1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Katiba Tanzania kwenye mtihani mzito

26 Machi 2014

Wakati kikao cha Bunge Maalum la Katiba nchini Tanzania kikiahirishwa tena, dalili zinaonesha hali ni ngumu na uwezakano wa kufikia muafaka kwa hatima ya taifa hilo la mashariki ya Afrika uko mbali kupatikana.

https://p.dw.com/p/1BVsI
Bendera ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Bendera ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Picha: Roberto Schmidt/AFP/Getty Images

Asubuhi ya leo, Spika Samuel Siita anayeongoza bunge hilo maalum alitumia dakika zisizodi 20 kuongoza kikao na baadaye kukiahirisha, licha ya jioni ya jana (25 Machi 2014) kusema kwamba ajenda za leo zingejumuisha ruhusa ya mjadala wa hotuba ya wiki iliyopita iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete kwenye bunge hilo na kuzua utata mkubwa.

Pia ilikuwa imekubalika kuwa hata hotuba ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, nayo ingelijadiliwa na wajumbe wa Bunge hilo la kwanza la aina yake ndani ya kipindi cha miaka 50 ya Muungano wa Tanzania.

Bunge lagawika tena

Hata hivyo, wakati akiahirisha kikao cha leo, Spika Sitta alitangaza kwamba hotuba hizo zisingelikuwa tena sehemu ya mjadala wa sasa.

Mmoja wa waasisi wa Muungano wa Tanzania ambao umekuwa mada kuu kwenye Katiba Mpya, Marehemu Mwalimu Julius Nyerere.
Mmoja wa waasisi wa Muungano wa Tanzania ambao umekuwa mada kuu kwenye Katiba Mpya, Marehemu Mwalimu Julius Nyerere.Picha: Getty Images/AFP

"Baada ya hoja mbalimbali kujitokeza hapa (bungeni) nilikuwa nimeridhika kwamba kungelikuwa na uwezekano wa kujadili hotuba zile mbili nzito (ya Rais Kikwete na Jaji Warioba), lakini baada ya mashauriano ya kina na makundi mbalimbali, imeonekana kwamba kufanya hivyo ni kama kutanguliza mjadala kuhusu rasimu yenyewe ya katiba kabla ya wakati wake." Alisema Spika Sitta akiongeza kwamba badala yake wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wanapaswa kuzichukulia hotuba hizo mbili kama nyenzo za kuwaandaa kuijadili Rasimu ya Katiba na sio kuzijadili hotuba zenyewe.

Kauli hiyo ya Spika Sitta ilipokelewa vyema na wajumbe wanaotokana na Chama tawala cha Mapinduzi (CCM) kwenye bunge hilo, lakini wajumbe kadhaa wanaowakilisha upinzani na makundi mengine yasiyokuwa ya kisiasa walionekana wakiinuka kuomba muongozo.

Hata hivyo, Spika Sitta alitangaza kwamba kikao hicho kifupi kabisa cha asubuhi kisingelipokea muongozo wowote na kwamba miongozo yoyote ingelipata nafasi baadaye jioni ya leo wakati litakaporudi kwenye mjadala.

UKAWA kuendelea kushiriki

Ajenda nyengine ambayo ilikuwa iamuliwe asubuhi ya leo ni ile ya upigaji kura kwenye bunge hilo, iliyowahi kuzua utata kabla ya kuwasilishwa kwa rasimu.

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) na mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Profesa Ibrahim Lipumba.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) na mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Profesa Ibrahim Lipumba.Picha: Mohammed Khelef

Katika wiki mbili nzima za mwanzoni, bunge hilo lilikwama kwenye vifungu namba 37 na 38 vya kanuni za uendeshaji ambavyo vilihusu upigaji wa kura ama ya siri au ya wazi.

Kwa sasa, bunge hilo limekwama juu ya ama wajumbe wa kile kinachotambuliwa kama Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wengi wao kutoka vyama vya upinzani, wataendelea kushiriki kwenye vikao hivyo ama la.

Hii ni baada ya hapo jana kujiuzulu nafasi ya ujumbe kamati ya uongozi wa bunge kwa mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba, baada ya kuteuliwa na Spika Sitta.

Hata hivyo, akizungumza na DW mapema leo, Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe, amesema kwamba bado wataendelea kushiriki kwenye vikao, ingawa wataendelea kupigania mageuzi ya msingi kwenye uendeshaji wa Bunge hilo ambalo linatakiwa kutoka na Katiba Mpya itakayopigiwa kura ya maoni ndani ya kipindi kisichozidi miezi miwili kutoka sasa.

Mwandishi: Mohammed Khelef/DW Kiswahili
Mhariri: Mohamed Abdulrahman