1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa Tuareg wajitangazia uhuru kaskazini mwa Mali

6 Aprili 2012

Vuguvugu la Ukombozi wa Azawad (MNLA) limetangaza kile ilichokiita "uhuru wa Azawad" kupitia taarifa kwenye mtandao na pia kupitia msemaji wao aliyezungumza na kituo cha televisheni cha France 24.

https://p.dw.com/p/14YpD
Mpiganaji wa Tuareg karibu na msikiti katika mji wa kihistoria wa Timbuktu kaskazini mwa nchi hiyo.
Mpiganaji wa Tuareg karibu na msikiti katika mji wa kihistoria wa Timbuktu kaskazini mwa nchi hiyo.Picha: Reuters

"Tunatangaza rasmi uhuru wa Azawad kuanzia leo," alisema Mussa Ag Attaher, ambaye aliongeza kwamba waasi hao wataheshimu "mipaka ya mataifa mengine."

MNLA imesema kwamba kutokana na mafanikio yao ya kuliteka eneo wanaloliita Azawad, wanasimamisha mara moja operesheni za kijeshi kuanzia usiku wa jana.

Katika tangazo hilo "la uhuru", Ag Attaher alisema: "Tunakubali dhamana na dhima kamili inayotuwajibikia kuilinda ardhi yetu. Tumekamilisha jukumu muhimu la ukombozi...sasa kazi kubwa zaidi iko mbele yetu."

Kabla ya tangazo hili kutolewa, jioni ya jana wanamgambo wa Kiislamu wenye silaha waliuvamia ubalozi mdogo wa Algeria ulio kwenye mji wa kaskazini mashariki mwa Mali, Gao, na kuwateka nyara wanadiplomasia saba.

Ag Attaher ameuita utekaji nyara huo kuwa ni jambo baya sana na kwamba kundi lake mwanzoni liliupinga vikali, ila baadaye lilipaswa kwenda nao ili kuokoa maisha ya watu walioshikiliwa.

Wanadiplomasia wa Algeria watekwa nyara

Wizara ya Mambo ya Nje ya Algeria imesema watu wenye silaha na waliobeba bendera za kundi la kidini la Salafi waliuvamia ubalozi wao na kuondoka na balozi wake na wafanyakazi wengine sita.

Kiongozi wa mapinduzi ya kijeshi wa Mali, Amadou Haya Sanogo.
Kiongozi wa mapinduzi ya kijeshi wa Mali, Amadou Haya Sanogo.Picha: dapd

Huku waasi wa Tuareg wakitangaza mafanikio ya mapambano yao ya miaka kadhaa kupigania uhuru wa eneo lao, washirika wao wa zamani waliogeuka kuwa maadui, wanamgambo wa Ansaruddin, wameanza kuweka utawala wa sheria za Kiislamu katika baadhi ya sehemu za kaskazini mwa Mali.

Kundi hilo linaloongozwa na Iyad Ag Ghaly ndilo hasa linaloonekana kuwa watawala wapya wa maeneo yaliyotekwa na waasi kaskazini mwa Mali. Chanzo kimoja katika jeshi la Mali kimeiambia kwamba jeshi hilo lina taarifa kwamba MNLA hawana dhamana yoyote kwa sasa, na badala yake ni kile kinachoitwa tawi la al-Qaida katika Sahel (AQIM), ndilo lenye udhibiti wa eneo hilo.

Taarifa iliyotumwa kwenye mtandao wa MNLA imeeleza dhamira ya waasi hao "kujenga mazingira ya kuwa na amani ya kudumu, kuanzisha taasisi za msingi kwa dola lililo na katika ya kidemokrasia kwa Azawad huru."

Kamati kuu ya MNLA imeitaka jumuiya ya kimataifa kulitambua mara moja taifa la Azawad, ingawa hadi sasa hakuna taifa lolote duniani lililotangaza kuutambua uhuru huo.

Hadi sasa hakuna taarifa zozote kutoka Baraza la Kijeshi lililochukuwa madaraka kwa nguvu mwezi uliopita kuhusiana na tangazo hili la uhuru wa Azawad.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Dahman