1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biashara haramu ya maliasili yachochea vita Kongo

Mohammed Khelef18 Aprili 2015

Biashara haramu ya pembe za ndovu, dhahabu na mbao yenye thamani ya mabilioni ya dola inachochea vita vya wenyewe kwa wenyewe mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yakiyafaidisha makundi yaliyo nje.

https://p.dw.com/p/1FALT
Eneo la mgodi wa Kalimbi, mashariki mwa Kongo.
Eneo la mgodi wa Kalimbi, mashariki mwa Kongo.Picha: DW/J. van Loon

Ripoti iliyotolewa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) inasema makundi ya kihalifu yenye silaha ambayo yana mafungamano na mataifa ya nje yanahusika kwenye utoroshaji wa kiwango kikubwa cha dhahabu, madini, mbao, mkaa, na pembe za ndovu, biashara ambayo kwa mwaka huingiza hadi dola bilioni 1.3.

Mapato yatokanayo na biashara hiyo yanayafadhili makundi 25 yenye silaha, ingawa wengine wanasema makundi hayo yanafikia 49, na ambayo yanachochea migogoro kwenye eneo la mashariki ambalo tangu hapo limeshasambaratishwa kwa vita vya muda mrefu.

Kudhibiti maeneo yenye utajiri wa madini ndiyo sababu kubwa ya kuyaingiza majimbo mawili ya Kivu kwenye miongo kadhaa ya mapigano, yakipoteza maisha na makaazi ya maelfu ya raia.

Martin Kobler, mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Kongo na anayeongoza kikosi cha wanajeshi 20,000 wa kulinda amani (MONUSCO) anasema laiti rasilimali zinazopotea mikononi mwa makundi ya kigaidi zingelitumika kujenga shule, barabara na hospitali, basi mustakabali wa Wakongo ungelikuwa mzuri sana.

Dhahabu yaongoza

Sehemu kubwa kabisa ya mapato yanayoingia mikononi mwa makundi ya wahalifu wenye silaha inatokana na dhahabu, ambayo huwapatia hadi dola milioni 120 kwa mwaka. Sehemu kubwa ya mapato hayo huchukuliwa na makundi yaliyo nje ya eneo hilo masikini kabisa, huku asilimia mbili ikikisiwa kurudi kwa makundi yenye silaha, yaani dola milioni 13, ambazo hutumika kuchochea zaidi mapigano.

Mwanaharakati wa Kikongo akiandamana kudai serikali iwapatie maji katika nchi ambayo ina kila aina ya utajiri wa madini.
Mwanaharakati wa Kikongo akiandamana kudai serikali iwapatie maji katika nchi ambayo ina kila aina ya utajiri wa madini.Picha: D.Kannah/AFP/Getty Images

Mapato haya yanawakilisha gharama halisi kwa ajili ya kiasi cha wapiganaji 8,000 wenye silaha kwenye eneo hili kwa mwaka, na pia kuyawezesha makundi yaliyoshindwa au kunyang'anywa silaha, kuibuka tena na hivyo kuendelea kulifanya eneo hilo lisiwe na utulivu, kwa mujibu wa ripoti hiyo.

Makundi ya kihalifu yanatumia fedha yanazopata kuendeleza mkakati wa "wagawe uwatawale" miongoni mwa makundi yenye silaha ili kuhakikisha kuwa hakuna kundi moja peke yake linaloweza kuimiliki na kuiendesha biashara hiyo.

Kongo ina kiwango kikubwa sana cha madini, ikiwemo dhahabu, shaba, chuma, almasi, na hata uranium, lakini sehemu kubwa ya raia wake wanaishi kwenye umasikini wa kutupwa.

Fedha zinapotea kiholela

"Hebu fikiria, laiti tungeliweza kutumia mamilioni ya dola yanayopotea kwenye mapato yanayoibiwa na makundi ya kihalifu mashariki mwa Kongo kuwalipa walimu, madaktari na kuinua fursa za kibiashara na utalii," anasema Kobler, akiongeza kwamba "Tunapaswa kuigeuza dhahabu kuwa kodi, na kodi kuwa maendeleo kwa ajili ya mustakabali wa watu."

Sehemu kubwa ya harakati za waasi zinahusisha udhalilishaji raia na usafirishaji haramu wa maliasili, huku waasi hao wakionekana kuchochewa zaidi katika kujinufaisha kiuchumi basala ya kuwa na ajenda ya kisiasa.

Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa inasema kuwa mitandao ya makundi hayo ya kihalifu ina mashiko yake ndani ya Kongo yenyewe - kama vile Kivu ya Kaskazini na Kusini - na hata mataifa jirani, kama vile Uganda, Rwanda, Burundi na Tanzania.

Kwa mujibu wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP, si madini pekee yaliyo hatarini kwenye vita hivi, bali pia wanyamapori, wakiwemo sokwe wa milimani wanaokutikana katika Hifadhi ya Taifa ya Virunga na walinzi wa wanyama hao.

Ndani ya kipindi cha miaka mitano iliyopita, zaidi ya walinzi 200 wameshauawa na kundi ya kihalifu, hasa wanaofanya biashara ya mkaa.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Sekione Kitojo