1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern kuumiza nyasi na Dortmund

31 Oktoba 2014

Katika miaka michache iliyopita, mechi kati ya Bayern Munich na Borussia Dortmund zilikuwa mechi kali sana za misimu ya Bundesliga. Dortmund kwa kawaida iliibuka kidedea, hata kama Bayern mwishowe ingeunyakuwa ubingwa

https://p.dw.com/p/1DfCd
Fußball Supercup Borussia Dortmund - Bayern München
Picha: Getty Images

Msimu huu, ni Borussia nyingine, ile inayotoka Mönchengladbach, ambayo inaonekana kuwa mpinzani wa karibu wa Bayern, baada ya kuwakaba mabingwa hao watetezi kwa kutoka sare ya kutofungana goli wiki iliyopita.

Dortmund kwa upande mwingine, inaendelea kuyumbayumba katika upande wa mkia wa ligi baada ya kuwa na mwanzo mbaya sana wa msimu. Kwa sasa vijana hao wa kocha Jügen Klopp wako nyuma ya viongozi Bayern na pengo la points 14 na wanakabiliwa na kibarua kikali cha kujaribu kupanda juu ya msimamo wa ligi na kufikia nafasi za kufuzu katika Champions League.

Na hii leo, Dortmund watacheza ugenini dhidi ya Bayern ambapo kocha Klopp anasema kuwa hayuko tayari kusalimu amri "Tutajitahidi sana ili kukabiliana na ubora wa Bayern. Hilo ni wazi na hatuwezi kulipuuza. Tunafahamu kuwa tuna ujuzi wa kuwatatiza Bayern. Na tukifaulu hilo basi tutaufungua mlango mpya. Na tukiweza kupita katika mlango huo tutakuwa katika upande ulio salama".

Fußball 1. Bundesliga 7. Spieltag FC Bayern München vs. Hannover 96
Arjen Robben anatarajiwa kuwa mwiba katika safu ya ulinzi ya DortmundPicha: REUTERS/L. Barth

Huku wakikabiliwa na matatizo ya msusuru wa majeraha, Dortmund wameshindwa mechi zake nne za mwisho katika Bundesliga. Bayern nao wameanza msimu kwa kusajili ushindi wa mechi sita na kutoka sare mara tatu.

Na Klopp anasema wataingia uwanjani Allianz Arena kwa ujasiri mkubwa. "Kwa bahati mbaya, hatuna tatizo la kujivunia mafanikio kwa wakati huu, na tunasalia kuwa hivyo kwa sababu hatuna mafanikio yoyote. Lakini hata hivyo, katika mchuano huu tutaonyesha heshima yetu katika namna tunavyocheza".

Arjen Robben ni mchezaji anayetarajiwa kuwasababishia Dormtund matatizo katika lango lao. Ili kujaribu kulijaza pengo la majeruhi, kocha wa Dortmund amekuwa akiwatumia kwa mzungumzo washambuliaji wake watatuCiro Immobile, Pierre-Emerick Aubameyang na Adrian Ramos.

Kando na Bayern, timu nyingine ambazo hazijashindwa mechi yoyote msimu huu ni Monchengladbach na Hoffenheim. Timu hizo mbili pamoja na Wolfsburg, ziko nyuma ya Bayern na tofauti ya points 4.

Mchuano wa Jumapili mjini Monchengladbach utakuwa wa kukata na shoka. Timu zote mbili zinacheza soka la kuvutia, la mashambulizi makali na zote zimepata ushindi katika mechi za katikati ya wiki za Kombe la Shirikisho la Kandanda Ujerumani - DFB

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri:Josephat Charo