1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bolt na Mo Farah kuwika mjini Glasgow

21 Julai 2014

Nyota wa mbio za kasi Mjamaica Usain Bolt na Muingereza Mo Farah wanatarajiwa kugonga vichwa vya habari tena wakati mashindano ya Riadha ya Jumuiya ya Madola yatakapoanza Jumatano wiki hii mjini Glasgow.

https://p.dw.com/p/1CgDb
Leichtathletik-WM Moskau
Picha: picture-alliance/dpa

Bolt, anayeshikilia rekodi ya ulimwengu katika mbio za mita 100 na 200 pamoja na bingwa mara mbili wa Olimpiki na ulimwengu, amekuwa akisisitiza tangu ushindi wake wa mashindano ya ubingwa wa dunia mjini Moscow mnamo mwaka wa 2013, kuwa michezo ya Jumuiya ya Madola ndiyo lengo lake.

Kwa hivyo Mjamaica huyo atakuwa nchini Scotland kuongeza msisimko kwa mashindano hayo ambayo huzishirikisha karibu nchi 71, hasa ambazo zilikuwa koloni za Uingereza.

Leichtathletik WM Moskau Mo Farah
Mo Farah ni Muingereza mwenye asili ya KisomaliPicha: Reuters

Lakini Bolt, ambaye pia ni mshindi mara sita wa dhahabu katika michezo ya Olimpiki, na anayeshiriki katika michezo ya Jumuiya ya Madola kwa mara ya kwanza mjini Glasgow, huenda atashiriki tu katika mbio za masafa mafupi za mita mia nne wachezaji wanne kupokezana vijiti. Hii ni kwa sababu hakushiriki katika mashindano ya ubingwa wa kitaifa nchini Jamaica. Wanariadha wa Jamaica Shelly-Ann Fraser-Pryce na Veronica Campbell-Brown, ni miongoni mwa nyota watakaowika kwa upande wa wanawake.

Kando na Mo FARAH wa Uingereza, pia Mkenya David Rudisha, bingwa wa Olimpiki katika mbio za mita 800 ambaye pia anashikilia rekodi ya ulimwengu wanatazamiwa kuwasisimua mashabiki.

Kwa upande wa Kenya, kikosi cha wanaume cha mbio za masafa marefu kinataraji kumaliza miaka 12 ya kutofanya vyema mjini Glasgow. Baada ya kutawala mbio zote katika Michezo ya 2002 mjini Manchester, Kenya imekuwa ikizidiwa nguvu na mahasimu wao wa Uganda katika Michezo ya karibuni ya Jumuiya ya Madola nchini Australia na India. Pia walipoteza mataji ya mbio za mita 5,000 na 10,000 yaliyonyakuliwa na Mo Farah katika Michezo ya Olimpiki 2012 na mashindano ya Ubingwa wa dunia 2013.

Mwandishi: Bruce Amani /DPA/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman