1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China yazidi kujitanua - wahariri

Mohammed Khelef11 Novemba 2014

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanazungumzia mkutano wa kilele wa APEC nchini China, kura ya maoni ya Catalonia na kashfa ya ngono dhidi ya watoto inayowaandamana wanasiasa hapa Ujerumani.

https://p.dw.com/p/1DlA5
Kiongozi wa China Xi Jinping (kushoto) na wa Japan, Shinzo Abe, wakiachana baada ya kusalimana.
Kiongozi wa China Xi Jinping (kushoto) na wa Japan, Shinzo Abe, wakiachana baada ya kusalimana.Picha: Reuters

Mhariri wa gazeti na Thüringen Zeitung anasema sasa China imekuwa ni zaidi ya soko kubwa tu la bidhaa za Magharibi. Nchi hiyo ina malengo ya wazi ya kimkakati, na si jambo la ajabu kwamba mkutano wa kilele wa APEC mjini Beijing umekuwa na umuhimu wa pekee.

Mataifa jirani yanaiangalia kwa shaka China kwa sababu taifa hili halidai chochote pungufu ya kuwa taifa pekee lenye nguvu kwenye eneo hilo, huku likipunguza dhima ya Marekani kwenye eneo la Bahari ya Pasifiki. Japan na Vietnam zina mzozo wa mpaka wa baharini na China, Taiwan inahofia kutwaliwa na China.

Mhariri anaendelea kwa kusema kuwa China haijitanui Asia tu, bali hata Afrika ambako anasema taifa hilo la pili kwa uchumi mkubwa duniani limekuwa likijikita kwenye tabia ya kibeberu ya kutwaa rasilimali za bara hilo masikini, huku falsafa yake ya “Himaya ya Kati“ ikiendelea.

Lakini kubwa kuliko yote ni kuwa China haiko pekee kwenye hayo. Urusi nayo inakuja juu. Marekani nayo haitaki kuwekwa nyuma.

Mfuasi wa uhuru wa Catalonia.
Mfuasi wa uhuru wa Catalonia.Picha: Reuters/A.Gea

Kura ya maoni ya Catalonia

Mhariri wa gazeti la Badische Zeitung la mjini Freiburg anazungumzia kile kilichoitwa kura ya maoni ya ishara katika jimbo la kaskazini mashariki la Uhispania, Catalonia, iliyofanyika Jumapili, na ambayo itaendelea kwa wiki mbili.

Kwa mtazamo wa mhariri huyo, licha ya kura hiyo kukosa uhalali wa kisheria, Uhispania haikutuma wanajeshi kwenda kuipinga.

Wacatalan walitumia haki yao ya kiraia kwa njia ya wazi na ya amani. Walipiga kura kisha wakaenda nyumbani kupumzika kungojea majibu. "Hakuna aliyefikiria kuongeza mafuta kwenye moto kwa kupeleka vikosi vya kuyalinda maeneo ya jimbo hilo linalodai uhuru wake," anasema mhariri huyo.

Na kwa maoni yake, serikali ya Uhispania ilijizuia pakubwa. Ilikuwa na nguvu na haki ya kuizuia hata kura hiyo ya ishara, ambayo hakika haikuwa kura ya maoni hasa. Maana kilikuwa kitendo cha uchokozi dhidi ya mamlaka ya nchi na ukuu wa katiba. Lakini licha ya kura yenyewe kukosa uhalali, hakuna aliyeguswa wala aliyeumizwa kwenye mzozo huo.

Kiongozi wa Die Grünen, Simone Peter.
Kiongozi wa Die Grünen, Simone Peter.Picha: AFP/Getty Images

Kashfa ya ngono dhidi ya watoto

Tumalizie kwa maoni ya mhariri wa gazeti la Der Tagesspiegel la mjini Berlin juu ya kashfa ya picha za ngono za watoto wadogo, ambayo inawaandama baadhi ya wanasiasa wa hapa Ujerumani. Safari hii ni chama cha walinda mazingira, Die Grüne, kilichozuka na kauli nzito.

Mwenyekiti wa chama hicho, Simone Peter, anasema kwamba Die Grüne kinataka kuchukuwa jitihada maalum za kuliweka suala hilo kuwa ajenda maalum, wakianzia na kulitungia sera na kisha kutoa mafunzo maalum kwa makada wake juu ya mkakati wa kukabiliana nalo. Sababu ni kuwa kampeni za mwaka jana za uchaguzi mkuu wa shirikisho, mada hiyo ilileta madhara makubwa kwa wanasiasa.

Mhariri anahoji kwa nini haya yanazuka leo, ambapo ndani ya kipindi kifupi cha majira ya kiangazi hadi sasa, tayari walau watu wanne wamesharipoti unyanyasaji huo wa kijinsia kwa watoto wadogo?

Mwandishi: Mohammed Khelef
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman
Vyanzo: Thüringen Zeitung, Der Tagesspiege, Badische Zeitung