1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern washerehekea ubingwa mjini Munich

25 Mei 2015

Baada ya patashika za ligi kumalizika, takribani mashabiki 15,000 wa Bayern Munich walijitokeza kuwaona mashujaa wao wa timu za wanaume na wanawake wakiyaonyesha mataji yao ya Bundesliga.

https://p.dw.com/p/1FWBe
Meisterfeier 1. FC Bayern München Rathaus
Picha: picture-alliance/dpa/A. Hassenstein

Mwenyekiti wa Bayern Karl-Heinz Rummenige alisema haijawahi kutokea kuwa timu mbili za klabu klabu moja ziliwahi kupata taji hilo kwa wakati mmoja.

Bayern Munich walidhihirisha umahiri wao kama mabingwa wa Ujerumani kwa mara ya 25 msimu huu lakini Wolfsburg na Borussia Moenchenglabach ziliibuka kuwa wapinzani wao wa karibu.

Borussia Dortmund waliwabandua Bayern katika Kombe la Shirikisho lakini wao wenyewe walikuwa na mwanzo mbaya wa msimu. Sasa wanaweza kujiliwaza na kandanda la Europa league baada ya kumaliza katika nafasi ya saba.

Kuyumba kwa BVB kuliweka pengo nyuma ya Bayern, ambalo lilijazwa na makamu bingwa Wolfsburg na Borussia Moenchengladbach, ambao wamekuwa na msimu wa kufana chini ya kocha Lucien Favre.

Bayer Leverkusen walimaliza katika nafasi ya nne na wataingia katika ligi ya klabu bingwa Ulaya katika hatua ya mechi za mchujo. Augbrug ilitinga katika jukwaa la Ulaya kwa mara ya kwanza katika historia yao baada ya kuumaliza msimu katika nafasi ya tano. Wameungana na Schalke ambao walimaliza katika nafasi ya sita.

Hoffenheim na Eintracht Frankfurt, ambayo ilikuwa na mfungaji wa mabao mengi Alexander Meier na magoli 19, zilimaliza katika nusu ya juu ya msimamo wa ligi.

Werder Bremen ilimaliza ya kumi wakati nayo FC Cologne ikimaliza katika nafasi ya 12 mbele ya Mainz kwa tofauti ya mabao. Hanover, Stuttgart na Hertha Berlin zilinusurika shoka la kushushwa daraja.

Mwandishi: Bruce Amani
Mhariri: Yusuf Saumu