Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema Umoja wa Ulaya unaweza kuweka vikwazo vipya dhidi ya utawala wa Rais Bashar Al- Assad wa Syria, bila kufafanua zaidi juu ya hatua hiyo. Merkel ametoa kauli hiyo leo, kabla ya kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Nabil al- Arabi, anayeitembelea Ujerumani. Kwa upande wake Arabi ametoa wito wa kukomeshwa mara moja kwa umwagaji damu unaoendelea kushuhudiwa Homs na Baba Amri, baadhi ya maeneo ambayo vikosi vya Syria vinayashambulia. Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa kujadili uwezekano wa kuiwekea Syria vikwazo zaidi mwishoni mwa mwezi huu. Wanadiplomasia wanahisi hatua hiyo itahusisha kuzizuia benki za Syria kuendesha shughuli zao katika nchi za Umoja wa Ulaya na kuweka marufuku kwa ndege za kibiashara zinazofanya safari barani Ulaya.
Ufaransa inatafakari mapendekezo yote yaliyotolewa na wanachama 22 wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu katika Umoja wa Mataifa, yanayoeleza namna ya kukabiliana na utumiaji nguvu unaofanywa na Jeshi la Syria dhidi ya waandamanaji. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Ufaransa Bernard Valero amesema Ufaransa na washirika wake mjini New York, Marekani wanajadii mapendekezo hayo likiwemo la kupeleka walinda amani nchini Syria. Aidha, Valero amesema nchi hizo hazina budi kufanya mazungumzo ya kina na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na washirika wengine wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kabla ya kufikia maamuzi. Wakati huo huo, Waziri wake wa Mambo ya Nje Hillary Clinton, amesema nchi yake itaendelea kuiwekea vikwazo Syria, mpaka hapo utawala wa Bashar Al- Assad utakapoacha kuwatesa wananchi wake. "Tutazidisha shinikizo la kidiplomasia dhidi ya Utawala wa Assad na tutazidisha vikwazo dhidi yake. Tutaendelea kuileta Jumuiya ya Kimataifa pamoja na kujaribu kukomesha machafuko yanayofanywa na utawala wa Assad", amefafanua Clinton.
Rais wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad kesho anatarajiwa kuzindua mafanikio ya kinyuklia ambayo hakuyafafanua, hatua inayoelezwa na wataalamu kuwa ni mafanikio hayo yatakayoudhihirishia Ulimwengu uwezo mkubwa na maarifa waliyonayo Wairan. Taarifa hiyo iliyochapishwa katika tovuti ya serikali inathibitisha kiapo alichokula Ahmadinejad, cha kuzindua miradi muhimu ya kinyuklia, Jumamosi iliopita katika hotuba yake ya kuadhimisha miaka 33 ya mapinduzi ya taifa hilo la Kiislamu. Mataifa ya Magharibi na Israel yanaituhumu Iran kuwa ina mpango wa kuunda kutengeneza bomu la atomiki, lakini Iran inakanusha ikidai kuwa mpango wake wa nyuklia ni wa amani.
Wamisri wanapiga kura leo katika hatua ya pili na ya mwisho wa baraza la juu la bunge la taifa , ambalo ni chombo cha ushauri kisichokua na madaraka ya uamuzi . Zoezi hilo ni la siku mbili litakalohusisha majimbo 14 kati ya 27, wakati duru ya pili ikipangwa kufanyika tarehe 22 na 23 mwezi huu. Katika uchaguzi wa bunge mwezi Novemba mwaka jana uliokuwa wa kwanza tangu vuguvugu lililomuangusha rais Hosni Mubarak mwaka mmoja uliopita ,vyama vya kiislamu vilifanya vizuri vikijinyakulia asilimia 47 ya viti bungeni.
Mtawala wa Kuwait ametangaza serikali mpya, na kumtaja Sheik Jaber Al Hamad Al Sabah kuwa Waziri Mkuu ambaye atashikilia wadhifa huo kabla ya uchaguzi wa bunge kufanyika. Baraza hilo jipya la mawaziri lina wanafamilia wanne wa Ufalme, miongoni mwa nafasi 16 na hii ni mara ya kwanza tangu mwaka 2005 kwa baraza hilo kutokuwa na waziri hata mmoja mwanamke. Katika bunge la sasa, pia hakuna mbunge mwanamke. Mwaka jana bunge hilo lilikuwa na wabunge wanawake wanne. Bunge jipya la mwaka huu lina viti 50 na vingi vimenyakuliwa na wabunge wa kambi ya upinzani wakiwemo Waislamu wenye itikadi kali.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tunisia amekishutumu kikundi cha wanamgambo kilichopambana na vikosi vya usalama katikati ya mji mkuu wa Tunisia mwezi uliopita, kuwa kinashirikiana na mtandao wa kigaidi wa Al- Qaeda. Waziri huyo Ali Laarayedh amesema watu hao 12 walioko chini ya ulinzi wana mawasiliano na seli za Al- Qaeda zilizopo Libya na ndiko wanakochukua silaha zao. Walipambana na askari katika Mji wa Bir Ali Ben Khalifa siku ya mwaka mpya. Serikali za nchi za eneo la Afrika Kaskazini zinahofia silaha hizo kupelekwa kwa wafuasi wa Tawi la Al- Qaeda katika nchi za Maghreb AQIM na makundi mengine yanayoshirikiana nao.
Vikosi vya Serikali ya Senegal vimepambana na watu wanaoshukiwa kuwa waasi wanaotaka kujitenga katika mji wa Casamance, na kusababisha vifo vya askari watatu na wengine sita kujeruhiwa. Vyanzo vya habari vya Jeshi na hospitali, vimethibitisha idadi hiyo ya vifo na majeruhi, yaliyotokea usiku wa kuamkia leo. Wakati huo huo, Rais wa Senegal Abdoulaye Wade, amekutana na Balozi wa Marekani mjini Dakar, Lewis Lukens, ambaye juma lililopita alikosoa nia ya kiongozi huyo kutaka kuongoza nchi hiyo kwa muhula wa tatu. Baada ya mkutano huo, Lukens amesema mazungumzo baina yake na Wade yalikuwa na manufaa na ameongeza kuwa Marekani ingependa kuona Senegal inafanya uchaguzi wa amani, uwazi na unaozingatia demokrasia. Tarehe 7 mwezi huu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Senegal Madicke Niang, alimwita Lukens ofisini kwake ajieleze baada ya balozi huyo kuhojiwa na kutoa shutuma kali katika vyombo vya habari vya Senegal.
Mlipuaji mmoja wa kujitoa mhanga amefariki dunia baada ya kujilipua mbele ya ofisi ya kamati ya uchaguzi mjini Aden, hii leo juma moja kabla ya raia wa Yemen kumchagua Rais mpya kufuatia kuondolewa madarakani kwa Ali Abdullah Saleh. Shambulio hilo linatafsiriwa kama ishara ya kupinga zoezi la uchaguzi mkuu wa Jumanne ijayo, ambao unapingwa na waasi wa Kusini mwa Yemen, waasi wa Kishia waliopo Kaskazini na wanamgambo wa Kiislam. Saudi Arabia na Marekani zinaamini uchaguzi mkuu huo, utamaliza ghasia zilizoibuka nchini humo, ambazo zinaonekana kutoa mwanya kwa kundi la kigaidi la Al- Qaeda, kujiimarisha katika eneo zima la usafirishaji mafuta katika Bahari ya Sham.
Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.de.