1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern yaishinda CSKA Moscow bila mashabiki

1 Oktoba 2014

Penalti iliyofungwa na Thomas Müller iliwapa Bayern Munich ushindi wa goli moja kwa sifuri ugenini dhidi ya CSKA Moscow. Mechi ilichezwa katika uwanja mtupu kutokana na vikwazo vya UEFA dhidi ya wenyeji.

https://p.dw.com/p/1DOG3
Fußball UEFA Champions League Bayern München CSKA Moskau
Picha: AFP/Getty Images/A. Nemenov

Ushindi wa Bayern Munich wa goli moja kwa sifuri dhidi ya CSKA Moscow katika Kundi E la Champions League haukuwa wa kukumbukwa hasa kwa matukio ya michezo: safu ya imara ya ulinzi ya CSKA ilihimili shambulizi moja baada ya jingine kutoka kwa washambuliaji wa Bayern Robert Lewandoswski, Mario Götze, Thomas Müller na Arjen Robben, wakati nayo mashambulizi ya kujibu ya CSKA yakionekana kuwa hafifu hata yasiweze kusababisha kitisho chochote.

Kando na penalty iliyofungwa na Müller katika dakika ya 22, jambo la kushangaza zaidi katika mechi hiyo huenda likawa ni kile kilichokuwa kikifanyika au kutofanyika katika viti vya mashabiki.

Vikwazo vya UEFA dhidi ya klabu hiyo ya Moscow vilimaanisha kuwa hakuna shabiki yeyote aliyekubaliwa uwanjani. Vurugu za mashabiki katika mchuano wao wa ufunguzi dhidi ya klabu ya Jamhuri ya Czech, Viktoria Plzen msimu uliopita ndizo sababu ya vikwazo hivyo,na ni idadi ndogo tu ya watu iliyoruhusiwa– wengi wao waandishi wa habari na maafisa wa timu – waliokubalika kuingia katika uwanja wa Khimki mjini Moscow.

UEFA Champions League Bayern München CSKA Moskau leere Tribüne
UEFA iliwapoga marufuku mashabiki kuingia uwanjani kufuatia tukio la vurugu mwaka wa 2013Picha: picture-alliance/dpa/P. Kneffel

Baadhi ya mashabiki walikusanyika nje ya milango ya uwanja huo, wakiimba nyimbo ambazo zilisikika kwa umbali ndani ya uwanja wenyewe. Mwishoni mwa mechi, makundi madogo ya watu – labda wageni wa wahisani wa mchuano huo – waliungana na wenzao nje ya uwanja.

Ushindi huo ndio wa 100 wa Bayern Munich katika Champions League na ni wao wa pili kutokana na mechi mbili za hatua ya makundi katika msimu huu. CSKA wamepoteza mchuano wao wa pili katika Kundi E baada ya kubumburushwa magoli matano kwa moja wiki mbili zilizopita na AS Roma ya Italia.

Manchester City ilitoka sare ya goli moja kwa moja na Roma katika mpambano mwingine wa Kundi E. BAYERN inaongoza kundi hilo na points sita, ikifuatwa na Roma na points nne. Manchester City ni ya tatu na point moja huku CSKA ikishika mkia bila chochote.

Mchuano ujao wa Bayern katika awamu ya makundi ni ugenini dhidi ya Roma mnamo Oktoba 21. Nayo CSKA Moscow itaialika Manchester City siku hiyo hiyo.

Mwandishi: Bruce Amani/DW
Mhariri: Mohammed Khelef