1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Boko Haram yatangaza utawala wa Kiislamu

24 Agosti 2014

Kiongozi wa Boko Haram ameanzisha utawala wa Kiislam katika mji wa kaskazini mashariki mwa Nigeria uliotekwa na waasi mapema mwezi huu wakati ikiripotiwa polisi 35 wa Nigeria hawajulikani walipo.

https://p.dw.com/p/1D01J
Kiongozi wa Boko Haram Abubakar Shekau.
Kiongozi wa Boko Haram Abubakar Shekau.Picha: picture alliance/AP Photo

Katika ukanda wa video wa dakika 52 ambao umepatikana na shirika la habari la AFP Jumapili (23.08.2014) kiongozi wa kundi hilo Abubakar Shekau amekaririwa akimshukuru Mwenyeenzimungu kwa kuwapa ushindi ndugu zao katika mji wa Gwoza na kuufanya kuwa sehemu ya utawala wa Kiislamu.

Ametangaza kwamba kwa sasa mji huo wa Gwoza ulioko katika jimbo la Borno hauhusiki kwa njia yoyote ile na Nigeria.

Shekau ambaye ameorodheshwa kuwa gaidi wa dunia na Marekani na kuwekewa vikwazo na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa amesema " Kwa uwezo wa Allah hatutoondoka katika mji huu. Tumekuja kukaa katika mji huu."

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya kibinaadamu (OCHA) mapema mwezi huu ilithibitisha habari kwamba mji huo uko chini ya udhibiti kamili wa waasi.

Boko Haram inadhibiti ardhi kubwa

Inaaminika kwamba kundi hilo la Boko Haram pia linadhibiti maeneo mengine karibu na Gwoza kusini mwa jimbo la Borno halikadhalika sehemu kubwa ya ardhi kaskazini mwa Borno na mji mmoja katika jimbo jirani la Yobe.

Sio rahisi kubainisha hasa maeneo yalioangukia mikononi mwa waasi hao wa Kiislamu wa itikadi kali kutokana na kwamba kuna wafanyakazi wachache wa misaada katika eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria,ni hatari kufanya safari katika maeneo hayo na katika jimbo hilo ambalo limekuwa chini ya utawala wa hali ya hatari tokea mwezi wa Mei mwaka jana na pia halina mawasiliano mazuri ya mtandao wa simu za mkono.

Shambulio la bomu la Boko Haram liliouwa watu 52 mwezi wa Machi 2014 huko Maiduguri.
Shambulio la bomu la Boko Haram liliouwa watu 52 mwezi wa Machi 2014 huko Maiduguri.Picha: picture-alliance/dpa

Waatalamu wameyaelezea mafanikio ya Boko Haram katika siku za hivi karibuni kuwa hayana kifani kuwahi kushuhudiwa kabla na kwamba kundi hilo linakaribia kukamilisha ndoto yake ya kuanzisha taifa la Kiislamu litakalofuata sheria kali za Kiislamu katika eneo zima la kaskazini mwa Nigeria.

Lakini wataalamu wengi wana amini kwamba jeshi la Nigeria lina uwezo wa kutenguwa kusonga mbele huko kwa waasi hao.Wanajeshi wa Nigeria wiki hii waligoma kupelekwa Gwoza bila ya kuwa na silaha zilizo bora kwa kile kinachoonekana kwamba ulikuwa ni uasi.

Polisi 35 wa Nigeria hawajulikani walipo

Imeripotiwa kwamba polisi 35 wa Nigeria waliokuweko kwenye chuo cha mafunzo katika eneo hilo la kaskazini mashariki mwa Nigeria hawajulikani walipo kufuatia shambulio dhidi ya kituo hicho mapema wiki hii.

Polisi wa Nigeria katika doria Abuja.
Polisi wa Nigeria katika doria Abuja.Picha: Reuters

Wanamgambo wa kundi hilo walikishambulia chuo hicho kilioko nje kidogo ya mji wa Gwoza hapo Jumatano na msemaji wa polisi ya Nigeria Emmanuel Ojukwu amesema katika taarifa kwamba polisi hao 35 ambao bado hawajulikani walipo kutokana na kushambuliwa kwa kituo hicho wanaendelea kutafutwa huku kukiwa na matumaini makubwa ya kujuwa mahala walipo.

Pia ameliambia shirika la habari la AFP katika nyakati tafauti kwamba ni mapema mno kuaguwa iwapo askari hao wanashikiliwa mateka na wanamgambo hao ambao wamekuwa wakiwateka nyara mamia ya watu wakati wa uasi wao uliodumu kwa miaka mitao sasa.

Ojukwu amesema baadhi ya mateka wameuwawa na miili yao bado haikupatikana wakati wengine yumkini wakawa wamekimbia kujihifadhi wakati wa mashambulizi ya wanamgambo hao lakini hadi hivi sasa hawakuripoti mahala walipo.Amesema jeshi linajiandaa kuukombowa mji wa Gwoza.

Kundi la Boko Haram linalolaumiwa kwa kusababisha vifo vya zaidi ya watu 10,000 tokea mwaka 2009 mara kwa mara limekuwa likielekeza mashambulizi yake dhidi ya polisi na jeshi katika kipindi chote cha uasi wao.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/AP

Mhariri : Iddi Ssessanga