1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Die Mannschaft yalakiwa kwa shangwe Berlin

15 Julai 2014

Moja kati ya hafla kubwa kabisa katika historia ya Ujerumani imefanyika leo(15.07.2014) mjini Berlin, ambako mamia kwa maelfu ya Wajerumani waliwalaki mashujaa wao wa katika eneo maarufu la lango la Brandenburg.

https://p.dw.com/p/1CdcX
Weltmeister Feier Berlin 15.07.2014
Picha: Alex Grimm/Bongarts/Getty Images

Mashujaa hao wa Die Mannschaft , walikaribishwa kishujaa nchini Ujerumani mjini Berlin. Kikosi cha wachezaji 23 wa timu ya Ujerumani kiliwasili katika uwanja wa ndege wa Tegel kikiwa kimechelewa kwa muda wa saa moja kutokana na uchelewesho wakati wa kuondoka mjini Rio de Janeiro.

Wa kwanza kujitokeza kutoka katika ndege hiyo ya shirika la ndege la Ujerumani Lufthansa alikuwa nahodha wa Die Mannschaft , Philipp Lahm , ambaye alinyanyua juu kombe hilo la dunia wakati akiteremka kutoka katika ndege hiyo.

Weltmeister Feier Berlin 15.07.2014 Bus
Basi la timu ya taifa likipita mjini BerlinPicha: picture-alliance/dpa

Hali nzuri ya hewa na sherehe

Kukiwa na hali nzuri ya hewa katika mji huo mkuu wa Ujerumani , watu wengi wakipepea bendera ya Ujerumani na kuvalia nguo zenye rangi ya dhahabu, nyeusi na nyekundu walianza kukusanyika katika eneo hilo la kujikusanya mashabiki kuanzia majira ya asubuhi leo.

Kiasi ya watu laki nne wanakadiriwa kuwa wamehudhuria hafla hiyo ya kuwakaribisha mashujaa wa kombe la dunia, ambapo kikosi hicho kilionekana katika basi la wazi lililoandikwa miaka ambayo Ujerumani ililinyakua kombe hilo , yaani 1954, 1974, 1990 na mwaka huu 2014 ikiwa ni mara ya nne na kuzunguka mjini Berlin.

Kikosi hicho hatimaye kiliwasili katika eneo la lango la Brandenburg na kupokewa kishujaa.

"Sisi wote ni mabingwa wa dunia," amesema kocha Joachim Loew, ambaye alivalia miwani ya jua na T-shirt nyeusi ikiwa na namba moja kubwa kifuani, aliwaambia mashabiki waliokusanyika , huku wakiimba , Deutschland !, Deutschland !.

Fußball WM 2014 Fans Jubel
Mashabiki wakifurahia kuwasili kwa timu ya UjerumaniPicha: picture-alliance/dpa

Nini siri ya ushindi

Alipoulizwa siri ya mafanikio, kocha wa Ujerumani Joachim Loew alisema kwa ufupi tu:

"Unahitaji uhalisia. Unahitaji wachezaji wenye uwezo wa asili, ambao wana uwezo wa kuongoza. Na unahitaji vijana , wenye uwezo wa kucheza kandanda."

Anajisiakiaje Joachim Loew kuwa kocha wa kwanza kutoka bara la Ulaya kuweza kuiongoza timu yake kunyakua kombe hilo katika ardhi ya America kusini. Loew Alisema.

"Hili ni suala litakalobakia milele. Mtu wa kwanza kutoka bara la Ulaya kunyakua kombe hili hapa Maracana, mjini Rio , katika ardhi ya taifa la kandanda. Ilikuwa kazi ngumu ya miaka kumi. Tumeweza katika miaka hiyo yote kunyanyua kiwango chetu. Tumekuwa kila mara na kikosi bora, tulijiamini na sasa ni wakati wetu."

Wachezaji walirukaruka na kucheza jukwaani na kuimba , hivi ndio Ujeruamni inavyoshinda , hivi ndio Ujerumani inavyoshinda.

Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe / dpae

Mhariri: Mohammed Abdul Rahman