1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brazil kumkosa Neymar nusu fainali na Ujerumani

5 Julai 2014

Brazil na Ujerumani zimefuzu hatua ya nusu fainali baada ya ushindi wa magoli 2-1 na 1-0 dhidi ya Colombia na Ufaransa, na sasa miamba hao wawili watamenyana Jumanne mjini Belo Horizonte, bila Neymar.

https://p.dw.com/p/1CWCC
Fußball WM 2014 Brasilien Kolumbien Viertelfinale
Picha: Reuters

Goli la mapema la nahodha wa Brazil Thiago Silva na mkwaju wa adhabu uliyopigwa na David Luiz kutoka umbali mrefu ilitosha kuwapa ushindi wenyeji wa mashindano hayo na kuwaondoa Colombia katika kinyang'anyiro cha wanane bora mjini Fortaleza.

Nyota wa Colombia James Rodriguez aliondoka uwanjani akibubujikwa machozi, baada ya goli lake la sita la mashindano hayo, ambalo lilitokana na mkwaju wa penati katika dakika ya 80 kutotosha kuizuwia Brazil kusonga mbele katika hatua ya nusu fainali mjini Belo Horizonte siku ya Jumanne.

Neymar akigaaga chini baada ya kuumia uwanjani.
Neymar akigaaga chini baada ya kuumia uwanjani.Picha: Reuters

Furaha ya ushindi yakatizwa na kujeruhiwa kwa Neymar

Ushindi wa Brazil uligubikwa na habari za kusitikisha kwa wenyeji, kufuatia kujeruhiwa kwa nyota wao Neymar ambaye ameelezwa kutoweza kushiriki michezo iliyobaki. Neymar naye aliondolewa machela katika dakika za mwisho za mchezo huo baada ya kuumizwa, na daktari wa timu ya Brazil Rodrigo Lazma aliiambia Televisheni ya Brazil kuwa itamchukua wiki kadhaa kupona. Madaktari wamesema amevunjika uti wa mgongo

Neymar ambaye amefunga magoli manne katika mashindano hayo na kuongoza mashmabulizi ya Brazil, aliumia baada ya makabiliano na Juan Zuniga wa Colombia katika dakika ya 88 na alionekana kuwa na maumivu makali.

Naye nahodha wa timu hiyo Thiago Silva ataukosa mchezo dhidi ya Ujerumani baada ya kupewa kadi mbili za njano, na hivyo kusimamishwa.

Ni marudio ya mwaka 2002

Nusu fainali kati ya Brazil na Ujerumani itakumbushia mashindano ya kombe la dunia ya mwaka 2002 ambayo miamba hao wa Amerika Kusini walishinda kwa magoli 2-0. Hii itakuwa mara ya pili kwa Ujerumani na Brazil kukutana katika nusu fainali, lakini wachezaji wa Brazil, kiungo Hulk na Centre half David Luiz wamesema mechi hiyo ya nusu fainali wanaichukulia kama fainali.

Olivier Giroud wa Ufaransa akisikitika baada ya timu yake kuondolewa na Ujerumani.
Olivier Giroud wa Ufaransa akisikitika baada ya timu yake kuondolewa na Ujerumani.Picha: Reuters

Ujerumani imeweka rekodi ya kufuzu hatua ya nusu fainali kwa mara ya nne mfululizo baada ya goli la kichwa la mchezaji wa Borussia Dortmund Mats Hummels kuwasaidia kuishinda Ufaransa goli 1-0 katika uwanja wa Maracana mjini Rio de Janeiro.

Hummels ambaye ndiye alikuwa mchezaji bora wa mechi hiyo, alieleza kushangazwa na mafanikio waliyoyafikia hadi sasa katika mashindano hayo, akiongozea kuwa ndoto inakaribia kuwa ya kweli sasa.

Kwa upande wake kocha wa Ujerumani Joachim Löw, amesema timu yake itakuwa na wakati mgumu katika nusu fainali hiyo kwa kuzingatia kuwa Brazil itakuwa inachezea nyumbani ambako ina mashabiki wengi.

Michezo ya robo fainali inaendelea jioni ya leo ikizikutanisha Uholanzi na Costa Rica na Ubelgiji itatoana jasho na Argentina.

Mwandishi. Iddi Ismail Ssessanga/rtre,ape,afpe
Mhariri: Abdul Mtullya