1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Alexis Tsipras aifikia ndoto yake

26 Januari 2015

Uchaguzi wa bunge nchini Ugiriki, mzozo wa Ukraine,na miaka 70 tangu ilipokombolewa kambi ya mateso ya wanatsi-ya Auschwitz ndio mada zilizogonga vichwa vya habari vya magazeti ya Ujerumani..

https://p.dw.com/p/1EQSP
Wafuasi wa Syriza washerehekea ushindi waoPicha: Reuters/A. Konstantinidis

Tunaanzia Ugiriki ambako wananchi wanaonyesha kuchoshwa na hatua za kufunga mkaja zinazozidi kuwatumbukiza katika hali ya umaskini.Wapiga kura wameamua kufuata ahadi za mabadiliko za kiongozi wa chama cha siasa kali za mrengo wa shoto-Syriza, Alexis Tsipras.Gazeti la "Pforzheimer Zeitung" linaandika:"Kwa mtazamo wa nchi mfano wa Ujerumani,uamuzi wa wagiriki haueleweki, au mtu anaweza kusema, hauna shukurani.Lakini anaefikiri kama hivyo,anashindwa kutambua ukosefu wa matumaini wa wananchi ambao kwa muda wa miaka michache tu wamejikuta wakitumbukia katika hali ya umaskini.Vipi hali itakuwa hivi sasa nchini Ugiriki,hakuna anaeweza kuashiria.La hakika ni kwamba Tsipras na nchi zilizosalia za kanda ya Euro wanaelekea katika uwanja wa malumbano,na ikiwa hakuna atakaetaka kuregeza kamba,hali hiyo inaweza kuleta balaa.Kwa Ugiriki na kwa nchi zote za kanda ya Euro."

Licha ya onyo kutoka nje,wagiriki wameamua kumuunga mkono Tsipras.Gazeti la "Badische Neueste" linashuku kama ahadi alizotoa katika kampeni za uchaguzi ataweza kweli kuzitekeleza.Gazeti linaendelea kuandika:"Tsipras hatokawia kugundua kwamba maneno matamu katika kampeni za uchaguzi nyumbani,hayafui dafu katika jukwaa la kimataifa.Hatokuwa mwanasiasa wa kwanza kunguruma kama simba mwanzoni na kuishia kimya kimya.Ukweli wa mambo atautambua hivi sasa.Msimamao mkali pekee hautasaidia kitu na akiregeza kamba pengine hilo litamsaidia mjini Brussels lakini nyumbani mjini Athen,litamharibia sifa.Si hasha,kama chama chake cha Syriza kikaishia hataimae kuwa "tukio tu" miongoni mwa matukio ya ndani nchini Ugiriki."

Vita Mashariki ya Ukraine

Mzozo wa Ukraine nao pia umegonga vichwa vya habari magazetini hii leo.Gazeti la "Nodwest-Zeitung" linaandika:"Matumaini ya kumalizika haraka mzozo wa Ukraine yanafifia.Hata kama wanasiasa wa pande zinazohasimiana wamekuwa kila mara wakisisitiza azma ya kufikia amani, kwa upande wa pili lakini wanaachia vita viendelee katika eneo la mashariki na matokeo yake hayakadiriki.Hakuna anaependelea kwa dhati ufumbuzi wa amani; si viongozi wa Ukraine wanaowahimiza wananchi wabebe silaha,na wala si serikali ya Urusi inayohadaa kwa kusema eti hawawaungi mkono waasi mashariki ya Ukraine.Kila wakati wananyunyiza mafuta katika cheche za moto.Na wanaotaabika na kuathirika katika mzozo huo wa umwagaji damu si wengine isipokuwa wananchi wa kawaida."

Kumbukumbu muhimu zihifadhiwe

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu miaka 70 tangu kambi za mateso za wanatsi za Auschwitz zilpokombolewa na kufungwa baada ya kumalizika vita vikuu vya pili vya dunia. Idadi ya mashahidi wa visa vya kikatili vilivofanywa na wanazi katika kambi za maangamizi inazidi kupungua. Na uchunguzi wa maoni ya umma umeonyesha asili mia 58 ya vijana hawajui hasa kilichotokea.Gazeti la Kölner Stadt Anzeiger linaandika:"Kila miaka inapopita ndipo nayo inavyokuwa shida kuendeleza kumbukumbu na kuwafanya watu daima wazikumbuke.Sababu ya hayo ni ile hali kwamba mashahidi wanaanza kumalizika.Hakuna, si filamu,hata ile ya Orodha ya Schindler iliyotungwa na Steven Spielberg,na wala si kitabu kitakachoweza kuhadithia jahanam ya Auschwitz au kambi nyengine za maangamizi. Kila mwanafunzi aliyevitembelea vituo vya maangamizi, basi hatosahau kamwe usimulizi wa manusura maishani mwake.Usimulizi wa mashahidi wa historia hauna mbadala.Neema hiyo lakini inatuponyoka."

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Iddi Ssessanga