1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ban Ki-moon akutana na Maliki

24 Julai 2014

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekutana na viongozi wa juu wa Iraq akiwataka waukwamue mkwamo wa siasa katika wakati ambapo mashambulizi ya kigaidi yakiangamiza maisha ya zaidi ya watu 60.

https://p.dw.com/p/1CiT8
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon.Picha: Reuters

Msemaji wa Ban Ki-moon amesema Katibu huyo Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekutana na Ayatullah al-Sistani katika mji wa Najaf kwa kile alichokiita "kutafuta busara zake kwenye mwenendo wa mambo nchini Iraq."

Kwa zaidi ya muongo mzima sasa, Ayatullah al-Sistani amesitisha ushiriki wake wa moja kwa moja kwenye siasa, lakini amejtokeza katika siku za hivi karibuni akitaka wanasiasa waichaguwe serikali mpya bila kuchelewa.

Ushawishi wake unachukuliwa kuwa ni muhimu katika kumuondosha madarakani Waziri Mkuu Nuri al-Maliki, anayeshutumiwa kwa kuwatenga raia wa madhehebu ya Sunni, na hivyo kurahisisha ushindi wa kundi la waasi la Dola ya Kiislamu kaskazini na magharibi mwa nchi hiyo.

Bunge lamchagua rais

Tayari hivi leo, bunge limemchagua Fuad Masum kuwa rais wa serikali ya shirikisho, hatua inayofungua njia kwa ajili ya uundwaji wa serikali mpya. Masum, ambaye ni Mkurdi, anachukuwa nafasi ya Jalal Talabani, ambaye alirejea nchini siku tano zilizopita baada ya kuwapo Ujerumani kwa miezi 18 akitibiwa.

Aliyekuwa Rais wa Iraq, Jalali Talabani.
Aliyekuwa Rais wa Iraq, Jalali Talabani.Picha: Getty Images

Kwa mujibu wa makubaliano yasiyo rasmi, Kurdistan kila siku ndiyo inayokalia kiti cha urais wa Iraq, tangu kupinduliwa na hatimaye kuuawa kwa Saddam Hussein zaidi ya muongo mmoja sasa.

Mashambulizi dhidi ya wafungwa

Wakati hayo yakiendelea, watu wapatao 60 wameuawa kaskazini mwa mji mkuu Baghdad, baada ya watu wenye silaha kuuvamia msafara wa wafungwa na kukabiliana na wanajeshi. Kwa mujibu wa maafisa wa serikali, wafungwa 52 wameuawa, wanajeshi wanane na huku wafungwa wengine saba na wanajeshi wanane wakijeruhiwa.

Bado haijafahamika ni nani waliohusika na mashambulizi hayo, ambayo yalianza kwa kuripuka kwa mabomu yaliyotegwa kando ya barabara, lakini kundi la Dola ya Kiislamu linatuhimiwa.

Katika mji wa kaskazini wa Mosul, unaodhibitiwa na kundi hilo, Umoja wa Mataifa umesema wanawake wote wenye umri wa kati ya miaka 11 na 40 wameamriwa kutahiriwa.

Wapiganaji wa kundi la Dola ya Kiislamu wanaotuhumiwa kutoa fatwa ya kuwatahiri wanawake.
Wapiganaji wa kundi la Dola ya Kiislamu wanaotuhumiwa kutoa fatwa ya kuwatahiri wanawake.Picha: AFP/Getty Images

Mratibu wa masuala ya kibinaadamu wa Umoja huo, Jacqueline Badcock, amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva, kwamba fatwa hiyo inawagusa wanawake na wasichana milioni 4, katika eneo ambalo halina utamaduni huo.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari mara tu baada ya kuwasili Baghdad, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, alilaani fatwa hiyo na pia unyanyasaji unaofanywa dhidi ya Wakristo na jamii nyengine za wachache katika maeneo yanayoshikiliwa na makundi yenye silaha.

Zaidi ya watu milioni mbili wamekimbia makaazi yao katika wimbi la hivi karibuni la machafuko, na Umoja wa Mataifa unasema familia nyengine 400 ziliwasili siku ya Jumapili kwenye miji miwili ya jimbo lenye utawala wa ndani la Kurdistan.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Sekione Kitojo