1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Burkina Faso: Katiba haitabadilishwa

Elizabeth Shoo30 Oktoba 2014

Baada ya maelfu ya watu kuandamana nchini Burkina Faso, hatimaye serikali ya nchi hiyo imesema haitabadili katiba kumwomgezea rais Blaise Compaore muhula mwingine madarakani.

https://p.dw.com/p/1Dedm
Burkina Faso Protest Ausschreitungen Parlament Brand
Picha: Getty Images/ AFP/ Issouf Sanogo

Kituo cha televisheni ya taifa nchini Burkina Faso kilikatisha matangazo yake ghafla kuiruhusu serikali kutoa ujumbe huu: "Serikali inapenda kuwafahamisha wananchi wote kwamba mpango wa kujadili uwezekano wa kubadili katiba umefutwa. Serikali inawaomba raia wawe watulivu."

Lakini ombi hilo halikusikilizwa. Maelfu ya waandamanaji wenye hasira walilivamia jengo la bunge na pia kituo cha televisheni ya taifa. Kituo hicho kililazimika kukatisha matangazo yake. Watu walioshuhudia matukio hayo kwa macho wanasema kwamba milio ya risasi imesikika kutoka ikulu ya rais. Hivi sasa maaskari wapatao 500 wamejiunga kuandamana.

Hali tete Ouagadougou

Kuna ripoti kwamba maafisa wa usalama wamewaua watu watatu na kuwajeruhi wengine, baada ya waandamanaji kujaribu kuivamia nyumba ya kaka yake rais Blaise Compaore. Polisi walifyatua pia risasi na kuwarushia waandamanaji mabomu ya machozi.

Machafuko mji mkuu wa Burkina Faso, Ouagadougou
Machafuko mji mkuu wa Burkina Faso, OuagadougouPicha: Getty Images/ AFP/ Issouf Sanogo

Moshi mweusi ulionekana ukipanda kutoka bungeni baada ya waandamanaji kuwasha moto ndani ya jengo hilo na pia kupora komputa na televisheni. Wengine waliiba hata pikipiki za polisi, kama anavyoeleza mwandishi mmoja wa shirika la habari la Reuters.

Wabunge wa Burkina Faso walikuwa wapige kura kubadili katiba ili imruhusu rais Compaore kuwania tena madaraka mwaka kesho. Mwanasiasa huyo amekuwa akiiongoza nchi yake tangu mwaka 1987.

Kiongozi wa upinzani, Zephirin Diabre, amesema kupitia mtandao wa Twitter kwamba anapinga aina yoyote ya mapinduzi. Vituo vya redio nchini Burkina Faso pamoja na duru za kidiplomasia zinaeleza kwamba viongozi wa upinzani wamefanya mazungumzo na jenerali Kouame Lougue kuhusu uwezekano wa kuwepo kwa kipindi cha mpito. Duru hizo hizo za kidiplomasia zinasema kwamba watu wa familia ya Compaore waekamatwa katika uwanja wa ndege wakijaribu kukimbilia nje ya nchi.

Waandamanaji wanamtaka rais Blaise Compaore aachie madaraka
Waandamanaji wanamtaka rais Blaise Compaore aachie madarakaPicha: AP

Jumuiya ya kimataifa yamkosoa Compaore

Ufaransa imemtaka Compaore azingatie sheria za utawala za Umoja wa Afrika, sheria zinazokataza mabadiliko ya katiba kwa ajili ya kumruhusu kiongozi kuongeza muda wa kukaa madarakani. Marekani pia imemkosoa Compaore kwa kutaka kubadili katiba, ikisema inaghadhabishwa na matukio yanayoendelea Burkina Faso.

Upinzani dhidi ya Compaore umekuwa ukiongezeka katika miaka ya hivi karibuni. Hata washirika wake na maafisa wa jeshi wameuwa wakizikosoa siasa zake. Jumanne mamia kwa maelfu ya watu walikusanyika katika mitaa ya Ouagadouguo na katika miji mingine kwa kile ambacho upande wa upinzani ulikiita kampeni ya kupinga mabadiliko ya katiba.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/reuters/afp

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman