1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la Usalama laidhinisha azimio kuhusu Syria

28 Septemba 2013

Baraza lausalama la Umoja wa Mataifa limeidhinisha azimio jana(27.09.2013)linalotaka kuondolewa kabisa kwa silaha za sumu za Syria lakini halitishii kuchua hatua za kijeshi dhidi ya serikali hiyo iwapo haitatekeleza.

https://p.dw.com/p/19pnn
Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa jijini New York
Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa jijini New YorkPicha: Getty Images

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limeidhinisha azimio jana Ijumaa(27.09.2013)ambalo linataka kuondolewa kabisa kwa silaha za sumu nchini Syria lakini halitishii kuchukuliwa hatia za kuiadhibu serikali ya rais Bashar al-Assad iwapo haitatekeleza.

Kura hiyo ambayo imepigwa kwa kauli moja na wajumbe wote 15 wa baraza la usalama imefikisha kilele wiki kadha za majadiliano ya kidiplomasia kati ya Urusi na Marekani. Ilikuwa katika msingi wa makubaliano kati ya nchi hizo mbili yaliyofikiwa mjini Geneva mapema mwezi huu kufuatia shambulio la gesi ya sarin Agosti 21 mwaka huu katika kitongoji kimoja cha mji wa Damascus ambapo mamia ya watu wameuwawa.

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Urusi Sergei LavrovPicha: Getty Images

Makubaliano ya Urusi na Marekani

Makubaliano kati ya Urusi na Marekani yameepusha hatua za kijeshi dhidi ya serikali ya Assad, ambapo serikali ya Marekani inaishutumu kwa shambulio la hapo Agosti. Serikali ya Syria na mshirika wake, Urusi , wanawalaumu waasi wanaopambana na serikali kwa shambulio hilo. Sehemu moja ya azimio hilo , lilielezewa na wanadiplomasia wa baraza hilo kuwa ni muhimu, linaidhinisha mpango kwa mpito wa kisiasa nchini Syria uliokubalika katika mkutano wa kimataifa mjini Geneva Juni mwaka 2012. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema baada ya kura hiyo kuwa mataifa makubwa yanamatumaini ya kufanya mkutano wa amani kwa ajili ya Syria katikati ya mwezi Novemba mjini Geneva.

Ameliambia baraza hilo kuwa mpango wa kuondoa silaha za sumu za Syria , "sio leseni ya kuuwa kwa silaha nyingine." "Wakati tukifikia hatua hii muhimu, hatupaswi kusahau kuwa maovu yaliyotendeka nchini Syria yanaendelea kwa mabomu na vifaru, maguruneti na bunduki," amesema. "Kuzuwia aina fulani ya silaha sio ruhusa ya nyingine." Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry amesema kuwa kura hiyo inaonesha kuwa "Hatua zina matokeo yake."

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amesema azimio la Syria ni la kutia moyo
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amesema azimio la Syria ni la kutia moyoPicha: Reuters

"Lengo letu kuu lilikuwa kuondoa na kuzuwia uwezo wa silaha za sumu nchini Syria. Na uwezekano wa matumizi ya nguvu za jeshi ambazo rais Obama amesiwasilisha zingeweza kutimiza lengo hilo. Lakini leo hii azimio hili linatimiza hata zaidi, kupitia njia za amani, litaweza kutoa kwa mara ya kwanza kuondoa kabisa uwezo wa nchi hiyo wa silaha za sumu," amesema. Azimio hilo haliruhusu kuchukuliwa hatua za moja kwa moja za kuiadhibu kijeshi ama kwa vikwazo serikali ya Syria iwapo haitatekeleza. Kwa msisitizo wa Urusi, azimio hilo linaweka wazi uamuzi wa pili wa baraza hilo kuwa utahitajika kwa ajili hiyo.

Urusi yatoa masharti

Lakini waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov amesema kuwa baraza la usalama litakuwa tayari kuchukua hatua iwapo kutakuwa na ukiukaji wa azimio hilo uliothibitishwa na upande wowote wa mzozo huo. "Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litakuwa tayari kuchukua hatua chini ya ibara ya 7 ya katiba ya umoja wa Mataifa, kwa uwazi kabisa," amesema. Kikwazo kikubwa katika azimio hilo kilikuwa upinzani wa Urusi katika kuliandika chini ya ibara hiyo ya 7 ya mkataba wa Umoja wa Mataifa, ambao unalipa baraza hilo mamlaka ya kuchukua hatua kutokana na maamuzi yake kwa kuweka vikwazo ama nguvu za kijeshi.

Urusi imeweka wazi , hata hivyo kuwa haitaunga mkono matumizi ya kijeshi dhidi ya serikali ya Assad , mnunuzi mkuu wa silaha za Urusi. Balozi wa Syria katika Umoja wa Mataifa , Bashir Ja'afari, amesema Uturuki , Saudi Arabia, Ufaransa, Qatar na Marekani zinapaswa kukubaliana na azimio hilo na ziwajibishwe iwapo zitaendelea kuwapa misaada waasi, ambao wanashutumiwa na serikali ya Assad kuwa walitumia gesi hiyo ya sumu dhidi ya jeshi la nchi hiyo.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre

Mhariri: Bruce Amani