1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BOBs 2012: Piga kura sasa

2 Aprili 2012

Jopo la majaji wa kimataifa limetangaza majina ya blogu zilizopendekezwa kuingia katika kinyanganyiro cha tuzo ya Deutsche Welle Best of Blog Awards. Sasa ni zamu ya watu wanaoutumia mtandao wa internet.

https://p.dw.com/p/14WUI
BOBs 2012: Upigaji kura umeanza
BOBs 2012: Piga kura sasa

Kuanzia tarehe 2 Aprili, watumiaji wa mtandao wa internet watakuwa na muda wa wiki nne wa  kuzitazama blogu zilizopendekezwa kwa ajili ya tuzo za Best of Blog Awards, yaani BOBs, kwa mwaka huu. Majaji walichagua jumla ya blogu 187 kati ya 3,200 zilizopendekezwa katika mtandao.

Timu ya BOBs imeandika maelezo kwa lugha 11 juu ya blogu zilizopendekezwa kuingia katika raundi hii ili kuwapa watumiaji wa mtandao picha halisi. Jambo hili linatoa nafasi nzuri kwa mtu kujifunza zaidi kuhusu miradi yenye ubunifu na ya kishujaa iliyoko mtandaoni na ambayo imeandaliwa kwa lugha ya kigeni.

Miradi mingi yenye ubunifu na ya kishujaa

Miongoni mwa tovuti za lugha ya Kijerumani zilizopendekezwa ni tovuti yenye jina la "Wheelmap". Mradi huu unawapa watumiaji wake nafasi ya kutafuta maeneo yanayofaa kutembelewa na baiskeli za kubebea walemavu na kuyawekea alama katika ramani ya dunia. Tovuti nyingine zilizopendekezwa ni "Campact" inayowapa watumiaji nafasi ya kuandaa na kufanya kampeni na vile vile "Entschubladen", tovuti inayotumia njia ya kimichezo na ya kufurahisha kubadili dhana potofu watu walizo nazo kuhusu watu wa jinsia tofauti.

Kwa mara ya kwanza, watu wanaweza kuzipigia kura blogu zilizopendekezwa katika makundi ya makundi 17 ya tuzo hizo, kupitia mtandao wa kijamii wa Urusi uitwao "VKontakte", mtandao wa kijamii wa Kichina ujulikanao kama "Sina Weibo" na kupitia tovuti ya "Open ID", mbali na kutumia mitandao ya Facebook na Twitter iliyokuwa ikitumika awali.

Washindi wote watatangazwa mtandaoni tarehe 2 Mei
Washindi wote watatangazwa mtandaoni tarehe 2 MeiPicha: Fotolia

Jopo la majaji linalojitegemea kufanya uamuzi.

Tarehe 1 mwezi Mei mwaka huu, majaji watakutana mjini Berlin, Ujerumani, na kuwateua washindi wa makundi makuu sita. Makundi hayo yanajumuisha mitandao ya kijamii, vidio na miradi mibunifu ya kuelimisha. Makundi makuu sita hayajapangwa kwa lugha na hivyo inamaanisha kwamba watu kutoka lugha zote 11 za mashindano wanagombania tuzo ya majaji.

Washindi wote wa tuzo za BOBs watatangazwa tarehe 2 mwezi Mei. Washindi walioteuliwa na majaji wataalikwa kufika Ujerumani kwa ajili ya kushiriki katika mkutano wa kimataifa wa vyombo vya habari, Deutsche Welle Global Media Forum, na kupokea zawadi zao katika hafla itakayofanyika tarehe 26 Juni.

Mwandishi: González, Gabriel

Tafsiri: Shoo, Elizabeth

Mhariri: Yusuf, Saumu