataifa wa John F. Kennedy, New York, Marekani.Picha: picture-alliance/dpa/J. Lane

Wafanyakazi wa huduma za afya waliliambia shirika la habari la AFP kwamba ghorofa iliyowekwa kwenye karantini katika Hospitali ya Carlos II mjini Madrid, ambako Romero ndiko alikoambukizwa, ilifungwa mwaka jana kutokana na mipango ya kukata matumizi na ilifunguliwa tena pale tu wamishionari wawili walipoletwa kutoka Afrika wakiwa tayari wameshaambukizwa Ebola mwezi Agosti.

Waziri Mkuu Mariano Rajoy alitembelea hospitali hiyo, huku Romero akisemekana kuwa kwenye hali mbaya ingawa thabiti.

Jitihada za kilimwengu

Kwa upande wake, serikali ya Canada siku ya Ijumaa (10 Oktoba) iliwataka raia wake kuondoka kwenye mataifa ya Afrika ya Magharibi yaliyoathirika vibaya zaidi na Ebola, huku ikichukuwa hatua kali kwenye mipaka yake kwa kuwapima wasafiri ambao wanatoka maeneo hayo.

Wanajeshi wa Marekani wakijitayarisha kuelekea kwenye kampeni dhidi ya Ebola Afrika ya Magharibi.
Wanajeshi wa Marekani wakijitayarisha kuelekea kwenye kampeni dhidi ya Ebola Afrika ya Magharibi.Picha: Reuters/H. McClary

Hatua kama hizo zinachukuliwa pia na Uingereza na Marekani kwenye viwanja vyake vyote vikubwa vya ndege. Taasisi ya Udhibiti wa Maradhi ya Marekani CDC,inakisia kuwa idadi ya watu walioambukizwa Ebola inaweza kufikia milioni 1.4 kufikia Januari 2015, ikiwa hatua kali hazikuchukuliwa kuyadhibiti maradhi hayo.

Kutoka Australia hadi Zimbabwe, na Brazil hadi Uhispania, watu wanaoonesha ishara za homa au waliowahi kukutana hivi karibuni na wagonjwa wa Ebola wamewekwa kwenye vitengo maalum vya uchunguzi au kuamuriwa kubakia majumbani mwao.

Fedha zaidi zinahitajika

Umoja wa Mataifa na viongozi wa mataifa yaliyoathirika vibaya kwa Ebola - Guinea, Liberia na Sierra Leone - wametoa wito wa msaada zaidi kwenye mstari wa mbele wa mapambano dhidi ya Ebola barani Afrika.

Mtu anayeshukiwa kuwa na Ebola akihamishiwa hospitali nchini Brazil.
Mtu anayeshukiwa kuwa na Ebola akihamishiwa hospitali nchini Brazil.Picha: Reuters/Mauro dos Santos (

Rais wa Guinea siku ya Ijumaa alikutana na Mkurugenzi wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), Christine Lagarde, aliyeahidi kuwa shirika hilo "lilikuwa tayari kufanya mambo mengine zaidi ikihitahika" katika kupambana na maradhi hayo.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Jan Eliasson, alisema ni robo moja tu ya "dola bilioni moja zinazohitajika" kupambana na maradhi hayo ndizo ambazo zimeahidiwa kutolewa hadi sasa. Aliomba wapatikane madaktari, wauguzi na wafanyakazi zaidi wa huduma ya afya.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/AP
Mhariri: Caro Robi