Urusi imekanusha uvumi kwamba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakaribia kupata muafaka juu ya mswada wa azimio linalolenga kusimamisha umwagaji damu nchini Syria.
Wanadiplomasia wamesema kuwa balozi wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa Vitaly Churkin ameeleza bayana mbele ya kikao cha faragha cha baraza kwamba angetumia kura ya turufu ya nchi yake kuupinga mswada huo iwapo kura itapigwa leo Ijumaa. Nchi kumi na tano wanachama wa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zimegawanyika juu ya mswada unaoungwa mkono na Ulaya pamoja na nchi za kiarabu, ambao unaitaka serikali kukomesha ukandamizaji dhidi ya waandamanaji, na kuidhinisha mpango wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kutekeleza mageuzi ya kisiasa nchini Syria.
Jana, wanadiplomasia walisema wameridhia matakwa ya Urusi kwa kuondoa kipengele kinachomtaka Rais wa Syria Bashar al Assad kuondoka madarakani.